KOCHA wa Fountain Gate, Mohamed Laizer amesema mchezo unaofuata utakuwa mgumu zaidi, kwani wapinzani wao wametokea kuchezea kichapo kikali dhidi ya Yanga.
Akizungumza na Mwanaspoti, Laizer alisema ugumu wa mchezo huo utakuwa kwenye maeneo mawili ambayo yote yanatokana na wapinzani wao, akitaja hasira ambayo wanayo baada ya kufungwa mabao mengi na Yanga kwenye mchezo wa juzi, hivyo hawatataka kurudia makosa.
Lakini, pili Fountain Gate itakuwa ugenini, jambo ambalo ni faida kubwa kwa wapinzani kwani ni ngumu kupoteza.
“Siwezi kusema Mashujaa watakuwa wepesi kwetu. Ukweli uliojificha ni kwamba hii huenda ikawa mechi ngumu kwa sababu ya hasira kali ambayo naamini wanayo. Unajua ukitoka kupoteza mchezo, (mchezo) unaofuata lazima uwe makini. Hivyo nguvu zote za Mashujaa zitakuwa kwenye pointi tatu muhimu,” alisema.
Aliongeza kuwa, “kikosi chetu kiko vyema kuhakikisha kinaikabili Mashujaa na kwa njia hii ya mazoezi na utimamu wa akili kwa wachezaji, naamini tutabeba alama tatu ugenini.”
Fountain Gate itakutana na Mashujaa wiki ijayo, Januari 29, ikiwa imecheza mechi 11 ikifikisha pointi hizohizo, ikishinda mechi tatu, sare mbili na kupoteza sita.