Mwanza. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amezindua rasmi meli ya Mv New Mwanza, ambayo ni kubwa zaidi katika ukanda wa Afrika inayofanya kazi katika maji matamu, ikiwa na kimo cha ghorofa nne, urefu wa mita 92.6, upana wa mita 17 na uzito wa tani 3, 500.
Baada ya uzinduzi huo uliofanyika leo Januari 23, 2026, Dk Mwigulu ameelekeza Menejimenti ya Wizara ya Uchukuzi kuhakikisha ujuzi uliopatikana kwenye ujenzi wa meli hiyo unaendelezwa.
Ameitaka Kampuni ya Meli Tanzania (Tashico) ishirikiane na wadau wengine kuhakikisha usalama wa wasafiri, waitunze meli hiyo ipasavyo na kuhakikisha usafiri wa majini unakuza diplomasia, uchumi na mahusiano kati ya Tanzania na nchi jirani kupitia meli hiyo.
Vilevile, amewataka wazingatie masuala ya bima kama sheria inavyoelekeza.
Mapema, Mkurugenzi Mtendaji wa Tashico, Eric Hamissi amesema ujenzi huo umekuwa somo kubwa linalojumuisha usanifu wa michoro, uwekaji wa mkufu wa meli kwenye cherezo, ushushwaji wake kwenye maji na ufanyaji safari za majaribio.
“Zote ni hatua muhimu za utengenezaji meli ambazo zimetoa mafunzo kwa Watanzania walioshiriki kwenye mradi huu,” amesema.
Hamissi amesema Mv New Mwanza ni meli kubwa zaidi ukanda wa Afrika katika maji matamu, yenye kimo cha ghorofa nne sawa na urefu wa mita 92.6 (karibu na uwanja wa mpira), upana wa mita 17 na uzito wa tani 3, 500.
Ameeleza, Mv New Mwanza imejengwa na mkandarasi kutoka Kampuni ya Gas Entec Ship-Building Engineering na Kang Nam Corporation za nchini Korea kwa kushirikiana na Suma JKT, kwa gharama ya zaidi ya Sh120 bilioni.
Uwezo wa meli hiyo ni kubeba abiria 1, 200, magari 20 na tani 400 ya mizigo. Aidha, inatembea kwa kasi ya knoti 16, sawa na kilomita 30 kwa saa, jambo linaloifanya kufika Bukoba kwa muda wa saa sita hadi saba kutoka Mwanza; tofauti na zingine zinazotembea kati ya saa 8 hadi 10.
Hamissi amesema meli hiyo ina madaraja sita, moja ni la hadhi ya juu (VVIP) lenye uwezo wa kuhudumia abiria wawili, daraja la watu mashuhuri (VIP) litakalobeba abiria wanne, daraja la kwanza litakalohudumia abiria 60 na daraja la biashara llitakalobeba abiria 100.
Madaraja mengine ndani ya meli hiyo ni daraja la pili litakalotumiwa na abiria 200 na daraja la uchumi litakalobeba abiria 834.
Wakiwa safarini, abiria watakaosafiri kwa meli hiyo watapata huduma ya vyakula na vinywaji vya aina zote (baridi na vikali) katika mighahawa na baa zilizoko ndani ya chombo hicho kulingana na uwezo na madaraja yao.
Pia kutakuwa na burudani ya muziki wa dansi kutoka kwa wanamuziki kwa ajiri wa abiria, kwa lengo la kufanya safari yao kuwa rahisi na nyepesi.
Ndani ya meli hiyo, kuna lifti yenye uwezo wa kubeba watu 20 kwa wakati mmoja, kwa ajili ya abiria wenye mahitaji maalumu.
Kwa wenye matatizo na dharura za kiafya wawapo safarini, amesema watapata huduma za vipimo na tiba katika zahanati maalumu iliyoko ndani ya meli, huku wajawazito na wanaonyonyesha nao wakitengewa eneo maalumu wakati wa safari.
Wanaotaka kufunga ndoa na kufanya sherehe wakiwa safarini ndani ya meli, nao watapata fursa kutokana na meli hiyo kuwa na ukumbi maalumu ya sherehe na burudani.
Meli hiyo ina sifa za ziada, ikiwemo uwezo wa kuhimiri mawimbi ya bahari kuu katika kundi la tatu la mawimbi, japokuwa inafanya safari ziwani.
Meli ya Mv New Mwanza.
Hamissi amesema meli hiyo ina vifaa vya kisasa vya usalama vinavyoweza kutoa taarifa kwenye vituo vya uokozi vilivyopo Mwanza, Kisumu, Mombasa, Dar es Salaam na kwenye meli zilizopo Bahari Kuu pasipo nahodha au mtendaji yeyote kushiriki.
“Meli hii inawezesha upakiaji na kupakua mizigo kwa haraka kutokana na kuwepo kwa milango mikubwa miwili, pia gari la mizigo linaweza kuingia ndani ya meli likiwa tayari na mizigo yake,” amesema
Nakuongeza, “Mv New Mwanza haina tofauti na kijiji kinachoelea huku kikitembea na wakazi zaidi ya 1,000 kwa kuwa ndani ya meli kuna huduma ya maliwato, maji safi, viyoyozi, majiko makubwa, sehemu za kuhifadhi chakula kwa muda mrefu, huduma ya kwanza kwa wagonjwa, chumba cha wazazi na mfumo wa uhifadhi wa maji taka,” amesema.
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema gharama za usafiri wa abiria na usafirishaji wa mizigo itakuwa nzuri, shindani na ya kueleweka, ambayo hata hivyo hakuitaja.
“Ili kuhakikisha meli ya Mv New Mwanza inatoa huduma bora, wizara kupitia Tashico itahakikisha inakuwa na ratiba ya uhakika.
“Tuwahakikishieni abiria, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla hakutokuwa na ubadilishwaji wa ratiba ya meli hii ovyo ovyo, ratiba itakuwa ya kupangwa muda mrefu na tutasimamia ratiba hiyo,” amesema.
Akitaja vipaumbele wakati wa safari za meli hiyo, Profesa Mbarawa amesema cha kwanza ni usalama wa abiria na matengenezo ya meli yatakayofanyika kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha meli hiyo inadumu muda mrefu kama ilivyosanifiwa.
Amesema kipaumbele kingine ni usafi wa meli na afya ya abiria pamoja na kusimamia mafunzo ya wafanyakazi kwa kuhakikisha wana weledi, ujuzi na nidhamu ili waweze kutoa huduma bora.
Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso ameipongeza Serikali kwa kukamilisha mradi huo akisema Serikali haina deni Kanda ya Ziwa.
Amesema pamoja na Serikali kujenga daraja la Kigongo Busisi, uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwanza, Reli ya Kisasa (SGR) inayoendelea kujengwa kutoka Mwanza-Isaka, ameiomba kukamilisha kipande cha Dodoma -Tabora ili kuwasaidia wananchi kurahisisha shughuli za usafirishaji.
Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu amezitaka taasisi za Serikali, mashirika ya umma na serikali za mitaa kuacha matumizi ya mazoea na badala yake kuelekeza fedha hizo kwenye miradi ya maendeleo.
Akizungumza baada ya uzinduzi wa Mv New Mwanza, Dk Nchemba amesisitiza kufanyika kwa tathmini ya kina ya miradi yote iliyosainiwa mikataba lakini imesimama kutokana na wakandarasi kutopata fedha za awali.
Amesema baada ya tathmini hiyo, Wizara ya Fedha ipitie mafungu yote, kasoro ya vyombo vya ulinzi na usalama na yale yanayohudumia afya, mengine yote yarejeeni. Yale ambayo ni ziada hayawezi kuathiri, kateni tupate fedha tupeleke kwenye miradi ambayo imesimama,” amesema Dk Nchemba.
Amepiga marufuku taasisi za umma kutumia fedha za umma kwa ajili ya kununuliana kalenda, kadi, vinywaji, maua tabia ambayo amesema hufanyika kwenye sherehe za mwanzo na mwisho wa mwaka.
Vilevile, amezielekeza wizara zote kukata matumizi yasiyo ya lazima ambayo hayaathiri utekelezaji wa majukumu yake, ikiwemo ununuzi wa magari, ili fedha hizo zikamilishe miradi ya miundombinu, hususan ujenzi wa barabara.
Ameitaka Tamisemi kuwaandikia wakuu wa mikoa, mameya, wenyeviti wa halmashauri kuwawataka wahangaike mambo yanayowahusu wananchi.
“Anza hata kuangalia ile sheria ya halmashauri inayosema meya atachaguliwa, mwenyekiti wa halmashauri anachaguliwa, alafu wale makamu wanachaguliwa kila mwaka…tunatakiwa tuhangaike na mambo yanayohusu halmashauri na wananchi, tusifanye kazi ya kugawana vyeo miaka yote mitano,” amesema.