JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa watatu ambao ni Mseveni Menat, Mkazi wa Uyole, Fred Lulandala, Mkazi wa Mapelele na Joseph Ngelenge, Mkazi wa Uyole Jijini Mbeya kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya Bhangi yenye uzito wa Kilo 168.
Watuhumiwa walikamatwa Januari 21, 2026 baada ya kuingia katika Stendi Kuu ya Mabasi Jijini Mbeya wakiwa kwenye Bajaji yenye namba za usajili MC 850 EWN aina ya TVS Kings wakiwa na dawa hizo za kulevya zikiwa kwenye mabegi nane wakitaka kuzisafirisha kuelekea Jijini Arusha.
Watuhumiwa wameeleza kuingiza nchini dawa hizo kutoka nchini jirani na walitaka kuzisafirisha kwa njia ya Basi kuelekea Jijini Arusha. Upelelezi unakamilishwa ili hatua zaidi za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
WATIWA MBARONI KWA WIZI WA PIKIPIKI YA MAGURUDUMU MATATU.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa watatu ambao ni Ajiri Mwapelele, Mkazi wa Iganzo, Evils Shabani, Mkazi wa Igodima Jijini Mbeya na Victor Paulo, Mkazi wa Igurusi Wilaya ya Mbarali kwa tuhuma ya wizi wa Pikipiki ya Magurudumu matatu maarufu Guta yenye namba za usajili MC 495 FFY aina ya Sinoray.
Watuhumiwa waliiba Pikipiki hiyo Januari 21, 2026 saa 9 usiku huko katika Kijiji cha Uhenga, Wilayani Wanging’ombe, Mkoa wa Njombe kwa mtu aitwaye Haruna Shomari Mahagile, Mkazi wa Kijiji cha Uhenga na kisha kuisafirisha Pikipiki hiyo hadi Mkoani Mbeya kwa ajili ya kuiuza.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilianza ufuatiliaji na Januari 21, 2026 saa 5 asubuhi huko Iganzo, Jijini Mbeya lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao wakiwa na mali hiyo ya wizi. Upelelezi unakamilishwa ili hatua zaidi za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa baadhi ya wananchi ambao bado wanajihusisha na uingizaji, usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya kuacha mara moja kwani ni kinyume cha sheria n ani hatari kwa afya zao na za wengine hususani vijana. Pia, wakumbuke ukikamatwa na utakapopatikana na hatia adhabu yake ni kifungo na usafiri uliotumika kusafirishia utataifishwa kwa mujibu wa sheria. Aidha, linatoa wito kwa baadhi ya watu wenye tamaa ya kujipatia mali kwa njia zisizo halali kuacha mara moja na badala yake watafute shughuli halali ili kujipatia kipato halali kwani kwa mujibu wa sheria ni uhalifu na haulipi na hauna nafasi kwenye jamii. Lakini uhalifu wowote ule kijamii ni aibu kwako na una dhalilisha familia.
Imetolewa na:
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.