Ecua, Doumbia kuibukia Sauzi | Mwanaspoti

WAKATI wowote kuanzia sasa, mastaa wawili wa Yanga watakwenda kuungana na aliyekuwa mshambuliaji wa kikosi hicho, Andy Boyeli, kule Afrika Kusini ambako watapelekwa kwa mkopo ili kupisha hesabu za usajili pale Jangwani.

Mastaa hao ni Celestine Ecua ambaye alisajiliwa dirisha kubwa msimu huu, huku akipewa mkataba wa miaka mitatu ya kukitumikia kikosi hicho akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast.

Wa pili ni kiungo kutoka Ivory Coast, Mohamed Doumbia, ambaye pia alitua Yanga dirisha kubwa msimu huu. Hawa ni miongoni mwa mastaa ambao watatolewa kwa mkopo.

Ecua na Doumbia wanaweza kuungana na Andy Boyeli tena baada ya Yanga kuwa kwenye mazungumzo ya kuwapeleka kwa mkopo Sekhukhune ya Afrika Kusini, ambako walimtoa Mkongomani huyo kwa mkopo wa miezi sita.

Mwanaspoti linafahamu kwamba, timu zote mbili zilikuwa kwenye hatua nzuri ya kukamilisha dili hilo la mkopo wa miezi sita kwa kila mchezaji.

Taarifa za ndani ya Yanga zimelidokeza gazeti hili kuwa, “tutawapeleka huko kwa mkopo, tupo kwenye hatua za mwisho. Wale ni marafiki zetu kwa muda sasa, unaona tunawapeleka ligi yenye ushindani zaidi na tutakuwa tunawafuatilia.

“Bado hawajaondoka nchini, lakini wakati wowote watakwenda Afrika Kusini. Tulishakubaliana kila kitu kuhusu maslahi yao wakiwa huko, tumebakiza makubaliano ya klabu kwa klabu tu.

“Viwango vyao wakiwa huko ndivyo vitatusaidia kufanya uamuzi kama tutaendelea nao au tutaamua vinginevyo. Bado tunaona vipaji vyao, lakini tunakwenda kuangalia kama watapata muda wa kutosha wa kucheza.”

Doumbia amechezea mechi saba akiwa hajafunga bao hata moja, huku akifikisha jumla ya dakika 396. Huku kwa mshambuliaji Ecua akiwa na rekodi ya kufunga bao moja.

Kabla ya mastaa hao hawajatolewa, Yanga ilikuwa na nyota 14 wa kigeni wakizidi wawili wanaotakiwa kikanuni.

Lakini baada ya kuwatoa, sasa wamebaki 12 ambao ni Djigui Diarra (Mali), Kouassi Attohoula Yao (Ivory Coast), Chadrack Boka (DR Congo), Frank Assinki (Ghana), Pacôme Zouzoua (Ivory Coast), Lassine Kouma (Chad), Duke Abuya (Kenya) na Moussa Balla Conte (Guinea).

Wachezaji wengine ni Laurindo Dilson Maria Aurelio ‘Depu’ (Angola), Maxi Mpia Nzengeli (DR Congo), Prince Dube (Zimbabwe) na Allan Okello (Uganda).