Hatua za dharura zachukuliwa maagizo ya ukamilishaji bweni la sekondari Iringa

Iringa. Baada ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Heri James kutoa amri ya kuendelea kwa ujenzi na uwekeaji wa vigae katikq bweni la Shule ya Sekondari ya Lugalo Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imeanza hatua za dharura kushughulikia ucheleweshaji katika mradi huo.

James alitoa maelekezo Januari 20, 2026 na kutoa siku saba kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana  na Rushwa ( Takukuru ) na Mkurugenzi  kuwasilisha yanayoeleza sababu za uzembe, upungufu au kuongezekana kwa fedha katika mradi huo pamoja na hatua zitakazochukuliwa.

“Kwa maofisa ambao Takukuru haitaweza kuwahoji kutokana na na nafasi walizonazo, aliagiza kuandaliwa mapendekezo yatakayowasilishwa kwa Katibu Tawala wa Wilaya (Ras) ili wawachukulie hatua stahiki.

Hata hivyo, mradi huu ulianza kwa lengo la kupunguza uhaba wa malazi kwa wanafunzi na kuboresha mazingira ya kujifunzia lakini ulisimama kwa muda kutokana na ucheleweshaji wa malipo na changamoti za kiutendaji.

Akizungumza Januari 22, 2026 wakati wa ziara ya ufuatiliaji, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Zaina Mlawa, amesema kazi za ujenzi zimeanza tena kwa nguvu, zikiwemo kuweka vigae na ukamilishaji wa shughuli nyingine zilizokuwa zimesimama.

“Tumeshachukua hatua za vitendo, kazi zinaendelea, na tunatarajia ifikapo Februari 15, 2026, ujenzi wa bweni hili utakuwa umekamilika.

Aidha, Mkurugenzi Zaina amesema kuwa mwezi wa saba bweni litakuwa tayari kupokea wanafunzi katika shule ya sekondari Lugalo.

Mkurugenzi Zaina ameongeza kuwa fedha za mradi huo tayari zimetolewa, na Halmashauri imejipanga kuhakikisha wazabuni na mafundi wanalipwa kwa wakati, kwa mujibu wa mikataba yao, ili kuepusha ucheleweshaji zaidi wa miradi ya maendeleo.

Hatua hizo za haraka zimetokana na maelekezo ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa,  Kheri James, ambaye aliagiza uchunguzi kufanyika ili kubaini chanzo cha ucheleweshaji wa malipo na kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ufanisi.

Pia, halmashauri imesema kuwa imetenga mikakati madhubuti ya kusimamia miradi yote ya maendeleo mkoani Iringa, kuhakikisha fedha za Serikali zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuwaletea wananchi tija inayotarajiwa.

Wazabuni na mafundi waliokuwa wamechelewa kulipwa wameonyesha kuridhishwa na hatua za haraka za halmashauri na kuahidi kushirikiana kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.

“kuna vitu havikwenda sawa lakini sasa hivi wakubwa washamlyamaliza kila kitu sasa kipo na kufikia Februari ujenzi utakamilika.”amesema Dickson Mlyuka mmoja wa wazabuni wa mradi wa ujenzi wa bweni hilo kutoka mkoani Iringa huku akiongeza kuwa

“Kuna vitu havikwenda sawa lakini sasa hivi wakubwa washayamaliza kila kitu kitakwenda vizuri,”.

Kwa upande wao wananchi na wadau wa elimu kutokea Halmashauri ya Manispaa ya Iringa wamesema kuwa wanapongeza hatua zilizochukuliwa huku wakieleza kuwa kukamilika kwa bweni hilo kutapunguza changamoto ya uhaba wa malazi na kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.

Wananchi hao wamesisitiza kuwa ni muhimu miradi kukamilika bila kucheleweshwa kwa sababu ya usimamizi wa kiutendaji.

“Mara nyingi miradi inacheleweshwa kwa kusubiri kila kitu kisimamie kikamilifu, lakini si sahihi kuacha mpaka hapo kwani mradi unapaswa kukamilika kwa wakati huku usimamizi ukifuatiliwa sambamba,” amesema mkazi wa Manispaa ya Iringa ambaye hakutaka jina lake litambulike

Nao wadau wengine wa elimu na wazazi wamesema kuwa hatua za haraka zinapaswa kuendelezwa katika miradi mingine, ili kuhakikisha maendeleo ya shule na malazi ya wanafunzi hayatatozwa, huku usimamizi ukiwa endelevu na madhubuti.

Mradi huo wa bweni la wasichana Lugalo una thamani ya Sh159 milioni na unashughulikia mahitaji ya muda mrefu ya malazi kwa wanafunzi wa kike na wa kiume, na kukamilika kwake kunatarajiwa kuongeza motisha kwa shule hiyo na kukuza maendeleo ya elimu mkoani Iringa.