Arusha. Serikali kupitia Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), imeondoa sokoni jumla ya viwatilifu 805 vilivyoainishwa kuwa na viambata hatarishi na ambavyo usajili wake haukuhuishwa kwa zaidi ya miaka 10 ili kudhibiti athari zinazohusiana na matumizi yake nchini.
TPHPA yenye jukumu la kusimamia uingizaji, usambazaji, na matumizi ya Viuatilifu nchini imeondoa viuatilifu hivyo baada ya kufanya mapitio ya viuatilifu vilivyosajiliwa nchini na kuainisha hatarishi.
Akizungumzia viuatilifu hivyo leo Jumanne Januari 22,2026, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru amesema wameondoa sokoni jumla ya viuatilifu 130 vilivyoainishwa kuwa na viambata hatarishi kwa mujibu wa FAO na WHO.
“Viuatilifu hivyo vyote vimebainika kuwa na kemikali aina ya Paraquat, Paraquat dichloride, Dimethoate na Acephate ambazo hizo zote kwa sasa zina madhara kwa afya ya mimea na binadamu” amesema.
Profesa Ndunguru pia amesema wameondoa viuatilifu 675 ambavyo usajili wake haukuhuishwa kwa zaidi ya miaka 10.
“Kutokuhuishwa kwa usajili kwa kipindi chote hicho kunadhihirisha mmiliki kutokuwa na uhitaji wa kiuatilifu husika”amesema na kuongeza;
“Kufuatia kuondolewa kwa viuatilifu vyenye viambata hatarishi vilivyotajwa, mamlaka inapenda kuutaarifu umma kuwa kuanzia tarehe ya leo, hakutakuwa na ruhusa ya kuingiza nchini bidhaa za viuatilifu vyenye viambata vilivyotajwa”.
Ametumia nafasi hiyo kuwataka wafanyabiashara wote kutembelea tovuti ya mamlaka kujua viwatilifu hivyo vilivyopigwa marufuku ili walio na akiba ya bidhaa hizo kumaliza kipindi cha miaka miwili.
Sambamba na hilo, profesa Ndunguru amesema wameanza kufanya tathimini kwa watoa huduma ya ufukizaji (Fumigation Service Providers) wa mazao ya kilimo, meli za shehena za mazao, mbao na maghala ya kuhifadhi nafaka nchini kuanzia Januari 14, 2026.
Amesema lengo ni kujiridhisha kuwa huduma hiyo inatolewa kwa mujibu wa matakwa na viwango kama vilivyoainishwa na sheria na kifungu cha 34 cha kanuni za afya ya mimea.
“Hili litahitimishwa Januari, 29, 2026 litaenda sambamba na kufungia watoa huduma za ufukizaji ambao hawatahakikiwa hadi atakapohakikiwa.”
Akizungumzia hatua hiyo mkulima kutoka Arusha, Saimon Lukumai amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza athari za viatilifu kuharibu mazao shambani lakini pia magonjwa mbalimbali kwa binadamu ikiwemo kansa.