Trump azindua “Bodi ya Amani” Davos, asema dunia inaweza kuongozwa kutokea Marekani

Davos. Rais wa Marekani, Donald Trump, amezua mjadala wa kimataifa baada ya kuzindua rasmi chombo kipya cha kimataifa alichokiita Bodi ya Amani, ambacho amelenga kiwe mbadala wa Umoja wa Mataifa.

Akitangaza amesema kuwa mara kitakapokamilika, Marekani na washirika wake “wanaweza kufanya karibu chochote wanachotaka.”

Trump ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Januari 22, 2026 wakati wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) mjini Davos, baada ya kusaini hati ya kuanzisha bodi hiyo akiwa pamoja na viongozi wa mataifa ya mwanzo yaliyokubali kujiunga na mpango huo.

Nchi zaidi ya 20 zimetia saini kuwa waanzilishi wa Bodi ya Amani, ambapo Umoja wa Mataifa ulioanzishwa  Oktoba 24, 1945 ulikuwa na wanachama waanzilishi 51 na sasa ina wanachama 193.

Utiaji saini wa Bodi ya Amani

Hafla ya utiaji saini ilianza kwa wawakilishi wa Bahrain na Morocco, ikifuatiwa na washirika wa karibu wa Trump akiwemo Rais wa Argentina Javier Milei, Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban, pamoja na Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al-Thani.

Viongozi wengine waliokuwapo ni Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif, Rais wa Paraguay Santiago Peña, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Prince Faisal bin Farhan al-Saud, na Rais wa Kosovo Vjosa Osmani.

Kwa ujumla, mataifa yaliyowakilishwa jukwaani ni Bahrain, Morocco, Argentina, Armenia, Azerbaijan, Bulgaria, Hungary, Indonesia, Jordan, Kazakhstan, Kosovo, Mongolia, Pakistan, Paraguay, Qatar, Saudi Arabia, Uturuki, Falme za Kiarabu (UAE) na Uzbekistan.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ambaye anakabiliwa na hati ya kukamatwa ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kuhusiana na vita vya Gaza, alitangaza nia ya kujiunga na bodi hiyo, ingawa hakuhudhuria hafla ya uzinduzi.


Akizungumza mbele ya viongozi wa dunia, Trump alisema:

“Mara bodi hii itakapoundwa kikamilifu, tunaweza kufanya karibu chochote tunachotaka. Na tutafanya hivyo kwa ushirikiano na Umoja wa Mataifa.”

Kwa mujibu wa hati ya kuanzishwa kwake, Bodi ya Amani inalenga kuwa chombo cha kimataifa cha kukuza uthabiti wa kisiasa, kurejesha utawala wa kisheria unaotegemeka, na kulinda amani ya kudumu katika maeneo yanayokumbwa au yanayotishiwa na migogoro ya kivita.

Trump alidai kuwa karibu kila nchi duniani ina nia ya kujiunga na mpango huo, licha ya kukosekana kwa baadhi ya washirika wakuu wa Marekani, wakiwemo Uingereza, Ufaransa na Canada.

Alisema barua za mwaliko zilitumwa siku chache zilizopita na viongozi waliokuwapo Davos walihudhuria kwa sababu tayari walikuwa katika jiji hilo.

Katika hotuba yake, Trump alijigamba kuhusu rekodi yake ya upatanishi wa migogoro, akidai kuwa amesaidia kumaliza vita nane duniani na kwamba yuko karibu kupata suluhu ya mgogoro wa Urusi na Ukraine.

“Leo dunia ni tajiri zaidi, salama zaidi na yenye amani kuliko ilivyokuwa mwaka mmoja uliopita,” alisema Trump.

Awali, bodi hiyo ilikusudiwa kusaidia kumaliza vita vya Gaza, lakini sasa imepanuliwa kuwa chombo cha kimataifa, hatua ambayo baadhi ya nchi za Ulaya zinaogopa huenda ikaidhoofisha au kuipiku Umoja wa Mataifa.

Rais huyo pia alisema vita vya Gaza vinaelekea ukingoni, akisema sasa vimebaki “mivutano midogo midogo,” huku akisisitiza kuwa Gaza itapaswa kudhibitiwa kijeshi, kuvuliwa silaha na kujengwa upya kwa uzuri. Alionya kuwa kundi la Hamas lazima liweke silaha chini au likabiliwe na “mwisho wake.”

Mkwe wa Trump na mshauri wake wa karibu, Jared Kushner, aliwasilisha mpango mkuu wa ujenzi wa Gaza, akieleza kuwa utatekelezwa kwa awamu na kulenga ajira kwa asilimia 100 na fursa za kiuchumi kwa wakazi wote.

Trump, akijieleza kama mfanyabiashara wa mali isiyohamishika, alisema:

“Ni eneo la bahari lenye thamani kubwa. Ni ardhi nzuri sana. Watu wanaoishi katika umaskini mkubwa wataishi maisha mazuri sana.”

Hatua ya Trump kuanzisha Bodi ya Amani imeendelea kugawanya maoni ya dunia, baadhi wakiona ni juhudi mpya za kidiplomasia, huku wengine wakihofia ni jaribio la kuimarisha ushawishi wa Marekani nje ya mifumo ya kimataifa iliyopo.

Kuanzishwa Umoja wa Mataifa

Umoja wa Mataifa (UN) ni shirika la kimataifa linalojumuisha nchi wanachama 193 kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Mbali na wanachama hao kamili, yapo pia mataifa mawili yenye hadhi ya waangalizi, ambayo ni Vatican (Holy See) na Palestina, yasiyo na haki ya kupiga kura katika Baraza Kuu la UN.

Umoja wa Mataifa ulianzishwa rasmi Oktoba 24, 1945, baada ya kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, kwa lengo la kuzuia kurudiwa kwa vita vikubwa, kulinda amani ya dunia, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kulinda haki za binadamu.

UN ilianzishwa na mataifa 51 ya awali, yaliyotia saini Mkataba wa Umoja wa Mataifa (UN Charter) katika mji wa San Francisco, Marekani, Juni 26, 1945. Mkataba huo ulianza kutumika rasmi Oktoba 24, 1945  siku ambayo sasa huadhimishwa kila mwaka kama Siku ya Umoja wa Mataifa.

Makao makuu ya Umoja wa Mataifa yapo New York, Marekani, huku ukiwa na ofisi kubwa pia Geneva (Uswisi), Vienna (Austria) na Nairobi (Kenya).