Huu hapa ujumbe wa Lissu kwa Mzee Mtei

Arusha. Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amemwelezea mzee Edwin Mtei kama kiongozi wa kisiasa na mtendaji wa Serikali jasiri aliyekuwa na uthubutu wa kuukataa uchawa.

Hotuba hiyo iligusiwa leo kwenye mazishi ya Mtei na Naibu Katibu mkuu wa Chadema (Bara), Aman Golugwa kwamba wamepokea salamu za ujumbe wenye kurasa tisa kutoka gerezani kwa Mwenyekiti wa chama hicho Tundu Lissu na itasambazwa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.

Katika salamu zake hizo alizozipa kichwa cha habari “Hotuba ya Heshima kwa Edwin Mtei” ambazo amezituma kwa waombolezaji akiwa mahabusu kwa zaidi ya siku 280 katika gereza la Ukonga Jijini Dar es Salaam, Lissu alisema maisha yake yalijaa busara tele.

Lissu ambaye anashikiliwa mahabusu kutokana na kesi ya uhaini inayomkabili, alisema ni kutokana na kutofautiana kwake na Rais wa awamu ya kwanza, Mwalimu Nyerere wakati yeye akiwa waziri wa Fedha, aliamua kujiuzulu.

“Mzee Mtei hakunyamaza mara alipogundua kwamba sera za kiuchumi za Serikali yake, sera alizoshiriki kuzitunga na kuzisimamia hazitekelezeki tena. Mzee Mtei alimkabili Mwalimu na kumweleza ukweli wake,” amesema Lissu na kuongeza;

“Alimkabili na kumweleza kwamba sera za kiuchumi za Azimio la Arusha zilikuwa zimeshindikana kutekelezwa; akamshauri Mwalimu kubadili msimamo wake ili kwenda sambamba na mahitaji ya nyakati na hali halisi ya uchumi wa kimataifa.

 “Mfumo wa Kikatiba na kiutawala wa aina hii sio tu ulimgeuza Rais kuwa Mungu mtu, bali pia ulitengeneza mazingira mazuri ya ‘uchawa’ miongoni mwa viongozi na watendaji wa Serikali na chama cha TANU na baadaye CCM,”alisema Lissu.

“Baadhi yenu mtakumbuka salamu rasmi za kisiasa za miaka hiyo “‘zidumu fikra za Mwenyekiti wa CCM!’ Mzee Mtei alikuwa na ujasiri wa kumweleza Mwalimu, kwa heshima zote, kwamba fikra zake za kiuchumi zilikuwa zimefeli,”ameeleza Lissu.

“Kwa ujasiri huo huo, aliwajibika kwa kujiuzulu nafasi pale Mwalimu alipomkatalia ushauri wake huo. Alikuwa na uadilifu wa kuona kwamba haikuwa sahihi kwake kuendelea kutumikia nchi wakati ametofautiana na kiongozi mkuu wa Serikali.

“Leo hii, kwa jinsi ambavyo ‘uchawa’ umekuwa ni donda ndugu na umekithiri ngazi zote za utumishi wa umma na hata katika sekta binafsi, tunaweza kupima kiwango cha juu cha ujasiri wa Mzee Mtei na uzalendo wake kwa nchi yetu.

“Itoshe tu kusema kwamba yale yote ambayo Mzee Mtei aliyapendekeza kwa Mwalimu na yakakataliwa, yalikubaliwa na kuanza kutekelezwa miaka miwili tu baada ya Mzee Mtei kulazimika kujiuzulu nafasi yake ya Waziri wa Fedha.

“Kwa maneno mengine, ukweli wa msimamo wake ulithibitishwa kwa vitendo, licha ya yeye mwenyewe kulazimika kuwa nje ya Serikali. Kwangu mimi, hii ndio thamani na maana kubwa ya maisha marefu ya Mzee Edwin Mtei,”alisisitiza.

Lissu alisema miaka 94 ya Mtei duniani aliitumia kuwapa Watanzania thamani kubwa na ni maisha yaliyojaa  busara na yalikuwa na maana kubwa kwa taifa.