Dodoma. Kujiondoa kwa Marekani katika Shirika la Afya Duniani (WHO) kunaweza kudhoofisha mifumo na ushirikiano ambao dunia inategemea kugundua, kuzuia na kukabiliana na vitisho vya kiafya, wamesema wataalamu wa afya ya dunia.
Marekani imetangaza kujiondoa rasmi katika WHO jana Alhamisi, Januari 22, 2025 baada ya mwaka mmoja wa onyo kuwa hatua hiyo ingeathiri afya ya umma nchini Marekani na duniani kote.
Serikali ya Marekani imesema uamuzi huo unatokana na kile ilichokitaja kuwa ni kushindwa kwa WHO katika usimamizi wa janga la Uviko-19.
Rais Donald Trump alitoa notisi ya kujiondoa WHO siku ya kwanza ya urais wake Januari mwaka 2025 kupitia amri ya utendaji.
Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja kutoka Idara ya Afya na Idara ya Mambo ya Nje ya Marekani, nchi hiyo itashirikiana na WHO kwa kiwango kidogo tu ili kukamilisha mchakato wa kujiondoa.
“Hatujapanga kushiriki hata kama waangalizi, wala hatuna mipango ya kurejea,” amesema Ofisa mwandamizi wa serikali anayeshughulikia afya. Marekani imesema inapanga kufanya kazi moja kwa moja na nchi nyingine badala ya kupitia mashirika ya kimataifa katika ufuatiliaji wa magonjwa na vipaumbele vingine vya afya ya umma.
Maana ya kujiondoa
Kujiondoa kwa Marekani kumesababisha mgogoro wa kifedha uliolilazimu WHO kupunguza timu yake ya usimamizi kwa nusu na kupunguza utekelezaji wa kazi, huku bajeti zikikatwa katika shirika lote.
Kwa muda mrefu, Marekani imekuwa mfadhili mkubwa zaidi wa shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa, ikichangia takribani asilimia 18 ya ufadhili wake wote. WHO pia itapunguza takribani robo ya wafanyakazi wake ifikapo katikati ya mwaka huu wa 2026.
Shirika hilo limesema limekuwa likishirikiana na Marekani na kubadilishana taarifa katika mwaka uliopita, lakini haijulikani ushirikiano huo utaendeshwaje kuanzia sasa.
Wataalamu wengi wa afya ya dunia wamekuwa wakihimiza uamuzi huo upitiwe upya, akiwemo hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus.
WHO pia imesema kuwa Marekani bado haijalipa ada inazodaiwa kwa miaka ya 2024 na 2025.
Nchi wanachama zinatarajiwa kujadili kujiondoa kwa Marekani na namna ya kushughulikia suala hilo katika kikao cha bodi ya utendaji cha WHO Februari mwaka huu.
Wataalamu wa afya ya dunia wamesema hali hiyo inaleta hatari kwa Marekani, WHO na dunia kwa ujumla.
“Kujiondoa kwa Marekani kutoka WHO kunaweza kudhoofisha mifumo na ushirikiano ambao dunia inategemea kugundua, kuzuia na kukabiliana na vitisho vya kiafya,” amesema Kelly Henning, kiongozi wa programu za afya ya umma katika Bloomberg Philanthropies, shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake Marekani.
“Huu ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za Marekani. Lakini kuna uwezekano mkubwa Trump akapita bila kuwajibishwa,” amesema Lawrence Gostin, mwanzilishi na mkurugenzi wa Taasisi ya O’Neill ya Sheria ya Afya ya Dunia katika Chuo Kikuu cha Georgetown, Washington.
Bill Gates, mwenyekiti wa Taasisi ya Gates, mfadhili mkubwa wa miradi ya afya ya dunia na baadhi ya kazi za WHO ameiambia Reuters akiwa Davos kuwa hatarajii Marekani kubadili msimamo wake kwa haraka.
Gates amesema ataendelea kushawishi Marekani irejee. “Dunia inalihitaji Shirika la Afya Duniani,” amesema.
Akizungumza na Mwananchi leo, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) Dk Mugisha Nkoronko amesema Marekani amekuwa akitimiza majukumu yake WHO kwa miaka mingi.
Walakini amesema kila taifa lina maazimio yake ya kuingia kama mwanachama na kupeleka kwenye mabunge yanayopitia mifumo yake wanakubali na wanapima maslahi yao binafsi, kama jambo lina matokeo hasi au chanya waendelee au wasiendelee.
“Marekani inajitoshemeleza kwa mambo mengi bila kuhitaji uwezo wa dunia, hata hivyo inawajibika kwa afya ya dunia kwani magonjwa hayana mipaka, kwa mantiki hiyo WHO ilitufanya tuwe wamoja, kujitoa kwao kutaleta mkwamo mkubwa kifedha,” amesema Dk Nkoronko.
Chini ya sheria za Marekani, ilipaswa kutoa notisi ya mwaka mmoja na kulipa ada zote zinazodaiwa takribani dola milioni 260 kabla ya kujiondoa.
Hata hivyo, Ofisa wa Idara ya Mambo ya Nje alipinga tafsiri kwamba sheria hiyo inaweka sharti la malipo kufanywa kabla ya kujiondoa.
“Wananchi wa Marekani tayari wamelipa zaidi ya inavyotosha,” msemaji wa Idara ya Mambo ya Nje alisema kupitia barua pepe mapema jana Alhamisi.
Idara ya Afya na Huduma za Kibinadamu (HHS) ilisema katika waraka uliotolewa Alhamisi kuwa serikali imekoma kutoa michango yake ya kifedha kwa WHO.
Trump alitumia mamlaka yake kusitisha uhamishaji wa rasilimali zozote za serikali ya Marekani kwenda WHO, akidai shirika hilo liliigharimu Marekani trilioni za dola, alisema msemaji wa HHS.
Katika wiki za karibuni, Marekani imechukua hatua za kujiondoa kwenye mashirika mengine kadhaa ya Umoja wa Mataifa, hali iliyozua hofu miongoni mwa baadhi ya wadau kuwa Bodi ya Amani iliyoanzishwa hivi karibuni na Trump inaweza kudhoofisha UM kwa ujumla.
Wakosoaji kadhaa wa WHO pia wamependekeza kuanzishwa kwa shirika jipya kuchukua nafasi ya WHO, ingawa waraka wa pendekezo uliopitiwa na utawala wa Trump mwaka jana ulipendekeza badala yake Marekani isukume mageuzi na uongozi wa Wamarekani ndani shirika hilo.