Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BOT) Emmanuel Tutuba amesema taasisi hiyo itaendelea kuienzi misingi ya awali aliyoweka na mzee Edwin Mtei akimtaja kama mtu aliyejitoa sadaka katika kipindi chake cha uongozi wa taasisi hiyo.
Mtei (94) aliyefikwa na umauti Januari 19,2026 alikuwa Gavana wa kwanza wa BoT kuanzia mwaka 1966 na miaka 12 baadaye akawa Waziri wa Fedha na Mipango ambapo alitumikia nafasi hiyo kuanzia mwaka 1978 hadi 1981 alipojiuzulu wadhifa huo.
Tutuba amesema Mtei alianza kazi katika kipindi kigumu lakini aliweka misingi thabiti, misingi imara, misingi ya haki, uadilifu na misingi ya kujitoa sadaka ambayo mpaka leo inaendeleza ndani ya taasisi hiyo.
Gavana huyo amebainisha kuwa BOT si tu itaiendeleza misingi hiyo bali itaiboreshwa kadri mahitaji na mabadiliko ya kiuchumi yatakavyokuwa.
Amesema wataendelea kuthamini mchango wake kwani jambo lolote linapoanzishwa linakuwa na changamoto ila alijitahidi kuweka mifumo na misingi thabiti ya kusimamia uchumi wa Taifa.
Gavana Tutuba amesema enzi za uhai wa Mzee Mtei, alibahatika kuzungumza naye ambapo alimweleza namna walivyopata changamoto kipindi hicho ikiwemo wakati wa kufanya malipo kwa hundi.
“Sasa hivi tunatumia muda wa saa mbili kufanya malipo ya hundi toka benki yoyote ile nchini.Mzee Mtei anasema wakati ule ilikuwa inachukua mwezi mzima kuithibitisha hundi kutoka kona mbalimbali za nchi yetu,”
“Hundi zilizokuwa zikisambazwa kupitia benki yoyote mfano mstaafu akilipwa kama yuko mikoa ilete Dar Es Salaam ipelekwe idara ya uhakiki wa hundi ambayo waithibitishe kisha ipelekwe benki.Aliniambia walivyokuwa kazi kwsnye mazingira magumu ya kufunga hesabu,”amesema na kuongeza
“Ilikuwa malipo ya kila siku lazima wayafunge kwa kutumia kaunta book na kuna zile leja maalum waandika kwa mkono enzi hizo kwa hiyo unaweza ukaona namna ya kufanya consolidation ya fedha zote za serikali na malipo ya watu wote ndani ya nchi ndani ya siku husika ili waruhusu malipo ya siku husika yafanyike,”
Amesema BoT imeanzisha maktaba na makumbusho ambazo zinaonyssha kumbukumbu katika muda wote aliohuduma Gavana huyo wa kwanza.
“Ukitembelea makumbusho yetu pale makao makuu utakuta mambo mengi ambayo yameanzia kabla ya kupata uhuru,tulivyopata uhuru na ilipovunjwa bodi ya sarafu ya EAC ambayo ilimwezesha yeye kuteuliwa na kuanzisha BoT,”
Amesema mwaka huu wanapoadhimisha miaka 60 ya kufanya shughuli za BoT pamoja na mengi ambayo yapo wataendelea kuyaenzi ya Mzee Mtei.
“Tumetunza kuanzia kaunta ya kwanza iliyotengenezwa wakati ule alivyomkabidhi Mwalimu Julius Nyerere hati ya kwanza utaona pale na hata noti za mwanzo zilizovyoanza kuchapishwa,ziko pale tumezitunza kuna mambo mengi.Kama nilivyosema mabadiliko ya mifumo yanaenda yanaboresha hali za maisha yetu,”
“Tuko vizuri kutunza historia ya mambo mbalimbali ya kiuchumi,kifedha na mifumo ya malipo na masuala mengine ya kiuchumi tunaendelea kutunza na yeye ndiye aliweka misingi ya awali tutaendelea kuienzi na kuiboresha kadri ya mahitaji na mabadiliko ya kiuchumi kwa sababu wakati ule alikuwa anaandika kwa mikono hatuwezi kusema sasa hivi tuandike kwa mikono,siku hizi kuna mifumo ya kisasa na teknolojia imeendelea kuboreshwa,”amesema
Mwili wa Mtei ambaye pia ni mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), unatarajiwa kuwasili nyumbani kwake Tengeru, Arusha kwa ajili ya maziko kesho.
Msemaji wa familia hiyo, Freeman Mbowe amewaeleza waandishi wa habari leo ratiba ya maziko itaanza saa tatu asubuhi Januari 24.
“Tumejaribu kutafuta njia kila kundi lipate nafasi ya kutoa salamu zake na liweze kushiriki kadri linavyoweza.Yako makundi mbalimbali ikiwemo vyama vua kisasa,vyama karibu vyote vimetupa taarifa ya kufika,”
“Chama kiongozi katika jambo hili ni Chadema ambapo huyu ni mwasisi wa chama chetu, kwa hiyo nafasi kubwa itatolewa kwa Chadema kwa sababu baba ni mwasisi wa chama chetu lakini baada ya hapo yatafuata makundi mbalimbali, Chama cha ACT Wazalendo kutoa taarifa za kushiriki kwao, viongozi wa serikali vilevile wametoa taarifa za kushiriki kwao, (BoT) na wengine,”ameongeza
Msemaji huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa zamani wa Chadema Taifa, amesema ratiba itaenda mpaka saa saba ambapo ibada rasmi itaanza.
“Tunategemea iada itafanyika hapa hapa na baada ya hapo tutakwenda kwenye makaburi ambapo tutatangaza utaratibu wa kwenda makaburini, hatutaki vurugu kwa watu kuvurugana,”amesema.