WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika ibada ya kumuaga aliyekuwa Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mzee Edwin Mtei, akimtaja kuwa kiongozi mahiri, mzalendo na nguzo muhimu katika historia ya uchumi na demokrasia ya Tanzania.
Akizungumza katika ibada hiyo ya mazishi iliyofanyika nyumbani kwa marehemu Tengeru, Dkt. Nchemba alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua mchango mkubwa wa marehemu kwa Taifa na Serikali mara zote itaenzi mchango wake mkubwa katika uchumi na demokrasia nchini.
Waziri Mkuu alisema Mzee Mtei alikuwa miongoni mwa Watanzania wachache waliobahatika kuhudumu katika nyadhifa zote kuu za sekta ya fedha, ikiwemo kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Waziri wa Fedha na mwakilishi wa Tanzania katika taasisi za fedha za kimataifa, mchango uliompa heshima ya kipekee kitaifa na kimataifa.
Alisema katika maisha yake ya utumishi wa umma, marehemu alitambulika kwa kusimamia misingi ya uadilifu, uaminifu, uzalendo, bidii na kumcha Mungu na kwamba mchango wake uliweka msingi imara wa taasisi za kifedha na nidhamu ya uchumi wa Taifa.
Dkt. Nchemba alibainisha kuwa Mzee Mtei pia alikuwa miongoni mwa waasisi wa demokrasia ya vyama vingi nchini, akiwa mwanzilishi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hatua iliyochangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha mfumo wa kisiasa na uhuru wa mawazo nchini.
Katika kuenzi mchango wa marehemu kwa vitendo, Waziri Mkuu alitoa maelekezo mahsusi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa hatua hizo ni sehemu ya kudumisha misingi ya maendeleo, haki na uzalendo aliyoyaishi marehemu.
Kuhusu miundombinu ya barabara, Waziri Mkuu alielekeza ukamilishwaji wa taratibu za manunuzi na kuanza mara moja kwa ujenzi wa barabara ya njia nne katika kipande cha Tengeru hadi Usa River, akieleza kuwa mkandarasi anatakiwa kuingia eneo la kazi bila kuchelewa.
Aidha, kwa kipande cha Usa River hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) chenye urefu wa kilomita 28, Waziri Mkuu alisema usanifu wa mradi ulikuwa umefikia takribani asilimia 80, na akaelekeza Wizara ya Ujenzi kwa kushirikiana na TANROADS kukamilisha haraka usanifu uliobaki na kutangaza zabuni mara moja, akisisitiza kuwa fedha za utekelezaji wa mradi huo tayari zipo.
Katika hatua nyingine, aliagiza ukamilishwaji wa barabara na madaraja katika maeneo korofi kati ya Kilimanjaro na Arusha ifikapo Februari 20, 2026, akielekeza Wizara ya Ujenzi na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha kuhakikisha barabara hiyo inafunguliwa na kuanza kutumika kwa lengo la kuondoa adha kwa wananchi.
Kuhusu mgogoro wa ardhi katika eneo la Mringa Estate, Waziri Mkuu alielekeza marekebisho yafanyike ndani ya mwezi mmoja kwa mujibu wa makubaliano ya awali, ili wananchi waliopaswa kunufaika na eneo hilo wapate haki yao. Aliagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kamishna wa Ardhi pamoja na maafisa ardhi husika kusimamia kikamilifu utekelezaji wa agizo hilo, hususan katika eneo lililonunuliwa na kampuni ya Bajuta Enterprises.
Waziri Mkuu alisisitiza kuwa utekelezaji wa maelekezo hayo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kuendeleza maendeleo jumuishi, kusimamia haki za wananchi na kudumisha heshima ya viongozi waliolitumikia Taifa kwa uadilifu na uzalendo akiwemo Mzee wetu Mtei.



