Chadema yatangaza kuanza shughuli za kisiasa, wanasheria wagongana

Dar/Arusha. Mvutano wa kisheria umeibuka kuhusu hatima ya zuio la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kufanya shughuli za kisiasa, baada ya kauli kinzani kutolewa kati ya uongozi wa chama hicho na jopo la mawakili wa wadai waliopata zuio hilo mahakamani.

Mvutano huo umekuja baada ya Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Wakili Dk Rugemeleza Nshala, kutoa taarifa kwa umma akieleza kuwa zuio hilo lilikuwa na muda maalumu wa miezi sita na tayari limeshakwisha.

Taarifa ya Dk Nshala pia imeungwa mkono na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho (Bara), John Heche, ambaye amesema kuwa kufuatia kukoma kwa zuio hilo, chama kiko tayari kuendelea na shughuli zake za kisiasa na siku si nyingi watatoa utaratibu wa kufanaya mikutano.

Hata hivyo, taarifa ya Dk Nshala na kauli ya Heche zimepingwa na kiongozi wa jopo la mawakili wa wadai, Wakili Shaban Marijani, aliyesema kuwa waliotoa taarifa hiyo wanajichanganya katika tafsiri ya amri ya mahakama.

Mvutano huo unatokana na amri ya Mahakama Kuu Dar es  Salaam iliyotolewa Juni 10, 2025 ikitoa zuio dhidi ya Chadema kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali za chama mpaka kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa mali inayokikabili itakapoamuliwa.

Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 imefunguliwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa  Chadema, Said Issa Mohamed, na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.

‎Walalamikiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga ni Bodi ya Wadhamini Waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.

Hata hivyo, leo Ijumaa, Januari 23, 2026 Chadema kupitia Mwanasheria wake Mkuu, Wakili Dk Rugemeleza Nshala kimetoa taarifa kwa umma kuwa zuio hilo lililkuwa la miezi sita tu, hivyo limeshakwisha.

“Tunapenda kuwaeleza Watanzania wote na wapenda demokrasia kuwa zuio la kufanya shughuli za kisiasa kwa Chadema lilikoma mnamo tarehe 10 Desemba 2025 ambayo ilikuwa ni mwezi wa sita kamili tangu zuio hilo lilipowekwa na Jaji Hamidu Mwanga mnamo tarehe 10 Juni 2025,”inasomeka taarifa hiyo iliyosainiwa na Dk Nshala.

Taarifa hiyo imesema kuwa kukoma huko ni kutokana na Kanuni ya 3 ya Amri ya 37 ya Sheria ya Mwenendo wa Madai (Sura 33, Marejeo yam waka 2023

Taarifa hiyo imefafanua kuwa kanuni hiyo na amri hiyo inasema kuwa Mahakama inaweza kutoa amri ya zuio kwa mujibu wa kanuni ya 1 au kanuni ya 2 na amri hiyo itakuwa na maisha kwa kipindi kilichotajwa na Mahakama, lakini kisichozidi miezi sita.

Pia, imesema kuwa kifungu hiki cha sheria kilitafsiriwa kwa kituo na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania katika kesi ya African Trophy Hunting Ltd vs Attorney General and 4 Others (Civil Appeal 25 of 1997) [1998] TZCA 11 (3 December 1998).

Imesema kuwa Mahakama hiyo ya juu kabisa nchini ilisema kuwa amri ya zuio inaweza kutolewa kwanza kwa miezi sita na inaweza kuongezwa zaidi, lakini nyongeza hiyo ikiwa ni pamoja na zuio la kwanza lisizidi jumla ya mwaka mmoja.

“Ieleweke kuwa kufikia tarehe 10 Desemba 2025 si Saidi Issa Mohamed, au Ahmed Rashid Khamis, ama Maulidah Anna Komu waliokwenda Mahakama Kuu kuomba muda wa zuio hilo kuongezwa,” inaeleza taarifa hiyo na kusisitiza:

“Hii inaamanisha kisheria kuwa, amri ya zuio dhidi ya shughuli za kisiasa za Chadema ilifutwa kwa utekelezaji wa sheria.”

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Arusha kuhusu taarifa hiyo, Heche amesema kuwa kufuatia taarifa hiyo sasa wako tayari kuendelea na shughuli za kisiasa na kwamba watatoa programu watakazoanza nazo na taratibu.

“Tutakuwa tayari kwa mikutano, kama vikao vya chama, ofisi za chama kufunguliwa na shughuli nyinginezo,” amesema Heche.

Hata hivyo, kiongozi wa jopo la mawakili wa wadai, Shaban Marijani amesema kuwa walioandika taarifa hiyo kuna mambo wanajichanganya .

Amesema kuwa amri ya mahakama imesema wazi kuwa zuio litadumu mpaka kesi ya msingi itakapokwisha na kwamba kama wao wana tafsiri nyingine ya amri hiyo ya mahakama waitoe.

Kuhusu tafsiri ya kanuni ya 3 Amri ya 37 ya Kanuni za Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai, Marijani amesema kuwa hiyo ni hoja kisheria ambayo inahitaji mjadala.

Amesema kuwa wakati kuna kesi rejea ambazo zinaunga mkono msimamo huo, lakini kuna kesi rejea nyingine ambazo zinapinga.

“Kwa hiyo wao kama wana hoja basi wailete mahakamani kwa utaratibu rasmi tukutane mahakamani na si kwenda kuzungumza tu kwenye media,” amesema.