Davos. Mkutano wa Uchumi wa Dunia uliofanyika Davos nchini Uswisi kwa siku tano kuanzia Januari 19 hadi 23, 2026, na kuratibiwa na World Economic Forum, umeibua mjadala kutokana na hotuba ya Rais wa Marekani, Donald Trump, ambayo inatajwa kuvuka mipaka ya mijadala ya kiuchumi na kugeuka kuwa jukwaa la kutafakari mustakabali wa kisiasa wa Marekani.
Akiwa mbele ya viongozi wa serikali, wawekezaji wakubwa na wawakilishi wa taasisi za kimataifa, Trump alitumia fursa hiyo kueleza mtazamo wake kuhusu mwelekeo wa siasa za Marekani, changamoto zinazokabili demokrasia ya nchi hiyo na nafasi ya taifa hilo katika uchumi wa dunia.
Hotuba yake ilichanganya hoja za kiuchumi na kisiasa, ikisisitiza umuhimu wa sera za ndani katika kuimarisha ushindani wa Marekani katika soko la kimataifa. Aidha, alijenga hoja kwamba mustakabali wa uchumi wa dunia hauwezi kutenganishwa na mabadiliko ya kisiasa yanayoendelea Marekani, akitaja masuala ya uongozi, sera za biashara na mshikamano wa kijamii kama nguzo muhimu za maendeleo ya taifa hilo.
Kwa kugeuza jukwaa la Davos kuwa nafasi ya mjadala wa kisiasa, Trump alionyesha jinsi siasa na uchumi vinavyoungana kwa karibu, huku hotuba yake ikizua mjadala mpana kuhusu nafasi ya Marekani katika mfumo wa dunia unaobadilika kwa kasi.
Trump alipofika kwenye kipaza sauti, hakuanza kwa salamu ndefu wala maneno ya upole. Alianza moja kwa moja, sauti yake ikiwa nzito na kali.
“Wengi wenu mnasema kuhusu ushirikiano wa kimataifa,” alisema kwa kejeli nyepesi, “lakini ukweli ni kwamba baadhi ya nchi zimejenga uchumi wake kwa kutumia udhaifu wa wengine. Marekani imechoka kuwa mfadhili wa ndoto za watu wengine.”
Ukumbi ulitikiswa na mchanganyiko wa mshangao na kimya. Wachumi walitazamana, viongozi wa Ulaya waliinua nyuso zao, na waandishi wa habari waliinua kalamu zao kwa hamu.
“Mnazungumza juu ya biashara huria,” aliendelea, akiinamisha kichwa kidogo kana kwamba anazungumza na mtu asiyeonekana, “lakini biashara huria imekuwa biashara ya upande mmoja. Wengine wanapata faida, Marekani inalipa gharama.”
Alisimama kidogo, akavuta pumzi, kisha akaongeza kwa sauti iliyojaa ukali, “Hilo haliwezi kuendelea.”
Aligeuza macho yake upande wa viongozi wa Ulaya, akasema, “Ulaya imekuwa bingwa wa mihadhara ya maadili. Mnapenda kutufundisha kuhusu demokrasia, mazingira na haki za kijamii. Lakini mnapofanya biashara, mnasahau maadili yenu haraka sana.”
Kisha akageuka upande mwingine wa ukumbi, mahali walipokaa wawakilishi wa Asia. “Nchi fulani zimejenga uchumi wake kwa kuiba teknolojia, kudhibiti sarafu na kufunga masoko yao huku zikidai kufunguliwa kwa masoko ya wengine,” alisema kwa sauti ya kukaza. “Hiyo si ushindani wa haki. Huo ni udanganyifu.”
Trump alitabasamu kwa sekunde chache, tabasamu lililojaa kejeli. “Lakini msijali,” alisema, “Marekani sasa imeamka. Na inapokuwa imeamka, dunia nzima inasikia.”
Aliendelea kwa mtindo wa hadithi, akielezea jinsi Marekani ilivyobeba jukumu la usalama wa kimataifa, mikataba ya biashara na misaada ya kifedha. Lakini kila sentensi ilikuwa na mkuki wa maneno.
“Wengine wanapenda kusema Marekani ni mkoloni wa kiuchumi,” alisema, akiinua mkono kidogo, “lakini ukweli ni tofauti. Marekani imekuwa kama benki ya dunia; kila mtu anakopa, wachache wanarudisha.”
“Na sasa,” aliongeza kwa sauti ya chini lakini nzito, “tunabadilisha mchezo.”
Katika safu ya mbele, viongozi wa taasisi za kimataifa walikaa kimya. Wengine walionekana kama watu wanaotazama dhoruba ikikaribia, bila kujua kama itapita au itaharibu kila kitu.
Trump aliinua kidole chake, akasema, “Dunia imezoea kuona Marekani ikitafuta makubaliano kwa gharama yoyote. Lakini zama hizo zimekwisha. Kuanzia sasa, makubaliano yoyote lazima yawe ya haki, au hayatawepo kabisa.”
Alipiga meza kidogo kwa kiganja cha mkono, sauti ikasikika hadi kona za ukumbi.
Katika dakika chache, jukwaa la uchumi lilikuwa limegeuka kuwa jukwaa la siasa za nguvu. World Economic Forum, ambalo kwa kawaida lilijivunia lugha ya diplomasia, lilionekana kama uwanja wa mapambano ya maneno.
Trump hakusimama hapo. Aligeuza mwelekeo wa hotuba yake kwa nchi zinazoendelea.
“Baadhi ya mataifa yanaamini kwamba maendeleo yanapatikana kwa kulaumu wengine,” alisema, akiinua macho yake juu kidogo, “lakini hakuna taifa litakalofanikiwa kwa kulaumu Marekani au Ulaya. Mafanikio yanahitaji nidhamu, uwajibikaji na ujasiri.”
Alimalizia kwa sentensi iliyotikisa ukumbi mzima. “Dunia inaweza kuchagua njia mbili,” alisema kwa sauti tulivu lakini kali, “njia ya ushirikiano wa kweli au njia ya ushindani wa wazi. Marekani iko tayari kwa zote mbili. Swali ni: Ninyi mko tayari?”
Baada ya hapo, makofi yalipigwa si kwa shangwe, bali kwa mshangao, hofu na kutambua kwamba siku hiyo, Davos haikuwa tena jukwaa la nadharia za uchumi tu.
Ilikuwa uwanja wa vita vya maneno, mahali ambapo nguvu ya kisiasa ilikuwa imevunja mipaka ya diplomasia.
Trump alishuka kutoka jukwaani kwa hatua za kujiamini, akiacha nyuma ukumbi uliojaa maswali, hasira zilizofichwa na hofu ya mustakabali wa mfumo wa uchumi wa dunia.