Bibi asimulia alivyotelekezwa mochwari vurugu za Oktoba 29

Dar es Salaam. “Nilitelekezwa kwenye chumba kwa zaidi ya saa tano katika hospitali ya Mwananyamala nikidhaniwa nimekufa. Baadaye nilipoanza kukohoa ndiyo wakaulizana, vipi huyu bibi, kumbe bado ni mzima?”

Hayo ni maneno ya Aurelia Joseph (75), mkazi wa Magombeni Kota, Dar es Salaam, ambaye amesimulia namna alivyowekwa mochwari kwa zaidi ya saa tano, akidhaniwa amefariki dunia wakati wa vurugu siku ya uchaguzi, Oktoba 29, 2025.

Mwanamke huyo amesimulia mkasa huo mbele ya Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, inayoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman.

Rais Samia Suluhu Hassan aliunda Tume hiyo kufuatia maandamano yaliyotawaliwa na vurugu siku ya uchaguzi, ikiwa ni njia ya kutafuta chanzo cha vurugu hizo kabla ya kuelekea kwenye maridhiano ya kitaifa.



Bibi asimulia alivyotelekezwa mochwari vurugu za Oktoba 29

Leo, Januari 23, 2026, Tume ilikuwa Magomeni, Wilaya ya Kinondoni, ambapo baadhi ya wananchi wamejitokeza kutoa ushahidi wa mambo yaliyotokea siku ya uchaguzi na wao kujikuta wakiwa waathirika.

Mmoja wa waliotoa shuhuda zao ni kikongwe, Aurelia, amepata fursa ya kusimulia alichokutana nacho siku hiyo, akisema alitelekezwa chumba cha maiti kwa zaidi ya saa matano akidhaniwa kufariki dunia baada ya kupigwa risasi.

Aurelia anasimulia kwamba siku ya uchaguzi alikwenda kituoni kupiga kura na alipomaliza alirudi nyumbani. Akiwa nyumbani, takribani saa 6 mchana, alichungulia dirishani akaona vurugu zikiendelea katika eneo hilo huku watu wakipoteza maisha.

“Niliona maiti tatu zikiwa chini, vurugu kubwa zikiendelea. Ghafla, nikapigwa na kuanguka chini, nilipopiga kelele kuomba msaada, nilianguka chini na kupoteza fahamu.

“Nilifumbua macho nikiwa hospitali ya Mwananyamala huku majeruhi wanakuja kwa wingi. Wakinitelekeza wakijua nimekufa,” amesimulia kikongwe huyo.


Amesema alitelekezwa kwenye chumba kilichokuwa na zaidi ya maiti 20 huku akishuhudia majeruhi wengine wakiendelea kupoteza maisha ndani ya chumba hicho, yeye mwenyewe akihofiwa kuwa amefariki.

Amesema ilipofika usiku alipoanza kukohoa, alishangaa kusikia wanaambizana “huyu bibi vipi, bado mzima?” ndipo wakamsogelea.

“Walinichukua wakanivua nguo zote, ndipo wakagundua nilikuwa nimepigwa risasi juu ya bega, baadaye madaktari wakasema kuna kikosi kinakuja hapa, wenye majeraha ya risasi mjiandae maana tunaambiwa tunahifadhi wahalifu humu.

“Baadaye kikosi kilikuja, kikaanza kutuhoji. Wakasema huyu bibi ndiye mwenye vurugu, wakaniuliza kwanza kura umempigia nani? Nikawajibu kwamba nimempigia anayestahili kuchaguliwa maana hana mpinzani. Wakasema kumbe huyu hajaenda kwenye maandamano,” amesema.


Baadaye, amesema waliambiwa kwamba waliopigwa risasi wote waondoke kurudi nyumbani kwani hakuna matibabu katika hospitali hiyo. Amesema aliondoka kwenda hospitali ya Magomeni ambako nako hakupata huduma kwani hakukuwa na madaktari.

“Baadaye nilianza tiba za kienyeji na hadi sasa sijapona. Madaktari waliniambia nina chembechembe za risasi zilibaki kwenye mkono wangu huu (akiuonyesha mkono wa kushoto),” amesema huku akiomba msaada wa matibabu zaidi kutokana na kutomudu gharama za matibabu yanayohitajika.

Baada ya kuhitimisha maelezo yake, mjumbe wa Tume hiyo, Jaji Mkuu mstaafu, Profesa Ibrahim Juma amemweleza kikongwe huyo kwamba kwa umri wake anastahili msamaha wa gharama za matibabu na kwamba watu wa Ustawi wa Jamii watamsaidia kupata matibabu hayo.

“Aurelia pole sana. Kwa umri wako una msamaha wa gharama za matibabu, watu wa Ustawi wa Jamii wapo, wamekusikia, watakusaidia,” amesema Profesa Juma, akizungumza na Aurelia, baada ya kumaliza kutoa ushahidi mbele ya Tume.

Wakati Aurelia akieleza yaliyomkuta siku ya uchaguzi, waathirika wengine wa vurugu zilizotokea siku ya uchaguzi wameeleza namna walivyopoteza wapendwa wao, jambo ambalo limebadilisha maisha yao.

Veronica Lyimo (37), mkazi wa Magomeni Kagera na mjasiriamali wa upambaji kwenye sherehe, amesema siku ya uchaguzi, yeye akiwa mapumzikoni nyumbani kwake, mume wake alipigwa risasi katika mazingira ya kutatanisha.

“Nilikuwa na mume wangu, akasema ngoja atoke kidogo, nilipoivisha chakula nataka nimuite aje ale, napiga simu hapokei, baadaye akapokea kijana mwingine, akasema mwenye simu hii amepigwa risasi hapa.

“Nilitoka nikakuta ana hali mbaya sana, amepigwa risasi yupo chini, tukampeleka Mwananyamala, nilipofika mume wangu najua kabisa yupo hai, lakini daktari akaniambia nenda wodi namba nne, nilipoenda nikakuta mume wangu amekufa.

Mwenye wa Tume ya Kuchunguza Matukio ya Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman (wa tatu kulia) akizungumza wakati wa kikao na waathirika wa matukio hayo alipokutana nao leo Ijumaa, Januari 23, 2026, Dar es Salaam.



“Daktari akasema nimethibitisha mume wako amekufa maana amepigwa risasi ya tumbo, imefika kwenye mapafu,” amesema mwanamke huyo huku akilia mbele ya Tume.

Alipohojiwa kuhusu mazingira ya tukio hilo, Veronica, akilia kwa kwikwi, amesema mume wake, Emmanuel Joseph, alipigwa risasi akiwa maeneo ya nyumbani kwake kabla ya kwenda kuthibitishwa amekufa wodi namba nne katika hospitali ya Mwananyamala.

“Katika tukio hilo, rafiki wa mume wangu, aliyeshuhudia tukio hilo, aliniambia zilikuja gari mbili, watu wakatoka kwenye Noa iliyokuwa mbele ya Diffender, wakawafyatulia risasi mume wangu na rafiki yake ambao wote walikufa,” amesema akiongeza kuwa alimzika mume wake Novemba 6, 2025.

Shuhuda mwingine ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi kituo cha Shule ya Msingi Mzimuni, Rahma Said (49), mkazi wa Magomeni Mapipa, amesema Oktoba 29, 2025, mtoto wake, Mohamed Salum alipigwa risasi akiwa nyumbani kwake Magomeni.

“Tulikuwa tunasimamia uchaguzi, likaja kundi la vijana zaidi ya 70 huku tukiona moto unawaka Magomeni Mikumi, tukakimbilia nyumba za majirani, baadaye mume wangu akanipigia simu akisema mwanangu amepigwa risasi akiwa nyumbani,” amesema.

Amesema baada ya kupigwa, walimpeleka hospitali ya Arafa, hakutibiwa, akarudi nyumbani, siku iliyofuata, Alhamis saa 7 usiku, akaniambia ganzi imemshika huku sehemu aliyopigwa risasi ikitoa damu nyingi, akafariki.

“Kilichotokea katika mtaa wetu wa Mzimuni ni msafara mkubwa wa vijana wakiwa na mabegi, madumu ya maji, huku wakisema ‘hatumtaki Mama Samia, kitaeleweka tu’, ulipita, hadi wasichana wadogowadogo walikuwemo,” amesema.


“Waandamanaji walijifunga kininja, wengine wakibeba makopo ya maji na wamejipaka vitu machoni, wala hawakuwa vijana wa mtaa wetu na nilipomuuliza mwanangu, alisema hajaenda kwenye maandamano lakini alipigwa risasi akiwa nyumbani,” amesema.

Amesema kifo cha mtoto wake kutokana na hali ikiyokuwepo, hakikuripotiwa polisi bali alimzika akisaidiwa na majirani wachache.

Kwa upande wake, mkazi wa Kimara Korogwe, Juma Matari (25), mfanyabiashara wa simu Manzese Darajani, amesema siku ya uchaguzi alikuwa mapumzikoni nyumbani kwake lakini akapigiwa simu na rafiki yake akimtaka afike eneo la biashara yake kufuatia sintofahamu iliyokuwa ikiendelea.

“Nilikutana na taharuki kubwa ya watu njiani, nilipofika pale nikakuta kundi la vijana wa umri wa miaka 25 – 27 wakiwa na silaha za jadi zikiwemo vipande vya mawe, mapanga na nondo, wakiwa zaidi ya watu 200, wakitokea Ubungo ndani ya barabara ya Morogoro.

“Walichoma kituo cha mwendokasi na kuvunja meza za wafanyabiashara, wakarusha mawe kwenye fremu na nyumba za watu huku wakisema ‘lazima haki itendeke’, wakachoma na sheli ya Lake Oil iliyopo eneo hilo,” amesema.

Amesema kundi lililofika hapo lilikuwa la pili kati ya makundi matatu ya watu zaidi ya 200, kila moja yaliyopita eneo hilo, akisema walichoma moto mali mbalimbali za wafanyabiashara zilizokuwa eneo hilo.

“Walipofika walivunja mageti ya fremu, wakachukua kabati lilikokuwa na zaidi ya simu 200 zenye thamani ya zaidi ya Sh60 milioni,” amesema, akiiomba Tume kuangalia ukubwa wa madhara waliyopata waathirika ili kuwasaidia kulingana na madhara waliyopata.

Baada ya kusikiliza na kupokea simulizi za waathirika hao, Profesa Juma amewataka Watanzania kuendelea kutoa ushirikiano kwa Tume hiyo ili kupata ukweli na kuhakikisha matokeo ya uchunguzi wa Tume hiyo ndiyo utakaosaidia kuepusha yaliyotokea yasitokee tena.

“Tunawashukuru waliotoa ushahidi wa walichokiona, tunawasihi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Tume ili tujue ukweli wa nini kilitokea wakati wa uchaguzi wa mwaka jana, sababu za kutokea na malengo yake yalikuwa yapi na athari zake zilikuwa zipi,” amesisitiza.