Karata ya Pedro Misri ipo hapa!

YANGA tayari ipo jijini Alexandria, Misri kuvaana na wenyeji Al Ahly katika mechi ya Kundi B, huku wawakilishi hao wa Tanzania wakiwa na matumaini na kuendelea ilipoishia na kuwatoa hofu mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo wakiwataka wawaombee dua tu ili wawape raha ugenini.

Kitendo cha Kocha Pedro Goncalves kuiongoza Yanga kucheza mechi 10 za mashindano tofauti bila ya kupoteza huku akishinda tisa na sare moja tangu atue Novemba 2025, kwa namna moja ama nyingine inampa jeuri ya kukabiliana kibishi na mabingwa wa kihistoria wa Afrika.

Mbali na hilo, majembe mapya yaliyotua Yanga kipindi cha dirisha dogo kuja kuongeza nguvu, pia yanampa jeuri Mreno huyo kuendelea kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Kilichobaki ni dua tu za Watanzania, wawakilishi wetu hao wafanye vizuri kwani wenyewe wamesema; “Msiwe na hofu, tutapambana nao.”

Al Ahly itakuwa mwenyeji wa Yanga katika mechi ya michuano hiyo itakayochezwa leo Ijumaa kwenye Uwanja wa Borg El Arab uliopo Alexandria nchini Misri kuanzia saa 1 usiku. Uamuzi wa Al Ahly kuitoa mechi hiyo Uwanja wa Cairo na kwenda Borg El Arab, imeelezwa ni mkakati wa kuhakikisha inashinda kwani huwa inautumia inapoona mechi ni ngumu kwao.

YANG 01


Yanga si wageni wa uwanja huo kwani waliwahi kupelekwa na wapinzani wao hao Aprili 20, 2016 na kupasuka mabao 2-1 wakatolewa katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya awali kutoka sare ya bao 1-1 jijini Dar na kushindwa kutinga makundi.

Al Ahly imeishtukia Yanga sio timu ya kuibeza kutokana na ilivyoanza kampeni yake kimataifa msimu huu kwani mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara, hivi sasa wanavutana shati na Waarabu hao katika msimamo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika kundi B la michuano hiyo, Al Ahly ina pointi nne sawa na Yanga, lakini Waarabu wapo juu kwa tofauti ya mabao, hivyo wanataka kuhakikisha wanashinda nyumbani, ili watakaporudiana ugenini nafasi yao ya kuendelea kukaa juu iwe palepale hata wakipoteza.

“Tupo tayari kukutana na Al Ahly ambayo ni timu ngumu na yenye rekodi bora Afrika. Tunazijua taarifa zao lakini jambo zuri ni tuna timu imara, tumefanya usajili uliotufanya kuwa na kikosi kilicho na uwiano mzuri.

“Nina furaha na ubora wa wachezaji wangu, tunakwenda kutumia ubora wa kikosi chetu kutafuta matokeo ya aina mbili tu, kushinda au kutoa sare, haitakuwa mechi rahisi lakini hatuwezi kuwa timu ambayo itasubiri wapinzani wetu kuamua mchezo,” alisema Pedro kuelekea mechi hiyo.

YANG 02


DEPU, DUBE WABEBA TUMAINI

Yanga imesajili wachezaji watano dirisha dogo wakiwemo kipa Hussein Masalanga, viungo Mohammed Damaro, Allan Okello na washambuliaji Emmanuel Mwanengo pamoja na Laurindo Aurélio ‘Depu’. Pia imemrudisha kwenye mfumo Kouassi Attohoula Yao aliyepona majeraha yaliyomweka nje ya uwanja muda mrefu jambo ambalo Pedro anajivunia nyota hao akiamini wanachokifanya kwenye uwanja wa mazoezi, kitatoa majibu mazuri uwanja wa mechi.

“Ukiangalia kuanzia mazoezini kuna ari imeongezeka ya kupigania nafasi. Kila mchezaji anajituma zaidi. Hali kama hii itatupa nafasi ya kufanya uamuzi mzuri wa nani aanze au nani acheze mechi ipi. Tuna timu pana ambayo sasa tunaweza kuchagua mifumo bora zaidi lakini kutoa nafasi kwa kila mchezaji kucheza, kama nilivyokwambia tuna mechi nyingi kutoka mashindano tofauti, lazima tuwe na hesabu za kuwapumzisha wachezaji,” alisema Pedro.

YANG 03


Mbali na nyota hao wapya, Yanga eneo la ushambuliaji kuna Prince Dube ambaye ameanza vizuri hatua ya makundi akipachika bao moja lililoipa Yanga ushindi wa kwanza 1-0 dhidi ya AS FAR Rabat.

Wakati Pedro akitambia majembe yake hayo, Al Ahly nao sio kinyonge kwani Januari hii imeingiza mashine tano mpya ikionekana kuimarisha zaidi ulinzi.

Nyota wapya waliotua kwa Waarabu hao ni Ahmed Eid (beki wa kulia), Youssef Belammari (beki wa kushoto), Amr El Gazar (beki wa kati), Abdelrahman Rashdan (beki wa kati) na Marwan Otaka (winga).

YANG 04


Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, timu hizi tayari zimekutana mara nane kwenye hatua tofauti huku ikishuhudiwa Yanga ikipata ushindi mara moja pekee.

Machi 1, 2014, Yanga iliichapa Al Ahly bao 1-0 kupitia Nadir Haroub ‘Canavaro’ dakika ya 84, mechi ya hatua ya kwanza iliyochezwa jijini Dar es Salaam, zilipokwenda kurudiana Misri, Waarabu hao walishinda 1-0, kisha penalti wakashinda tena 4-3 na kuitupa nje Yanga.

Rekodi zinaonyesha timu hizo katika mechi nane walizokutana, hakuna iliyomalizika bila bao, hivyo inatoa picha leo suala la nyavu kutikiswa ni la kusubiri tu muda ufike tuone.

Katika mechi hizo nane ambazo Al Ahly imeshinda tano, Yanga ikishinda moja na sare mbili ambazo zote ilikuwa jijini Dar, yamefungwa mabao 14 ndani ya muda wa kawaida, Yanga ikipachika manne na Al Ahly ikiwa nayo kumi.

Mara zote Yanga ilipokwenda nyumbani kwa Al Ahly, haijawahi kushinda wala kupata sare, imepoteza zote nne, hivyo Pedro leo ana mtihani wa kukiongoza kikosi kuweka rekodi ya kuambulia pointi kwa mara ya kwanza dhidi ya Waarabu hao wakiwa ugenini.

YANG 05


Mbali na hilo, kile ambacho kimetokea msimu huu kwa timu hizo hadi kufikia hapa, inaonyesha zote zimekuwa na muda unaofanana katika ufungaji wa mabao na kuashiria kwamba mechi inaweza kuamulia wakati huo.

Al Ahly iliyoanzia hatua ya pili na kufuzu makundi, hadi sasa imecheza mechi nne ikishinda tatu na sare moja, huku ikifunga mabao saba na kuruhusu mawili. Mabao iliyoruhusu yote ni hatua ya makundi.

Katika mabao hayo saba, matatu yamefungwa ndani ya dakika 15 za kuelekea kuhitimisha kipindi cha kwanza, huku kipindi cha pili ikifunga manne. Moja ndani ya dakika 15 za kwanza kipindi cha pili na mawili dakika kumi za mwisho. Moja lilifungwa hapo kati kati.

Yanga ilianzia hatua ya awali, tayari imecheza mechi sita, ikishinda nne, sare moja na kupoteza moja, imefunga mabao manane, imeruhusu moja.

YANG 06


Vijana hao wa Jangwani nao ni wazuri kutumia dakika 15 za mwisho kipindi cha kwanza kwani kati ya mabao hayo manane, mawili yamepatikana muda huo na mawili mengine yamefungwa dakika 10 za mwisho. Pia bao moja imefunga dakika 15 za kwanza kipindi cha pili.

Leo huenda tukashuhudia dakika 15 za mwisho kumalizia kipindi cha kwanza, au zile 15 za mwisho kabla ya mechi kumalizika bao au mabao yakapatikana kutokana na rekodi za timu zote zilivyo.

Al Ahly licha ya ukali wao, lakini ina kazi ya kufanya mbele ya Yanga iliyonyesha ukomavu mkubwa katika kujilinda kwani msimu huu katika Ligi ya Mabingwa Afrika, ipo na Pyramids pekee kwa timu ambazo hazijaruhusu nyavu zao kutikiswa hadi sasa ikiwa ni raundi ya pili imeshachezwa.