AFCON: Mwisho wa ubaya aibu

Dar es Salaam. Wabongo ni wepesi sana kujifunza, lakini wazito mno kuyaishi yale waliyojifunza. Nawazungumzia wabongo wa anga zote wakiwemo wanafunzi, waumini, wafanyakazi kwa wakulima. We mwenyewe fikiria ulipokuwa Shule ya Msingi, kila asubuhi ulikuwa unakwenda shuleni ukibeba kuni na dumu la maji.

Kuni za kupikia, maji ya nini? Ya kumwagilia bustani yako ya mboga pale shuleni. Ulijituma sana hadi muda wa kuvuna ulipofika, bustani yako ikawa ya mfano kwa wanafunzi wenzako.

Kwa bahati mbaya (kama unavyosema) hukufaulu kutoboa kwenye mtihani wa kuhitimu. Na mbaya zaidi wazazi hawakuweza kukutafutia shule ya kulipia kutokana na uwezo wao mdogo. Ndugu na jamaa nao wasingeweza maana nao walikuwa na watoto kama wewe walioshindwa kuwasomesha. 

Sasa umeamua kutulia kijiweni na vijana wenzio wenye akili mbovu kama wewe, mnakula vikali mkitambiana jinsi mnavyofanya bidii ya kuzungusha madubwi. 

Kwani kule shuleni si ulijifunza, tena ukalima bustani? Je, hukuuliza mazao yenu yaliishia wapi? Jibu lake hata mbumbumbu analo. Uliona jinsi mwalimu wako wa darasa na wa kilimo walivyokuwa na hekaheka baada ya mazao yako kuiva.

Basi wenzako waliyaingiza sokoni wakavuta mkwanja kimyakimya. Maana yake badala ya kulemaa kijiweni na kuvuta ndumu, shika jembe ukalime, utakachovuna utakiingiza sokoni na kitakulipa. Wateja wapo, maana hamna bingwa wa njaa hapa duniani.

Lawama hizi si ndogo. Ukute wewe ulisoma shule za Msondo kama mimi, halafu ukampeleka mwanao shule za Akademia. Mtoto akasahau kila kitu kasoro “Sir”, “Madam” na “Maid”. Hakuna cha babu wala mkaza mjomba hapo.
 

Mwisho wa siku anahitimu na kurudi nyumbani akiwa na begi la vyeti, lakini hajui hata kupika chai. Atajuaje na wakati Maid aliajiriwa kwa kazi hiyo? Huoni kuwa huyu mtoto hata angelipata kazi, angeishia kubembea tu kwenye kiti cha magurudumu?

Inasikitisha sana. Juzi kati tumepokea kijiti cha uenyeji wa mashindano ya AFCON kutoka kwa Morocco. Tumeyaona ya uwanjani lakini sina uhakika kama tuliyaona yale ya mtaani. Wachambuzi wa mambo wanatuambia kila fursa iliyochomoza kwenye mashindano hayo ilikamatwa na wenyeji. 

Hii ni kutokana na jinsi wenzetu walivyofundwa wakafundika. Tangu wakiwa wadogo, walishajua mikakati ya kujiendesha wenyewe kama wadudu.

Sasa ni zamu yetu. Sijajua kijiti hicho kitawasaidiaje vijana wetu, wala sitegemei bodaboda anayepeleka hesabu kwa tajiri kila jioni apate koneksheni ya kusafirisha kichwa cha mwarabu? Sio rahisi.

Nasema hivi kwa sababu matajiri wetu nao wamo kwenye mbio za wajasiriamali. Bongo mtu ana kiwanda lakini naye ni mmachinga. Ila kwa sababu tayari ana mtaji, inakuwa simulizi ya “mwenye kisu kikali…”.

Moroko tulijifunza mengi, kubwa likiwa “mgeni njoo mwenyeji ashinde”. Lakini wanenaji walinena: “Usishindane na mtu mwovu”. Sisi tumeendelea mara nyingi sana licha ya kuifikia hatua ile kwa mara ya kwanza. Bado tuliuthibitishia ulimwengu kuwa inawezekana kubato na mabingwa, na kumkazia mkubwa nyumbani kwake hadi akakufanyia figisu. 

Wao na ubaya wao, hata kama wangechukua ubingwa wangeishia pale. Sisi bado tunasonga kuwatafuta wenzake, nao watufanyie tantalila.

Ingelikuwa tumeenda kwenye mashindano yanayojumuisha sayari zote, tungeliwaacha mbali sana. Fikiria mtanange ungepigwa nchini “Chini Usipite” katika sayari ya “Juu Pita”, wangempata wapi yule refarii Mkongo awabebe.

 Kaniudhi sana yule jamaa… Afu kafanana na mwalimu wangu wa hisabati shule ya msingi. Huyu mwalimu alifanya nidharaulike kwa wenzangu; nilipopata swali aliniwekea alama ya kuuliza, nilipokosa akaniwekea mkasi!

Lakini nimeamini mwisho wa ubaya aibu. Nakumbuka nilimpeleka mwenzangu kwa rafiki kuangalia video. Akaninyima rimoti afu umeme ukakatika. Ndio yule refa; kwanza alitunyima sisi tuta la wazi, halafu akawakosesha Senegali bao kisha akawagonga na penalti.

 Lakini penati wakakosa na bao wakapigwa. Yaani Wasenegali walinikosha mpaka kumoyo, maana tangu sisi tulipofanyiwa mazingaombwe nilikuwa nawatazama wenyeji kwa jicho baya sana.

Wala nisiwe mnafiki, kocha wa Senegali aliposema “Sasa imetosha” nilimuunga mkono. Ila mimi ningefungwa jela maana nisingemwacha bila kumtoa angalau meno mawili… Akh!!! Shetani keshakuja jirani yangu.
 

Michezo si ugomvi, na asiyekubali kushindwa si mshindani. Nisingemtwanga kichwa cha meno, bali nisingelimwombea mema. Na ajiangalie sana maana atakutana na watu wenye hasira wamtupie Jini Astakafiru ashindwe hata kuomba maji.

Sasa hii ndio namna ya kulipa kisasi: Mtu akikupiga na matusi wewe mpige na ukimya, ataona sura nzito kuliko kiroba cha maharagwe. Na ile ndio inaleta tafsiri sahihi ya usemi wa “Mshahara wa dhambi”, maana sijui refarii baada ya fyongo zile kama atapata shavu la Kombe la Dunia yule! Na kama atakwenda, basi atarudi bila meno. 

Kuna akina Simon James kama wote kule. Yaani ukawaharibie starehe zao waliokufundisha wewe mpira?

Sisi tuyachukue mazuri yote tuliyoyaona kama maandalizi, fursa na koneksheni. Ingawaje kwa sasa ni ngumu sana kijana wa Kitanzania kulielewa hilo, lakini madamu limetufika basi hatuna budi kujifunza.