KIUNGO Mshambuliaji wa zamani wa Simba na Yanga, Hassan Dilunga amesaini mkataba wa kuichezea Mbeya City inayonolewa na kocha Mecky Maxime.
Chanzo cha ndani kutoka Mbeya City kimesema usajili wa Dilunga ni mapendekezo ya kocha Maxime, hivyo uongozi umetimiza wajibu wake kwa kufanikisha kupata saini yake.
“Dilunga ni mzoefu na sisi tunatoa ushirikiano kwa kocha kwa wachezaji ambao anawahitaji na kuona wataisaidia timu kufanya vizuri baada ya kurejea Ligi Kuu Bara,” kimesema chanzo hicho na kubainisha nyota huyo tayari amejiunga na wenzake kambini.
Dilunga ambaye alikuwa JKT Tanzania, kabla ya kusaini mkataba Mbeya City, alikuwa anafanya mazungumzo na TRA United ambapo hawakufikia mwafaka.
Chanzo hicho kimesema: “Dirisha dogo kila timu inakuwa inataka kuongeza nguvu kikosi chake, haikuwa rahisi kufanikisha saini yake, tunatambua alikuwa anatakiwa na timu nyingi.”