Dar es Salaam. Washtakiwa wanne wa kesi ya uhujumu uchumi wamekiri mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili yakiwemo kuchepusha mzigo kutoka nje iliyokuwa imeidhinishwa na kukwepa kodi zaidi ya Sh125 milioni.
Pia, washtakiwa hao wameilipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Sh125.5 milioni ambazo ni kodi waliyokuwa wameikwepa, fidia ya Sh24 milioni, huku mahakama ikiwahukumu kifungo cha nje cha mwaka mmoja, wakifanya shughuli za kijamii.
Washtakiwa hao wamefikia uamuzi huo kufuatia majadiliano na makubaliano ya kukiri makosa yaliyofikiwa baina ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na washtakiwa hao, ambayo yamesajiliwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, inayoketi Kinondoni.
Washtakiwa hao katika kesi hiyo ambao ni Athanas Msenye (45) Maria Said (37), Godfrey Chamali (31) na Polycap Haule (29) wote wakazi wa Dar es Salaam.
Katika kesi hiyo washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kuondoa lakiri ya forodha kutoka kwenye kontena la gari, kukwepa kodi kwa njia ya udanganyifu, kuchepusha mizigo kutoka kwenye njia iliyoidhinishwa.
Mashtaka mengine yalikuwa ni kutoa nyaraka ya uongo, kuisababishia mamlaka hasara na kupatikana na mali au bidhaa ambazo hazijalipiwa ushuru wa forodha.
Hata hivyo, waliingia katika majadiliano ya kukiri kosa na DPP na kufikia makubaliano yaliyowasilishwa mahakamani hapo jana Jumatano, Januari 21, 2025 na kusajiliwa kuwa hukumu ya mahakama hiyo.
Makubaliano hayo yamesomwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali, Zaituni Mrome, ambapo washtakiwa hao wote wamekiri mashtaka kuwa kweli walitenda makosa hayo na baada ya kukamilisha taratibu za kimahakama yamesainiwa na pande zote mbili.
Pia, katika makubaliano hayo washtakiwa hao wamekubali Jamhuri kutaifisha gari aina ya Scania, walilolitumia katika uhalifu huo. Hata hivyo pande zote zimekuliana kwamba kontena lenye futi 40 ambayo inashikiliwa na TRA pamoja na mzigo wake litarudishwa kwa mshtakiwa namba tatu.
Baada ya kusomewa makubaliano hayo na kukubali kabla ya kusajiliwa, washtakiwa hao wameulizwa na hakimu Kaseko ikiwa ni kweli wameingia makubaliano hayo kwa hiari yao bila kulazimishwa, na kama wanajua madhara ya makubaliano hayo, kuwa kuna haki za msingi wanazikosa.
Washtakiwa hao wote wamejibu kuwa ni kweli wameingia kwa ridhaa yao bila kulazimishwa, na kwamba wanajua madhara yake kuwa wanazikosa haki hizo.
Hakimu Kaseko baada kusikia majibu ya washtakiwa hao na kuridhika kuwa yamefikiwa kwa ridhaa yao, ameelekeza na pande zote yaani upande wa mashtaka na washakiwa wakayasaini, kisha mahakama ikawatia hatiani na kuwahukumu adhabu kwa mujibu wa makubaliano na sheria.
“Kwa kuwa mmeshtakiwa kwa kesi ya uhujumu uchumi na washtakiwa wote mmekiri, na kwa kuwa mmekiri makosa mahakama hii inawatia hatiani kama mlivyoshtakiwa,” amesema Hakimu Kaseko.
Hata hivyo kabla ya adhabu, Hakimu Kaseko amewapa nafasi washtakiwa kutoa shufaa zao, na wote mmojammoja waliomba huruma ya Mahakama iwaondolee kifungo cha miaka 20 jela na pia walikiri makosa yote na wameshafanya malipo yote.
Akitoa adhabu, Hakimu Kaseko amesema Mahakama imezingatia kuwa washtakiwa ni wakosaji wa mara ya kwanza, na kwamba wameingia makubaliano na DPP ya kukiri makosa mahakama inaona kuwa kukikiri kwao kunaonesha kujutia walichokitenda na wako tayari kubadilika.
“Hivyo mahakama inaamuru kuwa washtakiwa wote mtalipa kodi ya Sh125.5 milioni, lakini pia mtatumikia kifungo cha nje cha mwaka mmoja na ofisa huduma kwa jamii atawapangia kufanya shughuli mbalimbali za usafi bila malipo,”amesema Hakimu Kaseko.
Amesema pia washtakiwa wote mtalipa Sh12.6 milioni kama fidia ya TRA na Sh12.1 milioni kwa DPP kama fidia. Adhabu imetolewa kama mlivyoingia makubaliano wenyewe na kwa sababu mmeshaitekeleza hakuna kuomba rufaa.”
Katika mashtaka hayo ilidaiwa Februari 7, 2025 washtakiwa wakiwa eneo la Mikocheni ndani ya Wilaya ya Kinondoni walitoa nyaraka ya uongo kwamba mzigo unaohusu vifaa mbalimbali vya magari ilikuwa safarini kuelekea nchini Congo.
Walidaiwa kuwa hata hivyo waliuchepusha na kuuelekeza eneo la Mikocheni Dar es Salaam hali ambayo ilisababisha ukwepaji kodi wa zaidi ya Sh125.24 milioni.
Walidai siku na mahali hapo washtakiwa wote, walichepusha mzigo wa vifaa mbalimbali vya magari kutoka katika njia iliyokuwa imeidhinishwa kupita ya kutoka Dar es Salaam hadi Congo na wao wakaupeleka mzigo huo eneo la Mikocheni.
Washtakiwa Msenye na Amina pia walidaiwa kuwa tarehe hiyo katika bandari ya Dar es Salaam walitoa tamko la uongo kuhusu maelezo ya mzigo wa vipuri vya gari na kushindwa kujumuisha taa na sola.
Pia walidaiwa kuwa siku hiyohiyo Februari 7, 2025 eneo la Tabata Mwananchi, washtakiwa waliondoa lakiri ya forodha kutoka kwenye kontena la gari.
Vilevile walidaiwa kuwa washtakiwa wote kwa makusudi, walifanya kitendo cha kukwepa kodi na kuisababishia TRA hasara ya Sh125.24 milioni.
Walidaiwa pia kuwa tarehe hiyo, huko Mikocheni, washtakiwa Chamali na Haule walikutwa na vifaa mbalimbali vya magari huku wakijua kuwa vifaa hivyo havijalipiwa ushuru.