Morogoro.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, ameridhishwa na hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa katika mradi wa Kiwanda cha Sukari Mkulazi, akisema kuwa ndani ya muda mfupi kiwanda hicho kitaanza kujiendesha kwa faida, jambo linaloendana na maono ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuridhia kuendelea kwa mradi huo wa kimkakati.
Mhe. Sangu alisema hayo tarehe 22 Januari, 2026, wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya mradi huo, akiwa ameambatana na wabia wa kiwanda hicho akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, pamoja na Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza, ACP Dominic Kazmil. Kiwanda hicho kinamilikiwa kwa ubia na NSSF pamoja na Jeshi la Magereza kupitia shirika lake la uzalishaji mali (SHIMA).
“Niwapongeze sana wawekezaji wa mradi huu NSSF na Jeshi la Magereza. Kama Serikali, tunashukuru sana kwa mchango mkubwa wa mradi huu katika kuzalisha ajira, jambo ambalo ndilo muelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema Mhe. Sangu.
Alibainisha kuwa mradi huo tayari umeanza kuleta tija kwa Taifa na jamii kwa ujumla, ambapo hadi sasa umeweza kuzalisha ajira za moja kwa moja 1,920 na ajira zisizo za moja kwa moja takribani 8,000 ndani ya muda mfupi tangu ulipoanza kutekelezwa.
Mhe. Sangu alisema manufaa ya kiwanda hicho ni pamoja na kuchochea uchumi wa nchi, kuongeza mapato ya kodi, kuzalisha ajira kwa Watanzania na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja, hususan kwa jamii inayozunguka kiwanda hicho.
“Kiwanda hiki ni cha kimkakati na kinatekeleza maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuacha tabasamu kwa Watanzania, kwani tayari mradi huu umeanza kuleta mabadiliko makubwa kwa Taifa na jamii kwa ujumla,” alisema.
Aidha, aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara zinazounganisha mashamba ya wakulima wadogo wa miwa na kiwandani, hatua inayorahisisha usafirishaji wa miwa kutoka mashamba hayo kwenda kiwandani.
Aliahidi kuufuatilia mradi huo kwa karibu ili kuhakikisha unatimiza lengo la kupunguza nakisi ya sukari nchini, akieleza kuwa katika mwaka wa uzalishaji 2027/2028 kiwanda kinatarajiwa kuzalisha tani 50,000 za sukari.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni Hodhi ya Mkulazi, Dkt. Hildelitha Msita, aliishukuru Serikali kwa kuwekeza katika miradi inayogusa maisha ya wananchi na kukuza uchumi, huku akiahidi kuendelea kuusimamia mradi huo kwa weledi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NSSF aliishukuru Serikali kwa usimamizi mzuri wa mradi huo, akibainisha kuwa kama wabia watahakikisha kiwanda kinasimamiwa ipasavyo ili malengo ya mradi yatimie na kuleta faida endelevu kwa wanachama na Taifa kwa ujumla.
ACP Kazmil alisisitiza kuwa ushirikiano uliopo kati ya NSSF na Jeshi la Magereza umechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya mradi huo.
Diwani wa Kata ya Mkulazi, Edward William, aliishukuru Serikali kwa uwekezaji wa kiwanda hicho, akisema kuwa kimeleta manufaa makubwa kwa wananchi wa kata hiyo kupitia ajira, fursa za kiuchumi na uboreshaji wa huduma za kijamii.



















