BIGMAN imekamilisha usajili wa beki wa kati, Better Abdallah Mnyamisi, aliyekuwa akikichezea kikosi cha IAA cha jijini Arusha kinachoshiriki Ligi Daraja la Pili, baada ya kuzishinda Mbeya Kwanza na Stand United zilizokuwa zinamtaka.
Beki huyo alijiunga na IAA baada ya kuachana na TMA ya jijini Arusha inayoshiriki Ligi ya Championship, amefikia makubaliano ya kusaini mkataba wa miezi sita hadi mwisho wa msimu, kwa lengo la kuitumikia timu hiyo ya Mkoa wa Lindi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mnyamisi amesema timu mbalimbali zilionyesha dhamira ya kumhitaji dirisha hili dogo la usajili, ingawa amefikia uamuzi wa mwisho wa kwenda Bigman, akiamini ni sehemu nzuri ya yeye kuzidi kuonekana zaidi.
“Licha ya ofa nyingi ila nilizingatia pia na nafasi yangu ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza kwa sababu hilo ndilo lengo kubwa, nina uzoefu na Championship hivyo, nipo tayari kwa ajili ya changamoto mpya,” amesema Mnyamisi.
Nyota huyo licha ya kuichezea Championship msimu wa 2024-2025, ila ana uzoefu mkubwa pia wa kucheza Ligi Kuu Bara, kwani aliwahi kuitumikia Polisi Tanzania kuanzia msimu wa 2021-2022 hadi 2023-2024, kisha kuondoka na kujiunga rasmi na TMA.
Msimu wa 2024-2025, nyota huyo aliiwezesha TMA kumaliza Ligi ya Championship ikiwa nafasi ya tano na pointi 53, baada ya kushinda mechi 15, sare minane na kupoteza saba kati ya 30, iliyocheza, huku ikifunga jumla ya mabao 40 na kuruhusu 29.