WANASIMBA wanataka kuiona timu yao inafuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kama kawaida yake ilivyofanya misimu saba iliyopita kuanzia 2018, lakini sasa mlima ni mrefu kutokana na matokeo iliyopata katika mechi tatu za kundi D.
Kupoteza mechi tatu mfululizo za makundi katika michuano ya CAF, imekuwa ni matokeo mabaya zaidi kwa Simba kuyapata tangu ilipoanza kushiriki hatua hiyo kuanza mwaka 2003.
Simba iliyocheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita 2024-2025, mambo yamekuwa magumu msimu huu hatua ya makundi baada ya leo Januari 23, 2026 kupoteza mechi ya tatu hatua ya makundi ikifungwa bao 1-0 na Esperance.
Kabla ya hapo, Simba ilifungwa 1-0 nyumbani dhidi ya Petro Atletico, kisha ikapoteza kwa mabao 2-1 ugenini mbele ya Stade Malien.
Katika mechi hii iliyochezwa nchini Tunisia, bao la Jack Diarra dakika ya 21 akitumia vizuri pasi ya Mohamed Ben Hamida, lilifanya Simba kukubali kichapo hicho ikiwa ugenini na kufifisha matumaini ya kufuzu robo fainali kwani inaburuza mkia wa kundi D ikiwa haina pointi, huku Esperance ikifikisha tano.
Mashabiki wa Simba walionekana kulikatia tamaa chama lao kutokana na matokeo hayo hali inayofanya mechi ya marudiano wikiendi ijayo itakayochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kama vile ni ya kwenda kukamilisha ratiba.
Hata hivyo, Simba inaweza kushangaza kama itaichapa Esperance katika mechi ya marudiano na zingine zilizobaki, huku wapinzani wake wengine wakawa na matokeo mabaya mechi zilizobaki.
Hii ni mara ya kwanza Simba inapoteza mechi tatu mfululizo za hatua ya makundi, ikiipiku rekodi ya msimu wa 2022–2023 katika Ligi ya Mabingwa ilipopoteza mechi mbili za kwanza, lakini ikatoboa.
Mbali na kupoteza mechi tatu, Simba imefunga bao moja pekee, huku yenyewe ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne na kufanya kuwa na mlima mrefu wa kupanda ili kupambania nafasi ya kufuzu robo fainali.
Timu hiyo yenye rekodi ya kucheza robo fainali saba za CAF katika misimu minane iliyopita kuanzia 2018 hadi 2025, ili irudie rekodi hiyo, italazimika kushinda mechi tatu zilizobaki dhidi ya Esperance (nyumbani), Petro Atletico (ugenini) na Stade Malien (nyumbani), huku pia ikiomba matokeo mabaya kwa wapinzani wake wawili kati ya watatu ilionao kwenye kundi hilo ili kumaliza nafasi mbili za juu.
Simba imekuwa na rekodi nzuri ya kufuzu robo fainali kila inapotinga makundi tangu mwaka 2018, lakini safari hii inasubiriwa miujiza kutokea ili kufanikisha jambo hilo kutokana na msimamo wa kundi D ulivyo sasa.
Kabla ya Petro Atletico na Stade Malien zenye pointi nne kila moja hazijacheza kesho Jumapili, kundi hilo linaongozwa na Esperance yenye pointi nne, huku Simba haina kitu ikiwa mkiani.
Kocha Steve Barker katika mechi ya jana, alianza na nyota wawili wapya waliosajiliwa dirisha dogo ambao ni Djibril Kassali na Nickson Kibabage, hata hivyo.
Clatous Chama ambaye naye amesajiliwa dirisha dogo sambamba na Libase Gueye, waliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Morice Abraham na Jonathan Sowah wakati kipindi cha pili kinaanza.
Hii ni mechi ya tatu mfululizo Barker anatoka uwanjani bila ya ushindi, akianza na nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi alipofungwa 1-0 na Azam, kisha sare ya bao 1-1 katika ligi dhidi ya Mtibwa Sugar, kabla ya jana kufungwa 1-0 na Esperance kwenye Ligi ya Mabingwa.
Simba iliyoanza mechi kwa taratibu, ilionekana kushindwa kasi ya wapinzani wao waliokuwa na moto muda mwingi kiasi cha dakika tisini kuongoza katika mashambulizi Esperance wakipiga mashuti manne yaliyolenga lango kati ya sita, wakati Simba ikiwa na moja pekee kati ya matano.
Hata hivyo, Simba ilitawala mechi kwa asilimia 53, dhidi ya 47 za Esperance, hata hivyo haikuwa na maana kwani imeshindwa kuondoka na hata pointi wala bao.