Makosa ya barabarani Zanzibar yaongezeka kwa asilimia 43, ya jinai yakipungua

Unguja. Wakati makosa ya jinai yakipungua kwa asilimia 24.1 katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2025, visiwani Zanzibar, makosa ya barabarani yameongezeka kwa asilimia 43.

Akitoa taarifa kuhusiana na tathmini ya hali ya usalama Zanzibar leo Januari 23, 2026, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Kombo Khamis Kombo amesema makosa ya barabarani yaliyoongezeka ni 21,479 na katika ajali zilizotokea, waliopoteza maisha ni 206 ikilinganishwa na vifo 175 mwaka 2024 huku waliojeruhiwa wakiwa 258 mwaka 2025 ikilinganishwa na majeruhi 259.

Kamishana Kombo amesema makosa ya ukamataji yameongezeka kutoka 50,016 mwaka 2024 hadi kufikia makosa 71,495 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 43 huku polisi wakiendelea kuchuku hatua za udhibiti na elimu kwa watumiaji wa barabara.

Katika ajali hizo, wanaume waliopoteza maisha mwaka 2025 ni 210 na wanawake ni 23 ikilinganishwa na wanaume 149 waliofariki dunia mwaka 2024 huku wanawake wakiwa 18.

Majeruhi wanaume walikuwa 211 mwaka 2025 ikilinganishwa na majeruhi 187 mwaka 2024 huku wanawake walikuwa 47 mwaka 2025 ikilinganishwa 72 ya mwaka 2024.

“Jamii yetu inapaswa kutafakari kwa kina juu ya takwimu hizi za ajali za barabarani, idadi bado ni kubwa na ya kusikitisha, hasa ikizingatiwa kuwa waliofariki zaidi ni wanaume ambao ndio nguvu kazi ya taifa,” amesema.

Kamishna Kombo amesema ili kupunguza ajali za barabarani kunahitajika ushirikianao wa polisi, waandishi wa habari na wananchi kwa pamoja.

Wakizungumzia takwimu hizo, wadau wa usafirishaji wametaja miongoni mwa changamoto kuwa ni kutozingatia sheria barabarani kwa waendesha vyombo vya moto kwani bado wanakwenda mwendo wa kasi na kushindwa kudhibiti vyombo vyao.

Fatma Khamis Ali, mdau wa usafiri barabarani amesema: “Waendesha vyombo vya moto mara nyingi hawazingatii sheria, mwendo kasi na kutozingatia alama za usalama, kwa hiyo hili linaweza kuwa sababu ya kuongeza ajali.”

Naye Soud Haji, mtaalamu wa masuala ya haki za binadamu amesema makosa ya barabarani yanaendelea kugharimu maisha ya watu kwa sababu ya kufanya kazi kwa mazoea.

“Kuna haja askari wetu wa usalama barabarani wakabadilishwa maana kuna kuzoeana, kwa hiyo wakati mwingine makosa yanafanyika lakini hakuna hatua kubwa zinazochukuliwa,” amesema.

Akizungumza kuhusu makosa ya jinai, Kamishna Kombo amesema wamepokea makosa 2,386 kwa kipindi cha Januari hadi Desemba ikilinganishwa na makosa ya 3145 yaliyoripotiwa kwa kipindi kama hicho mwaka 2024 sawa na punguzo la makosa 759.

Amesema makosa dhidi ya binadamu yamepungua kutoka 1,116 hadi makosa 812 mwaka 2026, sawa na upungufu wa asilimia 27.2 huku makosa ya mauaji yakiwa 53, ikilinganishwa na makosa 66, sawa na pungufu ya asilimia 19.7.

“Katika makosa haya, kujichukulia sheria mkononi ni asilimia 94, wivu wa kimapenzi ni asilimia nne na ugomvi vilabuni ni asilimia mbili,” amesema.

Katika makosa ya kubaka yaliyoripotiwa yalikuwa 657 kutoka makosa 829, kulawiti makosa 93 ikilinganishwa na makosa 217, sawa na asilimia 57.1.

Kwa mujibu wa Kamishna Kombo, upungufu huo umetokana na elimu kwa jamii, hususani kuhusu madhara ya vitendo hivyo na ulinzi wa mtoto, pia, kuendelea kutoa elimu kuhusu matakwa ya kisheria yanayohusiana na umri na ridhaa.

Katika makosa ya kubaka pekee, yapo 657, kati ya hayo, makosa 450 wahusika ni wasichana na wavulana ni wapenzi waliokubaliana wenyewe kwa ridhaa yao, lakini kutokana na takwa la kisheria, msichana mwenye umri chini ya miaka 18 hutambulika kuwa bado ni mtoto mdogo. Hivyo makosa halisi ya kubaka yapo 207.

Kamishna amesema changamoto nyingine ambayo inajitokeza mbele ya mahakama katika kutoa ushahidi ni baadhi ya mashahidi wasichana kukataa kosa la kubakwa na kuendelea kumtetea mtuhumiwa kuwa hakumbaka bali wao ni wapenzi na na walifanya mapenzi kwa hiari yao, wakati mwingine hukana mbele ya mahakama kutomfahamu mtuhumiwa.

Kwa upande wa makosa ya kuwania mali, yamepungua kutoka 1,855 hadi kufikia makosa 1,481, sawa na asilimia 20 huku uvunjaji yameripotiwa makosa 580, ikilinganishwa na makosa 823, sawa na asilimia 29.5. Vilevile, wizi wa mifugo umepungua kwa asilimia 1.6 kutoka makosa 370 hadi 364.

Katika hatua nyingine, amesema katika kipindi husika, kesi 531 zimepata mafanikio mahakamani, kesi 307 zimefutwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mashahidi kutofika mahakamani kwa ajili ya kutoa ushahidi na kesi 174 zimefutwa vituo vya polisi huku kesi 41 zikiwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka.

Amesema kesi 62 zimehamishiwa Mamlaka ya Kuzuai na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na kesi 567 zipo chini ya upelelezi na kesi 704 zinaendelea kusikilizwa mahakamani zikiwa katika hatua mbalimbali.