Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kinondoni imeanza msako wa kuwatafuta Alex Msama na Benny Sammoh ili wajibu mashtaka yanayohusisha uhalifu wa kifedha.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo Alhamisi, Januari 22, 2026, Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kinondoni, Elizabeth Mokiwa, amesema washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi, yakiwemo kuongoza genge la uhalifu, kughushi nyaraka, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji fedha.
Mashitaka hayo ni kupitia shauri la uhujumu uchumi Na. 1371/2026, lililofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Januari 21, 2026.
“Washtakiwa Alex Msama na Benny Sammoh wanatafutwa ili wafikishwe mahakamani kujibu mashtaka ya uhujumu uchumi ikiwemo kuongoza genge la uhalifu, kughushi nyaraka, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu pamoja na utakatishaji fedha,” amesema Mokiwa.
Mokiwa amefafanua kuwa shauri hilo limetokana na uchunguzi wa tuhuma zinazohusiana na kiwanja namba 33, kilichopo Vijibweni, Kigamboni, mkoani Dar es Salaam, chenye Hati Na. 129621 iliyotolewa kwa kampuni ya Africa Energy Limited mwaka 2013.
Kwa mujibu wa Mokiwa, uchunguzi umebaini kuwa washtakiwa hao walighushi hati ya mauziano ya kiwanja hicho na kuwasilisha nyaraka hizo katika Baraza la Ardhi la Wilaya ya Temeke, wakionyesha kuwa Benny Sammoh alinunua kiwanja hicho kutoka kwa Mwinyikombo Wahela, jambo ambalo si la kweli.
“Baada ya kuwasilisha nyaraka hizo za kughushi, Benny Sammoh, kwa kutumia jina lingine la Ben Samson, alifanikiwa kuuza kiwanja hicho kwa kampuni ya World Oil Tanzania Limited,” amesema.
Ameongeza kuwa kupitia mauzo hayo, Benny Sammoh alijipatia jumla ya Sh984 milioni, kati ya Sh1.7 bilioni zilizokuwa zimeainishwa kwenye mkataba wa mauzo.
“Ushahidi unaonesha kuwa kati ya fedha hizo, Sh370 milioni kilihamishwa kwenda kwa Alex Msama kama sehemu ya fedha zilizotokana na mauzo ya kiwanja hicho,” ameeleza Mokiwa.
Mokiwa amesema uchunguzi huo umefanywa kwa ushirikiano wa maofisa wa Takukuru kutoka mikoa ya Kinondoni na Temeke na baada ya kukamilika, washtakiwa waliitwa kuripoti ofisini Desemba 2025 kwa ajili ya kufikishwa mahakamani, lakini walishindwa kutekeleza agizo hilo.
“Jitihada mbalimbali za kuwataka wafike ofisini hazikuzaa matunda, hivyo tumeanza kuwatafuta rasmi. Hati za kuwakamata zimeshatolewa na Mahakama ya Kisutu Januari 21,2026,” amesema.
Amesema shauri hilo linatarajiwa kutajwa tena mahakamani hapo Februari 25, 2026, huku Takukuru ikiomba ushirikiano wa wananchi katika kuwabaini watuhumiwa hao.
“Mwananchi yeyote mwenye taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa washtakiwa hawa anashauriwa kutoa taarifa kwenye ofisi yoyote ya Takukuru au kupiga simu namba 0738 150236. Zawadi nono itatolewa kwa atakayetoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwao,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Mokiwa amesema Alex Msama anatafutwa pia na Takukuru Mkoa wa Kinondoni kwa ajili ya kujibu tuhuma nyingine za kughushi nyaraka na uvamizi wa kiwanja namba 234, kilichopo Regent Estate, Mikocheni, wilayani Kinondoni.
Akitoa onyo, Mokiwa amewataka watumishi wa umma kuepuka kushiriki vitendo vinavyowezesha watu kujipatia umiliki wa ardhi kwa njia ya udanganyifu.
“Tunatoa tahadhari kwa watumishi wa umma kutoshiriki vitendo vya rushwa au kusaidia watu kujipatia viwanja kwa njia zisizo halali,” amesema.
Pia, amewataka wananchi kuwa makini kabla ya kununua viwanja, hasa vilivyopo katika maeneo ya kimkakati, na kuendelea kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa.