Gardiel Michael kutua Dodoma Jiji

BEKI wa Dodoma Jiji, Miraji Abdallah ‘Zambo’ yupo kwenye hatua za mwisho kutua Singida Black Stars, huku pia nyota wa kikosi hicho, Gadiel Michael akipigiwa chapuo la kurithi nafasi yake.

Chanzo kutoka ndani ya Singida kimeliambia Mwanaspoti kuwa Zambo aliyejiunga na Dodoma Jiji akitokea Coastal Union baada ya dili lake la kwenda Simba kuota mbawa yupo katika mazungumzo  kujiunga na kikosi hicho katika dirisha hili litakalofungwa Januari 30, 2026.

“Ni mchezaji tunayemuhitaji ili kuongeza nguvu eneo la upande wa kushoto, ingawa katika majadiliano yaliyopo ni kumtoa Gadiel Michael ili kwenda kwao, bado hatujafikia uamuzi wa mwisho ila ni kweli dili hilo lipo,” kilisema chanzo hicho.

Katika dirisha kubwa la usajili lililopita, Zambo alikuwa karibu kujiunga na Simba ingawa aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids baadaye alipendekeza asajiliwe Anthony Mligo wa Namungo, ndipo nyota huyo akajiunga na Dodoma Jiji.

Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua kipaumbele cha kwanza cha uongozi wa Dodoma Jiji ni kumpata Gadiel Michael, ambaye nafasi kwa nyota huyo kuendelea kubakia katika dirisha hili dogo ni ndogo kutokana na ushindani mkubwa wa nafasi uliopo.

Gadiel aliyejiunga na Singida Januari 2025, baada ya kuachana na Chippa United ya Afrika Kusini, inaelezwa hayupo katika mipango ya kikosi hicho kwa sasa, jambo linalotoa nafasi kwa Dodoma Jiji kutaka kumsajili kutokana na uzoefu pia wa nyota huyo.

Beki huyo wa kushoto amewahi kuchezea Azam ya vijana hadi ya wakubwa, Yanga, Simba na Fountain Gate zote za Tanzania kisha alitimkia Cape Town Spurs ya Afrika Kusini ambayo alijiunga  Januari 2024 kisha kuondoka Juni 2024.