Pamba Jiji yakomaa dirisha dogo

LICHA ya kuachana na wachezaji wanne kwenye dirisha dogo, Pamba Jiji imesisitiza kuwa haitasajili kipindi hiki kwani ina kikosi kitakachotosheleza mahitaji ya msimu uliosalia.

Pamba Jiji imeachana na kipa Arijifu Ali Amour, beki Abdallah Heri Sebo na winga Salehe Masoud huku ikimtoa kwa mkopo mshambuliaji Abdallah Iddi ‘Pina’ kwenda Muembe Makumbi ya Zanzibar.

Timu  hiyo inakamata nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikivuna alama 16 nyuma ya vinara Yanga wenye alama 17 na JKT Tanzania pointi 17. Pamba imecheza mechi tisa na kushinda nne, sare nne na kupoteza moja, huku ikifunga mabao 11 na kuruhusu sita.

Ofisa Habari wa Pamba Jiji, Moses William amesema uamuzi wa kutosajili unatokana na ripoti ya benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Francis Baraza ambaye ameridhika na nyota alionao, huku ugumu wa kupata mchezaji wa maana dirisha dogo ukichangia pia uamuzi wa timu hiyo kuamua kutulia dirisha dogo.

“Mpaka sasa hatujaingiza mchezaji yeyote na kama itatokea ataingia labda mchezaji mmoja kwa sababu sisi hatukuwa na changamoto kubwa. Benchi la ufundi hawana uhitaji wa wachezaji wapya,” alisema William na kuongeza;

“Kimsingi tulitumia vizuri dirisha kubwa na hatuna sababu ya kutumia nguvu dirisha dogo. Hakuna timu kwenye dirisha dogo ambayo ina mchezaji muhimu kwenye timu yake ikamuachia, siyo rahisi kumpata mchezaji ambaye nyie mnamtaka kwenye dirisha hili, ndiyo maana tumefanya hivyo.”

Akizungumzia vigezo vilivyotumika kuwaacha wachezaji hao, William alisema ni kutokana na mapendekezo ya benchi la ufundi yaliyozingatia takwimu zao katika mechi tisa za kwanza, muda waliocheza na mchango wao ndani ya kikosi hicho.

“Sababu za kuwatoa ni muda ambao wamecheza kwenye michezo yetu tisa ya ligi na mchango wao, kimsingi ni mambo ya muda wa kucheza. Benchi la ufundi wamefanya tathmini wakaona kuna haja ya kufanya hivyo,” alisema William na kuongeza;

“Lakini kingine ni makubaliano binafsi ya mkataba kwa hao wachezaji ambao tumeachana nao, kwahiyo sababu ni mbili tu, mambo binafsi ya kimkataba na mapendekezo ya benchi la ufundi kulingana na mchango wa hao wachezaji kikosini.”