Dodoma. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Leonard Akwilapo amesema kuanzia sasa uadilifu na haki vitakuwa dira na kipimo kwa watumishi wa wizara hiyo na hatasita kukaza nati kwa baadhi ya yao, anaodai wamelegea.
Aidha, amewashukia maofisa mipango miji kwa kile alichodai wanaharibu ramani, akitolea mfano wa kituo cha mafuta kilichojengwa katikati ya makazi ya watu katika Mtaa wa Baruti, jijini Dar es Salaam, akihofu huenda wahusika walipokea rushwa.
Agizo hilo limetolewa leo Ijumaa, Januari 23, 2026 na Waziri Akwilapo alipokuwa akizungumza na wakurugenzi, wakuu wa vitengo na idara, makamishna, maofisa mipango na wapima ardhi katika kikao cha mkakati kilichofanyika wizarani hapo.
Akwilapo amesema ndani ya Wizara ya Ardhi, licha ya mazuri mengi yaliyopo, bado kuna madudu na malalamiko kutoka kwa wananchi, huku suala la hatimiliki likionekana kama anasa.
Pia, ameonyesha kusikitishwa na majibu yanayokatisha tamaa kwa wananchi, akisisitiza kila mtu aheshimiwe bila kujali nafasi ya mkubwa au mdogo.
“Ninao mfano wa mtangazaji wa zamani, Abdallah Mlawa. Nimekutana naye akasema amezunguka hadi amechoka akifuatilia majibu ya maombi yake. Hivi watumishi mnajielewa kweli? Kwa nini jambo dogo hadi litolewe majibu kutoka wizarani, huko chini mnafanya nini?” amehoji Akwilapo.
Wakati Waziri akitoa maagizo hayo, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Kaspar Mmuya, ametangaza siku 14 za moto kwa watumishi wa ardhi katika Jiji la Dodoma kuanzia Jumatatu, akisema hakutakuwa na Jumamosi wala Jumapili kwake.
Amesema moja ya maeneo yenye shida ni Jiji la Dodoma na kutaja kitengo cha utoaji wa hati kuwa ndicho chenye tatizo zaidi.
Kabla ya kuwa Mbunge na Naibu Waziri, Mmuya alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma.
Amesema watu wengi wamezoea kuishi na matatizo ya watu, na katika uchunguzi wake amebaini kuwa mtu wa mwisho kutoa hati hutumia dakika moja na sekunde 30, lakini wananchi wanatafuta hati hadi miaka 10 bila sababu za msingi.
“Watu wanahangaika sana katika nchi hii. Kupata hati imekuwa kama anasa. Tunaanza na Jiji la Dodoma na nchi nzima. Nataka majibu siku ya Jumanne ijayo ili nijue waliokamilisha mchakato lakini hawajapata hati, nataka kujua wenye vikwazo, na mnipe majibu ya viwanja vilivyopimwa,” amesema Mmuya.
Naibu Waziri amesisitiza umuhimu wa utunzaji wa siri katika operesheni mbalimbali, akionya kuwa kuna hofu baadhi ya watumishi wanavujisha taarifa, na akaonya wakibainika watashughulikiwa.
Ofisa wa Tume ya Mipango wa Wizara hiyo, Mariam Mlayi, amemwambia Waziri kuwa ndani ya Jiji la Dodoma, kitengo cha malipo ni tatizo, hasa katika utoaji wa namba za malipo.
Mlayi amesema aliwahi kufika hapo akitaka kupatiwa namba ya malipo ili alipie kiwanja chake, lakini kila siku aliambiwa “njoo kesho” hadi akakata tamaa, hivyo akamwomba waziri aangalie suala hilo, akisema kama yeye akiwa mtumishi ametendewa hivyo, hali ikoje kwa wananchi wa kawaida.