Na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania(TTB) Ephraim Mafuru amesema kuzinduliwa kwa meli mpya kubwa na ya kisasa ya MV New Mwanza kunakwenda kufungua fursa katika sekta ya utalii ambapo sasa watalii watazunguka nchi za Afrika Mashariki kwa kutumia usafiri wa meli hiyo ambayo ni rahisi na nafuu.
Mafuru ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akizungumza baada ya Tanzania kuandika historia kubwa katika uwekezaji ya miundombinu ya usafiri, usafirishaji na utalii katika Bara la Afrika.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewekeza Sh.bilioni 120 katika meli hii. Watanzania wenzangu na Waafrika kwa ujumla Bodi ya Utalii Tanzania tunatoa mwito tutumie meli hii kuendeleza biashara zetu zinazozunguka katika Afrika Mashariki kwasababu Ziwa Victoria ndio ziwa kubwa kuliko maziwa yote katika Afrika
“Inauwezo wa kubeba mizigo mingi na kusafirisha abiria lakini pia kuleta watalii. Kwawale mlioko sekta ya utalii mtakubaliana nami ya kwamba watalii wanaozunguka katika Afrika Mashariki kutoka Kenya tunawageni 240,000 , na kutoka Uganda ni wageni kama 60,000 na wengi wanatumia barabara ,wengi wanatumia safari za anga
“Leo hii Serikali ya Awamu ya Sita imeidhihirishia dunia ya kwamba watalii sasa wanaweza kuzunguka Afrika Mashariki kwa kutumia usafiri rahisi na nafuu kupitia meli hii ya Mv New Mwanza,”amesema Mafuru kuhusu kuzinduliwa kwa meli hiyo sambamba na fursa ambazo zitapatikana katika kukuza utalii.
Awali wakati anazungumza meli hiyo Mafuru amesema ndani ya wiki mbili zilizopita yameshuhudiwa makubwa katika historia ya nchi yetu na leo katika Jiji la Mwanza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Mwigulu Nchemba ameongoza viongozi mbalimbali wa Serikali na Chama na wawekezaji walioko ndani ya Tanzania kushuhudia uzinduzi wa meli hiyo kubwa ya MV New Mwanza
“Kwamara ya kwanza katika bara la Afrika yaani vyombo vinavyotumika katika maji baridi katika maziwa Tanzania inakuwa nchi ya kwanza kwa ujenzi na uzinduzi wa meli kubwa MV New Mwanza ambayo leo imezinduliwa jijini Mwanza ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 1200 kwa wakati mmoja,magari madogo 20 na magari makubwa matatu
“Sasa unaweza kujiuliza tani 400 za mizigo zina uwezo wa kubebwa na meli hii, kwa Watanzania wenzangu ambao tunaweza kupiga picha tani 400 maana yake nini ? Ukichukua yale magari makubwa semitraila tani 400 ni magari 13.
Hebu piga hesabu msururu wa yale magari ,urefu wa hii meli ni karibu uwanja mmoja wa mpira kwani uwanja wa mmoja wa mpira una mita 92.”




