NMB yazindua bidhaa ya kisasa kwa wateja

Benki ya NMB imedhihirisha kiwango cha juu cha ubunifu, baada ya kuwa ya kwanza nchini kuzindua teknolojia mpya, ya kisasa na salama zaidi ya mfumo wa malipo ya NMB TAP, inayomuwezesha mteja kufanya malipo kupitia Pete, Bangili na Stika maalum.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo Ijumaa Januari 23, 2026, Mkurugenzi wa Uhusiano wa Wawekezaji, Uendelevu na Mawasiliano wa NMB, Innocent Yonazi, aliitaja NMB TAP kuwa ni ‘future of banking in Tanzania,’ inayokwenda kuiongezea nguvu mifumo yote ya malipo iliyoanzia katika pesa taslimu.

“Kwa muda mrefu tumekuwa tukifanya malipo kwa kadi na pesa taslimu, hiyo ndio ‘reality’ ya kibenki barani Afrika, hususani Tanzania. Sisi NMB lengo la kwenda na wateja wetu kwenye suluhisho zinazo kwenda na kasi ya maisha ya sasa (kidijitali) na sahihi zaidi za kibenki, tukaja na bunifu hii ya kwanza nchini.

“Mteja anahitaji kufanya malipo ya kibenki kwa haraka, unafuu, urahisi na usalama, vitu ambavyo vimo katika NMB TAP. Wanaume wengi walizoea kutembea na ‘wallet’ na wanawake wao mapochi na ‘hand bag’ za pesa, wateja wamekuwa watumwa wa mabenki, badala ya mabenki kuja na suluhisho za changamoto za kifedha.

“NMB kwa kushirikina na MasterCard tukaona haja ya kubadili hali hiyo, na kufanya mapinduzi makubwa juu ya mustakabali wa mifumo ya malipo nchini na kupitia NMB TAP, tunakwenda kumpa mteja huduma ambayo haijawahi kuwepo nchini Tanzania,” alisisitiza Yonazi.

Naye Mwakilishi Mkazi wa Master Card Kanda ya Afrika Mashariki, Shehryar Ali, aliipongeza NMB kwa bunifu zinazokidhi utatuzi wa changamoto za kibenki kwa wateja na kwamba wanajivunia ushirikiano baina ya benki hiyo na taasisi yao iliyobobea katika mifumo ya malipo ya kiteknolojia.