Sekeseke latikisa mrithi wa Jenista Peramiho, Takukuru yaingia

Dar es Salaam. Mchakato wa kura za maoni za ubunge wa Peramiho, Mkoa wa Ruvuma kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) umemalizika huku ukiacha vumbi la tuhuma za rushwa, vijembe, kuchafuana na lugha zisizofaa miongoni mwa wanachama na kuibua hofu ya mpasuko ndani ya jimbo hilo.

Makanda 27 akiwemo Victor Mhagama, mtoto wa Mbunge wa zamani wa Peramiho, Jenista Mhagama wamejitosa kuomba ridhaa ya CCM kupeperusha bendera katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Februari 26, 2026.

Uchaguzi huo unafanyika kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Jenista, aliyefariki dunia Desemba 11, 2025 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma baada ya kuugua maradhi ya moyo. Aliliongoza jimbo hilo kwa miaka 20 kuanzia mwaka 2005.

Kura za maoni zilizopoigwa Jumatano, Januari 21, 2026, umemalizika kwa mwanawe, Victor Mhagama kuwabwaga wenzake 26, wakiwemo viongozi wa CCM, waliowahi kuwa wabunge na watumishi wa umma.

Baada ya hatua hiyo, kinachosubiriwa ni vikao vya CCM wilaya, mkoa na Taifa kutoa mapendekezi na hatimaye uteuzi wa mwisho.

Hata hivyo, licha ya kura za maoni kuhitimishwa, kumeibuka malalamiko, tuhuma za rushwa na madai ya njama za kuuharibu mchakato huo, jambo linalodaiwa kuifanya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuingilia kati na kuwahoji baadhi ya viongozi wa CCM ngazi ya wilaya.

Mara baada ya matokeo kutangazwa usiku wa jana Jumatano na Msimamizi wa Uchaguzi wa CCM Wilaya ya Songea Vijijini, Juma Nambaila, kuliibuka mijadala mikali kwenye makundi mbalimbali ya WhatsApp juu ya uhalali wa matokeo hayo na madai ya uwepo wa kura feki.

Nambaila alimtangaza Victor kuwa mshindi kwa kupata kura 3,040 kati ya 8,577 halali zilizopigwa. Jumla ya kura zilizopigwa ni 9,167, zilizoharibika 590.

Aliwataja washindani wengine na kura zao kwenye mabano kuwa ni Getrude Haule (2,913), Dk Joseph Mhagama (943), Frank Matola (215), Dk Lazaro Kiomba (213), Dk Damas Mapunda (200) na Isabellah Mwampamba (131).

Wengine ni Joseph Masikitiko (126), Erasmo Mwingira (124), Allen Mhagama (114), Schoral Ngonyani (84), Lazaro Ndenji (68), Davis Ngonyani (62), Thea Ntara (57), Emil Ngaponda (51), Serafina Mkuwa (48) na Clemence Mwinuka (35).

Wengine ni Emelian Mbawala (24), Benjamin Kamtawa (23), Prosper Luambano (22), Dominic Mahundi (19), Fredrick Millinga (17), Sixmund Rungu (9), Rose Shawa (7), Rosemary Ngonyani (6) na Enoc Moyo (6).

Baadhi ya makada na wapembe wao kwenye makundi hayo, wamelalamika mchakato mzima wakidai haukuwa huru na haki.

 Walidai kuwa wamejumlisha kura zilizopigwa kutoka kwenye kata zao na kubaini kura za Victor, licha ya kuwashinda wengine, zimepunguzwa kwa makusudi ili kumuongezea mshindi wa pili, kitu ambacho walidai si sawa na kuwa matokeo hayo ni ya uongo.

Mwingine aliandika: “Kama walitaka kudanganya wajumbe na wanachama basi wangekuja na njia nyingine siyo hii.

“Dhuluma zilizofanywa na viongozi wilaya ya Songea Vijijini hazikubariki, Victor ni yatima hana mtu wa kumtetea, hivyo wamepanga kumdhulumu,” aliandika mmoja wa wachangiaji.

Mwingine alisisitiza: “Hii haikubariki kweli, makatibu mmeshiriki dhambi ya dhuluma ya kuiba kura za mtoto wa marehemu? Kijana wa watu amepata kura nyingi, mnatukatisha tamaa.”

Katika makundi hayo ambayo kuna viongozi mbalimbali wa chama na Serikali kuanzia mkoa hadi wilaya, hakuna ufafanuzi wala uliotolewa, lakini makada walitoa lugha za kejeli wakiiomba Takukuru kuingilia kati.

“Na makura yao fekiii yanazagaaa mitaani hukooo, kuna zile walizopeleka Kilagano ninazo hapa,” aliandika mmoja wa makada huku wengine wakituma meseji katika kituo kimoja cha redio kulalamikia mchakato huo kuwa haukuwa halali.

Mwingine aliadika: “Huu wizi sijui ni nini? Mnakotaka kupeleka Chama cha Mapinduzi ni kubaya, mnataka kudhurumu haki ya mtu bila sababu, uwongo huu haukubariki. Chama iki kina heshima kubwa sana mtu unakaa ofisini unapika matokeo bila aibu. Viongozi wa Songea Vijijini mjitafakari.”

Baada ya mijadala hiyo, Mwananchi lilipomtafuta Nambaila ambaye alisimamia uchaguzi huo, amesema ameona tuhuma hizo kupitia kwenye makundi ya WhatsApp na amepokea simu, ila matokeo ambayo wanadai yametangazwa kwenye kata yeye hayatambui,

Amewataka wanachama wayatambue matokeo yaliyotangazwa na msimamizi wa uchaguzi ambaye ni yeye na vikao vya chama ndio vitakavyoamua.

“Nimeona hayo malalamiko ya wanachama, hakuna kura feki ambazo zimekamatwa, watuonyeshe kama wana ushahidi. Mimi siwezi kutangaza matokeo ambayo si sahihi, hivyo wasubiri vikao vya kikanuni ndiyo vitateua mgombea,” amesema Nambaila.

Aidha, amewataka wanachama kutulia na kuviachia vikao vya kikanuni ngazi ya mkoa kuteua mgombea na mapendekezo yatawasilishwa ngazi ya Taifa kwenye kamati kuu  ambayo itafanya uteuzi wa mwisho wa mgombea mmoja atakayekwenda kuchuana na vyama vingine.

Mwananchi limezungumza na Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Ruvuma, Hamza Mwenda amefafanua kuhusu malalamiko yaliyopo na jinsi wanavyoyashughulikia.

Amesema katika kinyang’any’ro hicho kulichokuwa na watia nia 27 kati ya 28 waliochukua fomu, si ajabu kuwepo manung’uniko.

“Katika hawa watia nia 27 lazima utarajie manung’uniko na malalamiko yatakuwa mengi. Yapo manung’uniko yenye mashiko na yasiyo na mashiko, jukumu letu ni kupokea manung’uniko na malalamiko yote na kuyafanyia kazi. Yale yenye mashiko tunaendelea nayo kwa utaratibu wa kisheria na yasiyo na mashiko tunayaacha,” amesema Mwenda.

Amesema katika hatua za kupata ukweli wamekuwa wanafanya mahojiano na watu mbalimbali.

“Huko mitandaoni kila mmoja anasema lake. Kuna mtu anasema huko anahojiwa, amekamatwa na Takukuru lakini katika haya ni kuchafuana au nia nyingine. Sisi hatujamkamata Victor, isipokuwa tumemwita kufanya mazungumzo juu ya haya manung’uniko na tulipomaliza aliondoka.

“Na nikwambie tu, tumefanya nao (mahojiano) wengi na wengine wametuomba siku mbili tatu watakuja,” amesema.

Mwenda amekanusha pia madai ya kukamatwa kwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Songea Vijijini, Thomas Msolwa.

“Tulimwita naye kwa mahojiano, na sasa yuko mtaani huko atakuwa anakula zake bia. Kuna mtu anasema amekamatwa na fedha, hakuna ukweli wowote, bali hii yote ni huo mtiti wa watu 27, wanatengeneza wenyewe kwa wenyewe.”

Wakati hayo yakiendelea, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetoa mwaliko kwa taasisi na asasi za kiraia zenye nia ya kutoa elimu ya mpiga kura katika uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Peramiho na udiwani kwenye kata za Shiwinga, Jimbo la Mbozi kutoa maombi.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima kwenda kwa umma inaeleza maombi hayo yameanza kupokelewa kuanzia Januari 20 na mwisho itakwa Januari 29, 2026.

Miongoni mwa masharti kwa taasisi au asasi ni ziwe zimesajiliwa kisheria, imefanya kazi nchini kwa kipindi kisichopungua miezi sita tangu isajiliwe na katika utendaji wake iwe haijahusishwa na uchochezi au kuvuruga amani na iwe na uzoefu wa kutoa elimu ya mpiga kura.

Sambamba na hilo, Kailima pia amewaalika waangalizi wa ndani wa uchaguzi huo kutuma maombi kati ya Januari 20 na 26, 2026.