Dodoma. Serikali imetangaza kuanza utekelezaji wa awamu ya kwanza ya Bima ya Afya kwa Wote (BAW), hatua inayolenga kuwaondolea mzigo wa gharama za matibabu wananchi wasio na uwezo wakiwemo wazee, watoto, wajawazito na watu wenye ulemavu, ambao gharama zao zitabebwa na Serikali.
Waziri amesema Kitita cha Huduma Muhimu kwa awamu ya kwanza kitaanza kutumika Januari 26, 2026, kwa kundi la wananchi watakaogharamiwa na Serikali.
Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa amezungumza hayo leo Januari 24, 2026 wakati wa kikao kazi cha kitaifa cha kujadili utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.
Mkutano huo ambao umefanyika jijini Dodoma umelenga kuweka mwelekeo wa pamoja wa utekelezaji wa mpango huo unaotarajiwa kubadilisha taswira ya huduma za afya nchini.
Waziri amesema awamu ya kwanza ya utekelezaji itaambatana na kuanza kutumika kwa Kitita cha Huduma Muhimu, kitakachotolewa na Skimu za Bima ya Afya wakilenga makundi yaliyo hatarini ili kupata huduma za afya bila kikwazo cha fedha.
“Bei ya kitita hicho ni Sh150,000 kwa kaya isiyozidi watu sita, kikiwa kinazingatia utaratibu wa rufaa katika vituo vya afya vilivyoingia mkataba na Skimu za Bima ya Afya,” amesema Mchengerwa na kuongeza.
“Nasisitiza kuwa Bima ya Afya kwa Wote si mradi wa Wizara moja bali ni ahadi ya Taifa kwa wananchi wake, mafanikio ya mpango huo yatapimwa si kwa hotuba wala maagizo, bali kwa idadi ya wananchi wanaolindwa dhidi ya gharama za matibabu na wanaopata huduma kwa heshima,” amesema.
Baadhi ya Wakuu wa Mikoa walioshiriki kwenye kikao kazi cha kitaifa cha kujadili utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.
Katika kufanisha hayo, amewaelekeza Wakuu wa Mikoa yote nchini kubeba dhamana ya moja kwa moja, binafsi na isiyoweza kuhamishwa ya utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote katika mikoa yao.
Hata hivyo, ameeleza kuwa jambo hilo si jukumu la kiufundi linaloweza kuachwa kwa wataalamu pekee bali ni jukumu la kiuongozi linalohitaji uwepo, uamuzi na ufuatiliaji wa karibu wa mkuu wa mkoa mwenyewe.
Kwa mujibu wa waziri, mafanikio, mapungufu na changamoto za utekelezaji zitatathminiwa kwanza kupitia uongozi wa mkoa husika na kwamba mkoa ambao wananchi wake wanaelewa mfumo, wamesajiliwa kwa wingi na wanapata huduma bila vikwazo, utaonekana kama mfano wa uongozi unaotekeleza uamuzi wa Serikali kwa ufanisi.
Amesisitiza kuwa Bima Afya kwa Wote lazima iwe ajenda ya kudumu katika vikao vya maendeleo, vikao vya usalama na vikao vya tathmini ya utendaji na isizungumzwe kama taarifa ya ziada bali ijadiliwe kama ajenda ya msingi ya ustawi wa wananchi na uthabiti wa kijamii wa mkoa.
Amesema ubora wa huduma katika vituo vya afya ndio msingi wa kufanikisha Bima ya Afya kwa Wote na kusisitiza viongozi wa mikoa, wilaya na halmashauri kusimamia kwa karibu utoaji wa huduma ili wananchi wasipoteze imani waliyonayo kwa Serikali.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk Self Shekalaghe amesema afya ni mtaji wa uchumi na bila wananchi kuwa na afya njema, shughuli za uzalishaji haziwezi kuendeshwa kwa ufanisi.
“Mtu anapougua, familia nzima inaathirika kiuchumi na kisaikolojia, Bima ya Afya kwa Wote inalenga kuondoa dhiki hii kwa wananchi,” amesema
Dk Shekalaghe ameongeza kuwa Bima ya Afya kwa Wote ni suluhu ya kudumu kwa mzigo wa kifedha uliokuwa ukiikabili familia nyingi pindi mmoja wao anapougua, akieleza kuwa mpango huo utaondoa hofu ya gharama za matibabu na kuwezesha wananchi kupata huduma za afya kwa wakati.
“Serikali ina faraja kuona kuwa mzigo wa kugharamia afya sasa umepata mwelekeo wa utekelezaji unaogusa maisha ya wananchi wa kawaida, hususan makundi maalumu yaliyokuwa hatarini zaidi,” amesema.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe amesema utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ni hatua ya kihistoria itakayobadili namna Watanzania wanavyopata na kugharamia huduma za afya, hususan kwa makundi yasiyo na uwezo.
Ameeleza kuwa lengo ni kuhakikisha haki ya kupata huduma bora za afya inalindwa na kufikiwa na kila mwananchi bila kikwazo cha gharama.
Katibu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, John Jingu,l amesema wataalamu wa maendeleo ya jamii wana jukumu la kujenga uelewa na kubadilisha fikra za wananchi ili washiriki kikamilifu katika mpango huo.
Amesema mafanikio ya mpango huo hayatategemea sera pekee, bali yatachangiwa kwa kiasi kikubwa na namna wananchi watakavyoelewa haki na wajibu wao katika mfumo wa bima ya afya.