MWENYEKITI TUME YA UCHAGUZI AFUNGUA RASMI MAFUNZO YA WATENDAJI WA UCHAGUZI MKOANI IRINGA

NA DENIS MLOWE, IRINGA 

MWENYEKITI wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele, leo amefungua rasmi mafunzo ya siku tatu kwa watendaji wa uchaguzi ngazi ya mkoa, jimbo na kata yanayofanyika mkoani Iringa, akisisitiza uadilifu, weledi na uzingatiaji wa sheria katika mchakato wa uchaguzi.

Akizungumza mbele ya waratibu wa uchaguzi wa mikoa, wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi, maafisa uchaguzi, wahasibu, maafisa ununuzi na wanahabari, Mhe. Mwambegele alianza kwa kuwatakia washiriki heri ya mwaka mpya 2026 na kuwapongeza kwa kuteuliwa kutekeleza jukumu muhimu la kusimamia uchaguzi mdogo wa Ubunge Jimbo la Peramiho na Udiwani Kata ya Shiwinga.

Mwenyekiti huyo alieleza kuwa uteuzi wa watendaji hao umezingatia matakwa ya Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2024, ikiwemo sifa za uadilifu, weledi na uzoefu katika masuala ya uchaguzi. “Ni muhimu kuheshimu viapo vyenu na kutekeleza majukumu kwa kuzingatia Katiba, sheria za uchaguzi, kanuni na maelekezo ya Tume,” alisisitiza

Katika hotuba yake, Mhe. Mwambegele aliwakumbusha washiriki kuwa uchaguzi ni mchakato wenye hatua nyingi za kisheria zinazotakiwa kufuatwa kwa umakini ili kuepusha malalamiko na vurugu. Alionya dhidi ya kufanya kazi kwa mazoea kwa sababu  kila uchaguzi unatofautiana na mwingine.

Aidha, aliwataka watendaji kuwa karibu na vyama vya siasa vyenye usajili kamili na wadau wengine ili kuongeza uwazi, uaminifu na urahisi wa utekelezaji wa majukumu.

Katika mafunzo hayo, Mwenyekiti alibainisha masuala mahimu ambayo washiriki wanapaswa kuyazingatia, ikiwemo:

Kufanya utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini mahitaji na changamoto za miundombinu.

Kuhakikisha waajiriwa wa vituo vya kura ni wenye weledi na si watu waliopendekezwa kwa upendeleo, kuhakiki vifaa vya uchaguzi na kuhakikisha kila kituo kinafikiwa mapema.

Kuwapatia vyama vya siasa orodha ya vituo vya kupigia kura kwa maandalizi ya mawakala na kuhakikisha vituo vyote vinafunguliwa saa 1:00 asubuhi siku ya uchaguzi na kufanya mawasiliano ya karibu na Tume pale panapohitajika ushauri.

Mhe. Mwambegele pia aliwasihi washiriki kujifunza kwa makini, kushirikishana uzoefu na kuacha tabia ya kufanya kazi kwa mazoea, akisema maarifa na umakini ni msingi wa uchaguzi wenye ufanisi.

Baada ya kutoa maelekezo na maonyo muhimu, Mwenyekiti huyo alitangaza rasmi kufunguliwa kwa mafunzo ya siku tatu yatakayofanyika kuanzia Januari 24 hadi 26, 2026.

“Ni matarajio ya Tume kwamba kila mmoja atatoka hapa akiwa na ujuzi wa kutosha wa kusimamia uchaguzi huu mdogo kwa ufanisi,” alisema kabla ya kumaliza hotuba yake na kuwashukuru washiriki wote.Baadhi ya wasimamizi waliopata mafunzo walisema kuwa mafunzo hayo yawasaidia kusimamia vyema chaguzi ndogo za marudio.

Mmoja wa Wasimamizi hao kutoka jimbo la Peramiho,  Salum Kateule alisema kuwa mafunzo yaliyoandaliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Peramiho, mkoa wa Ruvuma. Uchaguzi huu umeitishwa kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge, Mheshimiwa Jenista Mhagama.

 Leo tumekutana kwa ajili ya mafunzo ya watendaji ngazi ya mkoa, watendaji ngazi ya jimbo na ngazi ya kata. Mafunzo haya yamefunguliwa na Mheshimiwa Mwenyekiti, ambaye ametukumbusha kusimamia vyema majukumu yetu ya usimamizi wa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Peramiho kulingana na sheria, katiba na kanuni za uchaguzi za mwaka 2016.

Wito wangu kwa wananchi wa Jimbo la Peramiho ni kwamba, kwanza, wajitokeze kuchukua fomu za kugombea. Kwa wale watakaoteuliwa, waendelee kuwasilisha sera na mipango ya vyama vyao kwa ajili ya kujinadi na kupata fursa ya kuteuliwa na wananchi.

Pili, nawaomba wananchi wa Jimbo la Peramiho kujitokeza kwa wingi wakati wa kampeni za uchaguzi, kuwasikiliza wagombea wote na kuwapa fursa sawa za kuwasikiliza.

Kateule aliwasihi wananchi wajitokeze siku ya kupiga kura ili kumchagua kiongozi ambaye wanamuona anafaa kuwatumikia na kuuwakilisha vyema Jimbo la Peramiho.

Naye Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la la mbozi, Dan Tweve, amesema maandalizi ya uchaguzi mdogo katika Kata ya Shiwinga yanaendelea vizuri kufuatia kifo cha diwani aliyeshinda kabla ya kuapishwa. 

Tweve amesema jukumu la wasimamizi ni kuhakikisha maandalizi ya msingi yanafanyika kwa ufanisi, ikiwemo kuwawezesha wagombea kuchukua fomu, kufanya kampeni kwa amani na hatimaye kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki na utulivu. 

Aidha, amesisitiza kuwa wapiga kura wote, wakiwemo watu wenye ulemavu, watapatiwa huduma na msaada unaohitajika ili washiriki bila vikwazo. Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika tarehe 26 Februari.