Lupembe jela miaka 28, kwa kukiri kosa la kusafirisha kilo 268 za heroine

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, maarufu “Mahakama ya Ufisadi, imemhukumu Isso Lupembe (55) kifungo cha miaka 28 gerezani baada ya kumtia  hatiani kwa kosa la kusafirisha kilo 268.50 za dawa za kulevya aina ya Heroine.

Lupembe alikuwa anakabiliwa kesi ya uhujumu uchumi kwa shtaka moja la kusafirisha kilo 268.50 za dawa za kulevya aina ya Heroine, yeye na wenzake watatu, Allistair Mbele (43) mkazi wa Mbezi Kibanda cha Mkaa pamoja na  raia wa Nigeria, David Chukwu(43).

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka   walitenda kosa hilo April 15, 2020 eneo la Mbezi Kibanda cha Mkaa.

Hata hivyo, Lupembe ametiwa hatiani baada ya kukiri shtaka hilo, wakati wa usikilizwaji wa awali, ambapo Jamhuri iliwasomea hoja za awali kabla ya kesi hiyo kuanza usikilizwaji wa mashahidi wa upande wa mashtaka.

Hukumu hiyo dhidi ya Lupembe imetolewa jana Januari 22, 2026 na  Jaji Monica  Otaru , baada ya Lupembe kukiri shtaka lake.

Wakati Lupembe akitiwa hatiani kwa kosa hilo, kutokana na kukiri kwake, mshtakiwa mwingine Alistair Amon Mbele, yeye ameachiwa huru na Mahakama hiyo,  baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini ( DPP) kumuondolea shtaka .

DPP ameieleza mahakama hiyo hana  nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya mshtakiwa huyo kwa mamlaka aliyo nayo chini ya kifungu cha 92 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), Marejeo ya mwaka 2023.

Hata hivyo, mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, David Chukwu(43) ambaye ni raia wa Nigeria yeye hajakiri shtaka hilo, hivyo anaendelea na kesi hiyo.

Awali, kabla ya kutolewa hukumu, wakili wa Serikali Elizabeth Muhangwa na Phoibe Magili, waliieza mahakama hiyo kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa hoja za awali na kisha kuendelea na usikilizwa na upande wa Jamhuri.

Waliieleza mahakama kuwa upande wa Jamhuri  wako tayari kuwasomea maelezo hayo na kwa ajili ya kuanza usikilizwaji.

Washtakiwa nao walieleza kuwa wapo tayari kusomea hoja za awali.

Baada ya kukumbushwa shtaka lao na kusomewa hoja za awali, mshtakiwa Chukwu na Mbele walikana mashtaka yao, huku mshtakiwa Lupembe akikiri kosa ndipo mahakama ikamtia hatiani kwa kosa hilo na kisha kumhukumu adhabu hiyo.

” Mahakama  imezingatia muda wa miaka mitano na miezi tisa ambao mshtakiwa amekaa rumande tangu alipokamatwa,” alisema Jaji Otaru na kuongeza:.

“Hivyo kutokana na hilo, mahakama imeelekeza kuwa atatumikia kifungo cha miaka 22 na miezi mitatu iliyobaki ili kukamilisha adhabu yake ya miaka 28.”

Kuhusu mshtakiwa Mbele, Jaji Otaru alisema kuwa kwa kuwa DPP amewasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya mshtakiwa huyo, mahakama hiyo inamuachia huru bila masharti mshtakiwa huyo.

Jaji Otaru kuwa  alisema kuhusu mshtakiwa Chukwu ambaye yeye hajakiri shtaka lake, kesi dhidi yake itaendelea  Februari 23, 2026 kuwa usikilizwaji, hivyo kwa kipindi hicho chote ataendelea kusalia rumande.

Baada ya kueleza hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 23, 2026 kwa ajili ya usikilizwaji ambapo upande wa mashtaka unatakiwa kupeleka mashahidi.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa aliyebakia katika kesi hiyo anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 36 ya mwaka 2020.

Anadaiwa kutenda kosa hilo  Aprili 15,  2020, eneo la Mbezi, Kibanda cha Mkaa.

Anadaiwa kuwa  siku hiyo maofisa wa DCEA, walimkamata yeye na wenzake  wakisafirisha dawa za kulevya  aina ya heroine zenye uzito wa kilo kiasi 268.50, kinyume cha sheria.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu Aprili 24, 2020  na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi.

Kutokana na shtaka linalowakabili halina dhamana washtakiwa hao walipelekwa mahabusu gerezani wakisubiri kesi yao kuamuliwa.