Wengi huenda wanamfahamu zaidi katika ulimwengu wa kisiasa lakini ni miongoni mwa watu wenye mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania, huenda kile tunachokiona leo katika uchumi wa Tanzania kwa namna moja ama nyingine, kwa ukubwa au udogo kimechangia na juhudi, maarifa na maono yake.
Edwin Mtei ambaye amefariki Januari 20, 2026 akiwa na umri wa miaka 94 ni miongoni mwa wataalamu wachache wa fedha na uchumi waliokuwa na nafasi ya kipekee katika historia ya Tanzania, si tu kama mtendaji mkuu wa taasisi muhimu, bali pia kama mshauri wa sera aliyeona mbali kuliko wakati wake.
Akiwa Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na baadaye Waziri wa Fedha na Mipango, Mtei alijikuta katikati ya uamuzi mgumu wa kiuchumi yaliyochagiza mwelekeo wa taifa katika miaka ya mwanzo ya uhuru.
Msingi wa kuanzishwa kwa BoT
Kabla ya kuanzishwa kwa Benki Kuu ya Tanzania mwaka 1966, Tanganyika, Kenya na Uganda zilikuwa zinatumia sarafu moja iliyosimamiwa na East African Currency Board (EACB), chombo kilichoanzishwa mwaka 1919 wakati wa utawala wa kikoloni.
Kazi kuu ya EACB ilikuwa kudhibiti na kusimamia sarafu katika mikoa hiyo. Kwa maneno mengine, EACB ilihakikisha kuwa sarafu iliyotumika katika eneo la Afrika Mashariki ilikuwa inategemewa, inathibitishwa na ina thamani thabiti.
EACB iliundwa na serikali ya kikoloni ya Uingereza kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Uingereza (Bank of England).
Ingawa EACB ilitekeleza baadhi ya majukumu ya benki kuu, haikutoa mamlaka kamili ya sera za fedha kwa serikali za nchi wanachama.
Baada ya Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961, matarajio ya uongozi wa kisiasa yalielekezwa katika kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki, ambalo lingeunda serikali moja ya shirikisho na benki kuu moja.
Hata hivyo, ilipofika mwaka 1963, ilibainika kuwa matarajio hayo hayakuwa na msingi wa haraka.
Tofauti za kisera na vipaumbele vya kiuchumi kati ya Kenya, Uganda na Tanganyika zilifanya iwe vigumu kuendelea na sarafu ya pamoja bila kuwa serikali ya pamoja.
Katika mazingira hayo, uamuzi wa kuanzisha benki kuu za kitaifa ulionekana kuwa wa lazima kwa kila nchi ili kudhibiti sera zake za fedha kulingana na mahitaji yake ya ndani.
Uteuzi wa Mtei na maandalizi ya taasisi
Wakati uamuzi huo unafikiwa, Edwin Mtei alikuwa Katibu Mkuu wa Hazina, nafasi iliyomweka moja kwa moja katika majadiliano ya kikanda kuhusu mustakabali wa EACB.
Alishiriki katika mazungumzo ya kugawanya mali na majukumu ya bodi hiyo, na hatimaye mwezi Februari 1965, Mawaziri wa Fedha wa nchi tatu katika mkutano wa Entebbe walikubaliana kila nchi ianzishe benki kuu yake ifikapo katikati ya mwaka 1966.
Katika mkutano huo wa Entebbe, ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Nsilo-Swai, Waziri wa Mipango ya Maendeleo, ambaye alikuwa Kaimu Waziri wa Fedha kwa kuwa Waziri wa Fedha, Paul Bomani, alikuwa mgonjwa.
Oktoba 1965, Mwalimu Julius Nyerere alimteua Mtei kuwa Gavana-Mteule wa Benki Kuu ya Tanzania. Alhamisi ya Januari 6, 1966 Rais Nyerere alitia saini Sheria ya Benki ya Tanzania, na hivyo kumfanya Mtei kuwa Gavana rasmi kuanzia tarehe hiyo.
Uteuzi huo ulimkuta Mtei akiwa na umri wa miaka 33 tu, jambo lililomfanya kuwa mmoja wa magavana wachanga zaidi wa benki kuu barani Afrika wakati huo.
Licha ya umri wake mdogo, uteuzi huo uliakisi imani kubwa ya Rais katika uwezo wake wa kitaalamu, nidhamu ya kazi na uwezo wa kushirikiana na wataalamu wa kimataifa.
Mtei alianza kazi mara moja kwa kukusanya timu ya wataalamu kutoka nchi mbalimbali kwa ushirikiano na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Gunnar Akermalm kutoka Benki Kuu ya Sweden aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu, huku wataalamu wengine wakitoka Benki ya England, Norway, Denmark na India.
Timu hiyo ilifanya kazi ya kuandaa sheria, taratibu za uendeshaji na mifumo ya mafunzo kwa Watanzania waliokuwa wanaingia katika taasisi hiyo mpya.
Sheria ya Benki Kuu na mwanzo wa shughuli
Kazi muhimu zaidi katika awamu ya maandalizi ilikuwa kuandaa Muswada wa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania.
Timu ya IMF iliyoongozwa na Jan Mladek ilifika Tanzania Novemba 1965 na kwa ushirikiano wa karibu na Mtei na Akermalm, iliandaa muswada huo ndani ya kipindi kifupi cha takribani wiki moja.
Bunge liliupitisha muswada huo Desemba 1965, na Rais Nyerere alitia saini Januari 1966, hatua iliyowezesha Benki Kuu ya Tanzania kuanza kazi rasmi.
Jukumu kubwa la kwanza lilikuwa kubadilisha sarafu ya Afrika Mashariki ‘East African Shilling’ na kuanzisha shilingi ya Tanzania.
Hili lilihitaji maandalizi ya kina, kuanzia uchapishaji wa noti na utengenezaji wa sarafu, hadi usafirishaji na usambazaji wake nchi nzima.
Mtei alihakikisha kuwa noti na sarafu zilitengenezwa kwa viwango vya juu, zikiwa na alama na maandishi yaliyokubalika kitaifa.
Ushirikiano na Royal Mint ya Uingereza na kampuni ya Thomas de la Rue ulihakikisha kuwa sarafu mpya ilipatikana kwa wakati.
Sarafu za kwanza zilifika Dar es Salaam Machi 1966 na kuhifadhiwa kwa ulinzi maalumu, huku noti zikianza kuwasili mwishoni mwa Aprili ya mwaka huo.
Kabla ya uzinduzi rasmi, sarafu mpya zilihamishwa hadi matawi ya benki za kibiashara kote nchini ili kuhakikisha upatikanaji wake mara moja kwa wananchi.
Uzinduzi na mafanikio ya awali
Benki Kuu ya Tanzania ilizinduliwa rasmi na Mwalimu Nyerere Jumanne ya Juni 14, 1966. Katika hotuba yake, Rais alieleza kuwa ingawa hatua hiyo ilionekana kama kurudi nyuma kutoka kwenye azma ya ushirikiano wa Afrika Mashariki, ilikuwa muhimu kwa taifa huru kuwa na udhibiti kamili wa sera zake za fedha.
Uzinduzi huo uliambatana na kubadilisha rasmi sarafu, ambapo viongozi wakuu wa serikali na wananchi walibadilisha fedha zao siku hiyohiyo.
Mchakato wa kubadilisha sarafu ulifanikiwa kuliko ilivyotarajiwa. Wananchi walionyesha hamasa kubwa kuona na kutumia sarafu mpya, na ndani ya miezi michache, sehemu kubwa ya noti za zamani ilikuwa imekusanywa.
Katika maeneo ya mpakani, ubadilishaji uliendelea kwa muda mrefu kutokana na uhusiano wa kibiashara na nchi jirani.
Sambamba na hilo, BoT ilianza kujenga mahusiano ya kimataifa kwa kufungua akaunti na kupanga mifumo ya malipo na benki za nje.
Chini ya uongozi wa Mtei, Benki ilihakikisha kuwa akiba ya fedha za kigeni ilisimamiwa kwa ufanisi, ikiwa ni pamoja na kuwekeza fedha katika masoko ya London na New York ili kupata riba hata kwa uwekezaji wa muda mfupi.
Ujenzi wa makao makuu ya Benki
Baada ya kuimarisha shughuli za awali, Mtei alielekeza nguvu katika ujenzi wa jengo la kudumu la makao makuu ya Benki Kuu.
Mtaalamu wa usanifu majengo, H. L. Shah (Sukhi) alichaguliwa baada ya mchakato uliokuwa na mvutano wa kisiasa, lakini uongozi wa Benki ulisimama imara katika uamuzi huo.
Mwananchi Engineering & Contracting Company (MECCO), kampuni iliyoanzishwa kwa juhudi za TANU, ikaibuka mshindi wa zabuni.
Jengo hilo lilifunguliwa rasmi Jumatatu ya Julai 7, 1969, likiwa limegharimu takribani shilingi milioni 11.
Lilikuwa ishara ya mamlaka, uthabiti na uhuru wa sera za fedha za Tanzania. Licha ya kuungua kwa moto mwaka 1984, muundo wake wa kipekee umeendelea kuwa alama muhimu ya historia ya fedha nchini.
Mtei na mijadala ya sera za uchumi
Tangazo la Azimio la Arusha mwaka 1967 liliweka Tanzania katika mkondo wa ujamaa na udhibiti mkubwa wa serikali katika uchumi.
Mtei, akiwa Gavana wa Benki Kuu, alihusika moja kwa moja katika mijadala ya awali na alitoa tahadhari kuhusu athari za muda mrefu za baadhi ya hatua zilizopendekezwa.
Alisisitiza umuhimu wa usimamizi bora, kulinda uzalishaji na kuhakikisha fidia ya haki kwa mali zilizotaifishwa.
Hofu zake zilihusu hasa kutoroshwa kwa mtaji, upungufu wa fedha za kigeni na hatari ya kushuka kwa uzalishaji.
Ingawa alishiriki katika kuanzisha udhibiti wa fedha za kigeni ili kulinda akiba ya taifa, sera hizo baadaye zilichangia kuibuka kwa soko la magendo ya fedha.
Changamoto za kiuchumi na uongozi wa BoT
Katika kipindi cha uongozi wake, Tanzania ilikabiliwa na kushuka kwa uzalishaji wa mazao ya biashara, uendeshaji usio na tija wa mashirika ya umma, mfumuko wa bei na uhaba wa bidhaa za matumizi.
Mtei alitumia majukwaa mbalimbali kuelezea athari za sera hizo na umuhimu wa nidhamu ya kifedha, ingawa ushauri wake haukupata uzito mkubwa katika mazingira ya kisiasa ya wakati huo.
Baada ya kuondoka BoT na kuhamia Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1974 na baadaye kurejea kama Waziri wa Fedha mwaka 1977, Mtei alijikuta tena katika kiini cha mjadala mkali wa sera, hasa katika mazungumzo na IMF mwaka 1979.
Tofauti zake na Rais Nyerere kuhusu kupunguza thamani ya shilingi na mageuzi ya kiuchumi zilimfanya ajiuzulu, tukio lililoashiria mgongano mkubwa kati ya itikadi na uhalisia wa kiuchumi.
Hata hivyo, historia ilithibitisha kwamba mapendekezo mengi ya Mtei yalitekelezwa baadaye katika miaka ya 1980 chini ya Programu za Marekebisho ya Miundo. Ingawa yeye mwenyewe alikuwa nje ya serikali wakati huo, mchango wake katika kufungua mjadala na kuweka msingi wa mageuzi hayo hauwezi kupuuzwa.
Edwin Mtei alikuwa zaidi ya mtendaji; alikuwa sauti ya tahadhari na busara katika safari ya uchumi wa Tanzania. Kuanzia kuanzisha BoT, kusimamia sarafu ya taifa, hadi kushiriki katika mijadala migumu ya sera za kitaifa na kimataifa, alionesha uthubutu wa kitaalamu na uaminifu kwa maslahi ya taifa.