NISHATI SAFI YA RAFIKI BRIQUETTES IWAFIKIE WATANZANIA WOTE

:::::::::

Watanzania wametakiwa kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutumia nishati safi ya kupikia (mkaa mbadala wa Rafiki briquettes) unaozalishwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO). 

Rai hiyo imetolewa leo Januari 24, 2026 na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Meja Jenerali Mstaafu Mhe. Balozi Jacob Kingu akiwa ameambatana na Wajumbe wa REB na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) walipotembelea kiwanda cha Nishati safi ya Rafiki Briquettes kinachomilikiwa na STAMICO kilichopo Kisarawe Mkoani Pwani.

Balozi Kingu amewataka STAMICO kuongeza kasi ya uzalishaji wa mkaa wa Rafiki briquettes ili watanzani wote nchini waweze kutumia nishati safi ya kupikia na salama. 

“Hii ajenda ya matumizi ya nishati safi ambayo kinara wake ni Rais wa Awamu ya Sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan inalenga kumkomboa Mwanamke ili aachane na matumizi ya nishati isiyo safi na salama. Tunahamasisha na kutekeleza maono haya ya Kiongozi wetu”, amesema Balozi Kingu

Ameongeza kuwa, ushirikiano wa REA na STAMICO katika Kutekeleza Miradi ya Nishati Safi ya Kupikia umelenga kufikia asilimia 80% ifikapo mwaka 2034 (Mkakati 2024-2034).

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mha. Hassan Saidy ameongeza kuwa Wakala unaendelea kushirikiana na Wadau mbalimbali ili kuhakikisha Mkakati wa Nishati safi ya kupikia unatimiza malengo yaliyowekwa, ikiwa ni pamoja na kuongeza upatikanaji na usambazaji wa mkaa mbadala.

Naye, Sophia Mgonja Mjumbe wa Bodi ya REB amewapongeza STAMICO kwa namna wanavyotengeneza mkaa mbadala katika kiwanda hicho cha Nishati safi cha Rafiki briquettes na kuwataka wadau mbalimbali kutumia nishati safi hiyo inayozalishwa ili kuifanya ajenda ya nishati safi kuwa endelevu na kuwafikia watanzania wengi. 

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa STAMICO Mha. Baraka Manyama amesema kuwa mradi wa Rafiki Briquettes umesaidia katika utunzaji wa mazingira (umeokoa majanga ya kimazingira), pia umekua chanzo kikubwa cha ajira kwa makundi mbalimbali wakiwemo wanawake, vijana na wadau mbalimbali.

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) wamesaini mkataba wa kujenga kiwanda kipya cha kuzalisha nishati mbadala (Mkaa mbadala wa Rafiki Briquettes) mkoani Geita ambapo mkataba huo una thamani ya shilingi bilioni 4.5 na ujenzi unaemdelea.








Mwisho