PDPC YATOA MIEZI MITATU YA NYONGEZA USAJILI, TAASISI ZAONYWA UKAGUZI MKALI WAANZA APRILI


Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imetoa miezi mitatu ya nyongeza kwa taasisi zote za umma na binafsi zinazokusanya au kuchakata taarifa binafsi kukamilisha usajili wao kwa hiari.

Hatua hiyo inalenga kutoa nafasi ya mwisho kwa taasisi kujirekebisha kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa maagizo ya Serikali, Mkurugenzi wa PDPC, Dr Emmanuel Lameck Mkilia, amesema nyongeza hiyo inaanza Januari 8 hadi Aprili 8, 2026.

Amesema uamuzi huo umetokana na maelekezo ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb.).

Dr Mkilia amesisitiza kuwa dirisha hilo halimaanishi kusitishwa kwa utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44.

Badala yake, amesema ni fursa ya mwisho kwa taasisi kuhakikisha zinazingatia sheria kabla ya kuanza kwa ukaguzi mkali.

Ameeleza kuwa kuanzia Aprili 8, 2026, PDPC itaanza kufanya ukaguzi wa taasisi zote zinazokusanya, kuhifadhi, kuchakata au kusafirisha taarifa binafsi.

Amesema taasisi zitakazobainika kukiuka sheria zitakabiliwa na adhabu kali ikiwemo faini, kifungo au vyote kwa pamoja.

Pia, amesema wakiukaji wanaweza kuamriwa kulipa fidia kwa waathirika wa ukiukwaji wa faragha.

Katika hatua nyingine, Dr Mkilia amesema PDPC itaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Wiki ya Faragha na Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

Maadhimisho hayo yatafanyika kuanzia Januari 26 hadi 30, 2026.

Amesema lengo ni kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki ya faragha na wajibu wa taasisi katika uchumi wa kidijitali.

PDPC imezitaka taasisi kuchangamkia fursa hiyo ili kuepuka athari za kisheria zitakazoanza mara baada ya muda wa nyongeza kumalizika.