Rungwe. Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya imetumia zaidi ya Sh249 milioni kuboresha miundombinu ya zahanati katika Shule ya Msingi Katumba II Mchanganyiko.
Shule hiyo inayohudumia wanafunzi wenye mahitaji maalumu, imepewa fedha hizo kuweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa huduma bora za afya kwa kundi hilo.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa mwarobaini wa changamoto za kiafya zinazowakabili wanafunzi wenye ulemavu wa viungo vya aina mbalimbali, ambao huhitaji huduma za karibu na rafiki kulingana na hali zao.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi, Januari 24, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Renatus Mchau, amesema fedha hizo zimetolewa na Serikali Kuu kutokana na umaalumu wa shule hiyo na mahitaji ya wanafunzi wanaoisoma.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Mbarali, Renatus Mchau akizungumza na Mwananchi ofisini kwake. Picha na Hawa Mathias
Amesema pamoja na ukarabati wa zahanati, Serikali pia hutoa zaidi ya Sh14 milioni kila mwezi kwa ajili ya kugharamia mahitaji mbalimbali ya shule hiyo ikiwemo chakula cha wanafunzi.
“Serikali kila mwezi inatoa Sh14 milioni kusaidia mahitaji ya shule. Hata hivyo, bado kuna changamoto ya baadhi ya wazazi kutorejea kuwachukua watoto wao wakati wa likizo, jambo linaloongeza mzigo kwa walimu na uongozi wa shule,” amesema Mchau.
Ameeleza kuwa maboresho ya zahanati hiyo yanaambatana na ujenzi wa jengo la mapokezi, nyumba ya mtumishi na vyoo, ili kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya wanafunzi na jamii inayozunguka shule hiyo.
Mchau ameishukuru Serikali Kuu kwa kuendelea “kuitupia jicho” Shule ya Katumba II Mchanganyiko yenye zaidi ya wanafunzi 250 wenye mahitaji maalum, akisema uwekezaji huo utapunguza usumbufu kwa walimu na wanafunzi endapo kutatokea dharura za kiafya.
“Pamoja na idadi kubwa ya wanafunzi, halmashauri inatenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu, ikiwemo ujenzi wa bweni lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 80, kwa lengo la kuongeza wigo wa huduma,” amesema.
Kwa upande wake, Kaimu Ofisa Elimu Awali na Msingi Wilaya ya Rungwe, Kotasi Mbwilo, amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya Shule ya Katumba II na shule nyingine, ili kuwawezesha watoto wenye mahitaji maalum kutimiza ndoto zao za kupata elimu bora.
Amesema halmashauri ina jumla ya shule za msingi 160, zikiwemo 10 binafsi, huku akibainisha kuwa katika kipindi cha miaka miwili shule tatu mpya zimefunguliwa na vyumba vya madarasa kuongezeka kutoka 1,157 hadi 1,195.
Mbwilo ameongeza kuwa halmashauri imepokea Sh659 milioni kupitia mradi wa BOOST kwa ajili ya ujenzi wa shule mbili mpya katika maeneo ya Ndaga (Kata ya Ndanto) na Kisa (Kata ya Kisondelo).
Mkazi wa Msasani wilayani Rungwe, Ester John, ameipongeza Serikali kwa maboresho makubwa katika sekta ya elimu, akisema miundombinu rafiki imeongeza hamasa ya wazazi kuwapeleka watoto shule.
“Tunaona miundombinu sekta ya elimu hususani shikizi na mahitaji maalum zikijengwa kwa viwango vya hali ya juu jambo ambalo kama wazazi sada tunaona umuhimu wa elimu kwa watoto,”amesema.