Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amezielekeza Ofisi za Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa Mikoa nchini kuhakikisha zinachukua hatua kwa wadaiwa wote wa kodi ya pango la ardhi.
Mhe. Dkt. Akwilapo ametoa kauli hiyo leo, tarehe 23 Januari, 2026, wakati wa kikao chake na watumishi wa Sekta ya Ardhi kilichofanyika jijini Dodoma.
Amesema Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ina jukumu la kukusanya mapato yatokanayo na Sekta ya Ardhi, hadi sasa imekusanya asilimia 37 ya lengo lake la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 290.
“Ninatambua kuwa kila mkoa umepewa lengo la kukusanya maduhuli; hivyo, kila mmoja wetu atapimwa utendaji wake katika kufikia malengo ya makusanyo yaliyowekwa na mfanye bidii na uonekane unafanya vinginevyo tutakuita na kukuliza kama unatosha hapo ulipo,” amesema.
Ikumbukwe kuwa tarehe 23 Desemba, 2025, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alitoa taarifa kwa umma ya kuwataka wamiliki wote wa ardhi kulipa kodi ya pango la ardhi kufikia Desemba, 2025, kabla Wizara haijaanza kuchukua hatua za kisheria.
Hatua zinazoweza kuchukuliwa kwa wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi ni pamoja na kufikishwa mahakamani na kufutiwa umiliki wa ardhi. Hatua hiyo ni kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi, Sura ya 113, fungu la 48(1), 50, 51 na 52.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya amewataka Makamishina wa Ardhi Wasaidizi wa Mikoa kuyapitia upya maombi yote ya wananchi waliokamilisha taratibu zote za kuomba hati milki za ardhi.