Katika njia isiyo ya kawaida ya siasa za kimataifa, kisiwa cha barafu kikubwa zaidi duniani cha Greenland kimevutia tena hisia kali katika ngazi ya kisiasa ya kimataifa.
Si tu kwamba historia yake ya kale inazungumzia ustaarabu wa binadamu waliojifunza kuishi katikati ya baridi kali, bali leo hii kisiwa hiki kimekuwa kitovu cha mjadala mkali wa kisiasa, kiusalama na kiuchumi.
Katika Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) unaoendelea huko Davos, Rais wa Marekani, Donald Trump ametoa kauli inayogusa dunia zima: Anaamini Marekani inastahili na inahitaji kudhibiti kisiwa cha Greenland.
Kauli hii imeibua lawama kutoka kwa washirika wa Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi (NATO), kusababisha kuitishwa kwa mikutano ya dharura katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa na kuzusha mjadala kuhusu mustakabali wa uhusiano wa kimataifa kati ya Marekani, Denmark na jamii ya Greenland yenyewe.
Lakini, kwa nini Trump amesema anataka kuchukua kisiwa hiki? Je, madai haya yanatokana na sera ya usalama? Au ni mbinu ya kisiasa ya kuchochea kuungwa mkono katika uchaguzi wa ndani ya Marekani?
Greenland ni kisiwa kikubwa zaidi duniani, kikiwa kimefunikwa kwa zaidi ya asilimia 80 na barafu nene isiyoyeyuka kirahisi.
Licha ya sura yake ya ukimya na baridi kali, historia ya Greenland ni simulizi ya ustahimilivu wa binadamu, migongano ya ustaarabu na mabadiliko ya taratibu yaliyokifanya kiwe moja ya maeneo yenye uzito mkubwa wa kijiografia na kisiasa kwenye dunia ya sasa.
Historia ya kisiwa hiki inaanzia maelfu ya miaka kabla ya ujio wa Ulaya yenyewe. Kwa mujibu maandishi ya wanahistoria ya binadamu na tamaduni zao za zamani katika vitabu vya historia ya Arctic, wakazi wa kwanza wa Greenland walikuwa jamii za Paleo-Inuit waliowasili takribani miaka 4,500 iliyopita.
Jamii hizi zikiwamo za Saqqaq, Dorset na baadaye Thule ziliishi kwa kuwinda wanyama wa baharini kama nyangumi na sili, zikitegemea ujuzi wa hali ya juu wa kuishi katika mazingira magumu ya baridi kali. Jamii hizi ni makundi ya kale ya watu wa kaskazini mwa Amerika na Greenland, walioishi katika milenia ya kwanza kabla ya watu wa Inuit wa kisasa.
Makazi ya watu yalipo katika pembezoni mwa Kisiwa cha Greenland kilichopo kaskazini mwa Bahari ya Atlantiki. Picha na Mtandao
Kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa ya 2007, ‘Climate Change In The Arctic: An Inuit Reality’, jamii ya Thule, ambayo ndiyo chimbuko la Wainuit wa leo, iliingia Greenland karibu mwaka 1,200 baada ya Kristo; ikileta teknolojia ya boti za ‘kayaki’ (boti ndogo, nyepesi na ya mwinuko), mikuki ya kuwindia nyangumi na mtandao thabiti wa kijamii. Idadi ya watu katika kipindi hiki ilikuwa ndogo huku makadirio ya kihistoria yakionyesha hawakuzidi 10,000 katika maeneo yote ya kisiwa.
Uvumbuzi wa Ulaya ulianza mwishoni mwa karne ya 10, wakati Erik the Red, Mnorwei aliyefukuzwa Iceland kwa kosa la mauaji, alipoongoza safari kuelekea Magharibi.
Katika mkusanyiko wa maandishi yanayoitwa ‘The Saga of the Greenlanders’, Erik the Red anaelezewa kama mtu mwenye maono makubwa na ujasiri, aliyekipa jina kisiwa hicho “Greenland” kwa lengo la kuwashawishi walowezi zaidi wajiunge naye.
‘The Saga of the Greenlanders’, Erik the Red
Historia inaeleza kuwa makazi ya Wanorwei yalistawi kwa karne kadhaa, yakijikita katika ufugaji na biashara ndogo.
Hata hivyo, maandishi hayo pia yanaonyesha dalili za kuporomoka kwa makazi hayo kutokana na mabadiliko ya tabianchi, kutengwa kijiografia na migongano na jamii za asili.
Greenland na Muungano wa Denmark–Norway
Kuanzia karne ya 14, Greenland iliingia rasmi chini ya muungano wa kifalme wa Denmark na Norway.
Muungano huu uliimarishwa na mamlaka ya Kanisa la Kilutheri na biashara ya kifalme. Hata hivyo, katika kitabu chake, ‘A History of Scandinavia: Norway, Sweden, Denmark, Finland, and Iceland’ (1983), mwandishi T. K. Derry anasema kwa kiasi kikubwa Greenland ilikuwa koloni, ikitawaliwa kwa mbali, bila uwekezaji mkubwa wa maendeleo.
Muungano wa Denmark–Norway ulisambaratika rasmi mwaka 1814 baada ya Vita vya Napoleoni (1803–1815), kupitia Mkataba wa Kiel uliosainiwa Januari 14, 1814 kati ya Denmark na Norway.
Norway ilitenganishwa na Denmark, lakini Greenland, Iceland na Faroe Islands zilibaki chini ya Denmark.
Moja kwa moja hii iliifanya Greenland kuwa mali ya ufalme wa Denmark, na ikaendelea kudhibitiwa na ufalme huo, lakini pia kuendeleza kutengwa kwa Greenland na dunia ya kisasa.
Vita Kuu I & II na mabadiliko ya hatima
Vita Kuu I (1914—18) havikuigusa Greenland moja kwa moja, lakini Vita Kuu II (1939—45) vilibadilisha historia yake kwa kiasi kikubwa.
Denmark ilipovamiwa na Ujerumani mwaka 1940, Greenland ilijikuta katika hali ya kipekee ya dharura kiutawala.
Marekani, kwa hofu ya Ujerumani kutumia Greenland kama kituo cha kijeshi, iliingia makubaliano na balozi wa Denmark huko Washington DC., Henrik Kauffmann, kulinda kisiwa hicho.
Katika kitabu ‘Politics and Development in the North American Arctic’ cha waandishi Roman Czarny, Magdalena Tomala na Iwona Wrońska, inaelezwa kuwa Marekani ilijenga viwanja vya ndege na vituo vya kijeshi Greenland, hatua iliyoiweka Greenland moja kwa moja katika ramani ya usalama wa kimataifa. Idadi ya watu wakati huo ilikuwa takribani 22,000.
Mkataba wa Ulinzi, Vita Baridi
Mwaka 1951, Denmark na Marekani zilisaini Mkataba wa Ulinzi wa Greenland ambao ulihusisha Serikali ya Marekani na Serikali ya Ufalme wa Denmark Aprili 27, 1951.
Mkataba huu, uliotiwa saini na wawakilishi wa serikali zote mbili, uliiruhusu Marekani kujenga na kuendesha vituo vya kijeshi, ikiwamo ‘Thule Air Base’ (sasa Pituffik Space Base), bila kudai umiliki wa kisiwa hicho.
Katika kipindi cha Vita Baridi, Greenland ikawa kituo muhimu cha ufuatiliaji wa mapema wa makombora ya masafa marefu, hasa kutoka Umoja wa Kisovyeti.
Kwa mujibu wa ‘Encyclopaedia Britannica’ nafasi ya Greenland katika Arctic ilifanya iwe ngao ya kwanza ya ulinzi wa Marekani dhidi ya mashambulizi ya nyuklia.
Idadi ya watu, hadhi ya kisasa
Leo, Greenland ina idadi ya watu takribani 56,000, wengi wao wakiwa Wainuit. Licha ya kuwa raia wa Denmark, Greenland ina hadhi ya kujitawala (Home Rule 1979, Self-Government 2009), ikihifadhi lugha, tamaduni na kumbukumbu zake za kihistoria.
Muonekano wa makazi ya watu yalipo katika Kisiwa cha Greenland kaskazini mwa Bahari ya Atlantiki. Picha na Mtandao
Kutoka katika historia yake ya kale hadi karne ya 20, Greenland imejijengea sifa ya kisiwa cha kipekee kinachounganisha ustahimilivu wa binadamu na umuhimu wa kimkakati wa kisasa.
Kutoka kwa jamii za Paleo-Inuit, kupitia wavumbuzi wa Ulaya, hadi uhusiano wa kisiasa na kijeshi na Marekani katika Vita Baridi, Greenland imeonyesha kuwa kisiwa hiki si tu ni eneo la baridi kali, bali ni kiini cha historia, usalama na nguvu ya kimataifa.
Historia yake inaonyesha uwiano mgumu kati ya ukuaji wa jamii za kibinadamu, nguvu za kigeni, na nafasi ya kipekee ya kijiografia, mfumo ambao leo unaendelea kuunda mjadala mkali wa kisiasa duniani.
Muonekano wa makazi ya watu yalipo katika Kisiwa cha Greenland. Picha na Mtandao
Hata hivyo, historia haionyeshi yote. Katika karne ya 21, Greenland imeibuka kuwa kitovu cha nguvu, rasilimali na mvutano wa kimataifa, likiweka mbele maswali makubwa kuhusu usalama, uhuru na haki za kisiasa.
Ni kisiwa ambacho sasa kinatazamwa kwa umakini na mataifa makubwa kama Marekani na China, huku mabadiliko ya tabianchi na fursa za rasilimali yakibadilisha ramani ya kisiasa ya Arctic.
Katika toleo lijalo, tutaingia kwa kina katika jiografia ya nguvu ya Greenland, rasilimali zake zinazoweza kubadilisha teknolojia za dunia, na mvutano wa kisiasa unaoibua ujumbe ambao, hauna budi kusoma kwa kila anayependa kuelewa mustakabali wa siasa za kimataifa.