Dar es Salaam. Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Bobi Wine ameibuka na kusema hatatii agizo, akijibu wito wa Mkuu wa Majeshi nchini humo alioutoa Jumanne akimtaka kujisalimisha Polisi.
Katika mahojiano ya simu na Shirika la Habari la AFP, Bobi Wine amejibu vitisho vilivyotolewa na Jenerali Muhoozi Kainerugaba, akionesha hayuko tayari kutii agizo lake.
Jumanne iliyopita, Mkuu huyo wa Majeshi ya Uganda ambaye ni mtoto wa Rais Museveni, aliandika katika ukurasa wake wa X akimtaka Bobi Wine kujitokeza na kuripoti polisi ndani ya saa 48.
Katika agizo lake, Kiongozi huyo ambaye amekuwa akishutumiwa kutumia jeshi kukabili wapinzani wa kisiasa wa baba yake, Rais Museveni, alisisitiza kuwa kama Bobi Wine asingejitokeza ndani ya muda aliompa angeshughulikiwa kama mhalifu.
“Ninampa saa 48 ajisalimishe kwa Polisi, asipofanya hivyo tutamchukulia kama mhalifu na kumkabili ipasavyo,” alisema Muhoozi.
Katika hali inayozidisha mvutano wa kisiasa tangu uchaguzi mkuu wa urais wa wiki iliyopita, Wine hajajitokeza kama alivyotakiwa na Jeshi hilo.
Bobi Wine, mwenye umri wa miaka 43 na anayejulikana pia kama Robert Kyagulanyi, amesema yuko mafichoni tangu Jumamosi baada ya kile alichokitaja kuwa ni jaribio la vikosi vya usalama kuvamia makazi yake.
Akizungumza na shirika la habari la AFP siku ya Jumatano, Januari 21, 2026, Bobu Wine amesema analazimika kuhama mara kwa mara huko aliko jificha ili kujinusuru, huku akilindwa na raia wa kawaida.
“Ni kweli ninahama mara kwa mara, lakini kwa sasa ninahifadhiwa na kulindwa na watu wa kawaida,” amesema.
Kiongozi huyo wa Chama cha National Unity Platform (NUP) amedai mazingira ya sasa ya usalama si rafiki kwake, akisisitiza kuwa sababu ya kukimbilia mafichoni si kosa lolote la jinai bali ni msimamo wake wa kisiasa na uamuzi wake wa kugombea urais dhidi ya chama tawala.
Akijibu kuhusu agizo la Mtoto wa Rais Museven ambaye ni mkuu wa majeshi nchini humo la kumtaka ajitokeze na kufika polisi, Wine amesema hataenda maana hajatenda kosa.
“Mimi si mhalifu bali ni mgombea urais. Si kosa kugombea dhidi ya baba yake,” amesema Wine,
Uchaguzi wa urais uliofanyika Alhamisi iliyopita ulimpa Rais Museveni, mwenye umri wa miaka 81, ushindi wa muhula wa saba kwa kupata asilimia 72 ya kura zilizopigwa.
Hata hivyo, Wine alikataa matokeo hayo na kuyataja kuwa “ni wizi wa waziwazi” akidai yaligubikwa na udanganyifu, vurugu na vitisho dhidi ya wapinzani.
Mvutano huo uliingia hatua mpya baada ya Mkuu wa Majeshi ya Uganda kutoa kauli kali kupitia mtandao wa kijamii wa X, kauli zilizozua taharuki kubwa ndani na nje ya nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki.
“Tumeua magaidi 22 wa NUP tangu wiki iliyopita. Ninaomba wa 23 awe Kabobi,” aliandika Jenerali Muhoozi Kainerugaba, akitumia jina la utani analomwita Bobi Wine.
Kauli hiyo imekuwa ikikosolewa vikali na wanaharakati wa haki za binadamu pamoja na wachambuzi wa siasa, wakidai kuwa ni hatari kwa matumizi ya lugha ya vitisho kutoka ngazi ya juu ya jeshi dhidi ya kiongozi wa upinzani.
Hata hivyo, katika majibu ya Bobi Wine ameonesha kutokuwa na hofu dhidi ya vitisho hivyo, akisema hana hofu binafsi, lakini ameeleza wasiwasi wake kuhusu mustakabali wa demokrasia nchini Uganda na usalama wa wafuasi wa chama chake.
“Katika udikteta, hupangi mikakati. Unachofanya ni kujibu aina ya ukandamizaji uliopo,” amesema, akionesha nia ya kuendelea na mapambano ya kisiasa dhidi ya utawala wa Rais Museveni.
Kwa mujibu wa Wine, chama chake kwa sasa hakiwezi kuweka mkakati wa muda mrefu kutokana na mazingira ya vitisho, kukamatwa kwa wanachama, na madai ya utekaji wa wafuasi wa upinzani yaliyoripotiwa katika maeneo kadhaa ya nchi hiyo kufuatia vurugu za uchaguzi huo.
Uchaguzi huo pia umeshuhudia vurugu katika baadhi ya maeneo pamoja na kuzimwa kwa huduma za intaneti na mitandao ya kijamii, hatua iliyodaiwa kudhibiti taarifa na kuzuia mawasiliano ya wapinzani pamoja na waangalizi wa uchaguzi.
Kadri siku zinavyosonga mbele, mvutano kati ya Bobi Wine na uongozi wa kijeshi unaendelea kuwa kipimo cha mwelekeo wa siasa za upinzani nchini Uganda, huku macho ya Afrika na jumuiya ya kimataifa yakielekezwa kuona kama hali itatulia au kuingia awamu mpya ya msukosuko wa kisiasa.