Waliopora Iphone, Sh 635,000 watupwa jela miaka 30

Morogoro. Mahakama ya Wilaya ya Morogoro imewahukumu vijana sita (vishandu) wakazi wa Chamwino kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha, tukio lililotokea Machi 31 mwaka 2025.

Akitoa taarifa kwa umma leo Januari 22,2026 mjini hapa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema vishandu hao walihusika na tukio la unyang’anyi lililotokea saa moja usiku wa Machi 31, 2025 katika eneo la Shule ya Msingi Chamwino Manispaa ya Morogoro.

Mkama amesema watuhumiwa hao walimvamia, mfanyabiashara na mkazi wa Chamwino, Abubakar John wakitumia silaha za jadi na kumjeruhi kichwani kwa panga kabla ya kumpora simu aina ya iPhone na fedha taslimu Sh635, 000.

“Baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao na kuwafikisha mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.”amesema Kamanda Mkama.

Kamanda Mkama amesema baada ya usikilizwaji wa kesi chini ya Hakimu, Theresia Kaniki wa Mahakama ya Wilaya ya Morogoro mahakama iliwakuta na hatia Januari 19, 2026 na kuwahukumu kifungo cha miaka 30 jela.

Waliokutwa na hatia ni, Ramadhani Shabani Abdallah (24), Amos John Pagu (23), Said Shabani Aidan (20), Ally Hassan Ally (20), Joseph Raymond Haule (18) na Adrian Exavel Thomas (18), wote wakazi wa Chamwino.

“Jeshi la polisi linatoa wito kwa vijana wote kuachana na vitendo vya uhalifu na badala yake kujikita katika shughuli halali za kujipatia kipato kwani mkono wa sheria ni mrefu na hautamwacha mtu yeyote anayejihusisha na uhalifu,”amesema Kamanda Mkama.