Sintofahamu zuio la shughuli za Chadema

Dar es Salaam. Kuzuiliwa kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kufanya baadhi ya shughuli zake katika mikoa ya Mbeya, Rukwa na Njombe siku ya maadhimisho ya miaka 33 ya chama hicho, kumeibua sintofahamu na malumbano baina ya viongozi wa chama na Jeshi la Polisi.

Katika maadhimisho hayo, yaliyofanyika Januari 21, 2026, Jeshi la Polisi katika mikoa hiyo lilizuia shughuli zilizopangwa kufanywa na wanachama katika maeneo hayo na kuwashikilia baadhi ya viongozi wao.

Ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu ya kuanzishwa kwa chama hicho kilichopata usajili wa kudumu Januari 21, 1993, makada wa chama hicho waliandaa shughuli za upandaji miti, kufanya usafi huku wengine wakishusha bendera nusu mlingoti kuomboleza kifo cha mwasisi wa chama hicho, Edwin Mtei aliyefariki Januari 19, 2006 na maziko yake kufanyika leo.

Wanachama wa Chadema walikumbana na changamoto ikiwemo kukamatwa na Polisi wengine wakidai kunyimwa fursa ya kupanda miti au kufanya usafi kwenye maeneo ya umma, jambo ambalo ni wajibu wao kama wananchi.

Mkoani Njombe, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Njombe Mjini, Reginald Danda alisema siku hiyo walipanga kukutana kutafakari kuhusu chama chao tangu kuanzishwa kwake, pamoja na kupanda miti na kufanya usafi shuleni na hospitalini, hata hivyo hawakupewa kibali.

Huko Rukwa, Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) Mkoa wa Rukwa, Aida Khenani alisema Nkasi Kaskazini waliamua kuadhimisha miaka 33 ya Chadema kwa kupanda miti na walikuwa wameandaa miche 1,600, hata hivyo walizuiliwa kufanya shughuli hiyo.

Mkoani Mbeya, Chadema kilipanga kufanya uzinduzi wa tawi la chama hicho katika Kata ya Inyala pamoja na kushiriki bonanza la kumbukizi ya mwasisi wa chama hicho kama njia ya kuenzi mchango wake.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema Mbeya vijijini Getrude Nyangesere alisema wakiwa kwenye shughuli hiyo, Polisi wakiongozwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mbeya Vijijini, walifika na kuwatawanya wananchi waliokuwa eneo la stendi ya Inyala.

Mbali na hayo, amesema katika tukio hilo, Polisi waliwakamata Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Masaga Kaloli, Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Mbeya, Elisha Chonya pamoja na wanachama wengine kadhaa.

Katika tukio hilo, amesema bendera ya chama ambayo waliipandisha nusu mlingoti kama ishara ya kuomboleza kifo cha Mtei, ilishushwa na Jeshi la Polisi.

Kati ya matukio hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga pekee ndiye alitoa taarifa kwa umma akithibitisha jeshi hilo kuwashikilia viongozi wa Chadema, Masaga na Chonya huku akieleza sababu za hatua hiyo kuwa kufanya mkusanyiko usio halali.

Alifafanua kwamba chama hicho kimezuiliwa na Mahakama kufanya shughuli zozote za kisiasa.

“Ikumbukwe kuwa Chadema kimezuiliwa na Mahakama kufanya shughuli zozote za kisiasa, upelelezi unakamilishwa ili hatua zaidi za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa,” alisema Kamanda huyo katika taarifa yake. Makamanda wa Njombe na Rukwa hawakupatikana kuzungumzia hatua zilizochukuliwa kwenye maeneo yao

Mvutano wa kisheria kuhusu zuio

Wakati Kuzaga alitaja zuio la mahakama, mvutano wa kisheria umeibuka kuhusu hatima ya zuio hilo, baada ya kauli kinzani kutolewa kati ya uongozi wa Chadema na mawakili wa wadai kwenye kesi ya mgawanyo wa rasilimali iliyopo mahakamani.

Mvutano huo umekuja baada ya Mwanasheria Mkuu wa chama Chadema, Dk Rugemeleza Nshala kutoa taarifa kwa umma akieleza kuwa zuio hilo lilikuwa na muda maalumu wa miezi sita na kuwa tayari limeshakwisha.

Taarifa ya Dk Nshala imeungwa mkono na Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche, kuwa kufuatia kukoma kwa zuio hilo, chama kiko tayari kuendelea na shughuli zake za kisiasa na siku si nyingi kitatoa utaratibu wa kufanya mikutano.

Hata hivyo, taarifa ya Dk Nshala na kauli ya Heche zimepingwa na kiongozi wa jopo la mawakili wa wadai, Wakili Shaban Marijani, akisema waliotoa taarifa hiyo wanajichanganya katika tafsiri ya amri ya mahakama.

Marijani amesema zuio dhidi ya Chadema ni mpaka kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa mali inayokikabili chama hicho itakapoamuliwa.

Mvutano huo unatokana na amri ya Mahakama Kuu Dar es Salaam iliyotolewa Juni 10, 2025 kufuatia mambo ya wadai, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Said Issa Mohamed na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu dhidi ya Bodi ya Wadhamini Waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.

Januari 23, 2026 Dk Rugemeleza Nshala alieleza katika taarifa kwa umma kuwa zuio hilo lilikuwa la miezi sita tu, hivyo limeshakwisha.

Dk Nshala amesema kukoma huko ni kutokana na Kanuni ya 3 ya Amri ya 37 ya Sheria ya Mwenendo wa Madai, inayosema:

 “Mahakama inaweza kutoa amri ya zuio kwa mujibu wa kanuni ya 1 au kanuni ya 2 na amri hiyo itakuwa na maisha kwa kipindi kilichotajwa na Mahakama, lakini kisichozidi miezi sita; Na kwamba amri ya zuio inaweza kutolewa kwanza kwa miezi sita na inaweza kuongezwa zaidi lakini nyongeza hiyo ikiwa ni pamoja na zuio la kwanza lisizidi jumla ya mwaka mmoja.

Alifafanua kuwa nyongeza hiyo ya muda wa zuio haikuwa kuombwa na wadai hao, hivyo kisheria limekoma.