Dar es Salaam. Kadiri Tanzania inavyopanua masoko yake ya mitaji, bidhaa za kifedha zilizokuwa zikihusishwa na taasisi kubwa pekee zinaanza kuwafikia wananchi wengi.
Utoaji wa hivi karibuni wa Sukuk ya Al Barakah ya Benki ya CRDB ni miongoni mwa ishara zinazoonesha mwelekeo huo, hasa kwa wananchi.
Katika mchakato huo, Benki ya Stanbic ilishiriki kama mshirika mwenza wa upangaji wa Sukuk hiyo, ikitoa msaada wa kitaalamu katika maandalizi na utekelezaji wa muamala mzima.
Hii ni awamu ya tatu, Stanbic imehusika kuipangilia Sukuk ya CRDB, hali inayoonesha kuimarika kwa uzoefu wa taasisi za kifedha nchini katika kuandaa bidhaa za uwekezaji.
Hayo yameelezwa leo, Ijumaa Januari 22, 2025 na Makamu wa Rais Mwandamizi wa Stanbic anayesimamia masoko ya mitaji Afrika Mashariki, Sarah Mkiramweni.
Amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa karibu kati ya Benki ya Stanbic, wapangaji na wadhibiti wa sekta ya fedha.
Amesema vyombo vya kifedha vinavyoungwa mkono na mali halisi vina nafasi ya kuimarisha masoko ya mitaji na kuongeza machaguo ya uwekezaji kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uwekezaji wa Benki ya Stanbic, Ester Manase amesema mafanikio ya Sukuk ya CRDB yanaonesha kuongezeka kwa imani ya wawekezaji. Ameeleza ushauri wa kitaalamu, maandalizi ya nyaraka na uhamasishaji wa wawekezaji ni mambo muhimu katika kuhakikisha bidhaa hizo zinaeleweka na kukubalika sokoni.
Amesisitiza mchango wa Stanbic hauishii kwenye Sukuk ya CRDB pekee, bali pia imehusika katika upangaji wa dhamana za miundombinu, dhamana za kijani na mikopo mikubwa ya pamoja inayolenga kuunga mkono ajenda za maendeleo.
Ameeleza hatua hizo zinasaidia kuelekeza mitaji kwenye miradi ya maendeleo inayochangia ajira, huduma bora na ukuaji wa uchumi.