Dar es Salaam. Wakati uhakika wa mawasiliano ya anga ukitajwa kuchochea ndege za kimataifa kupita Tanzania kuongeza mapato, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imesema matumizi ya teknolojia za kisasa yanachangia uhakika huo pamoja na kuepusha ajali angani.
Teknolojia hizo ikiwemo ile ya mifumo mipya ya mawasiliano kati ya rubani na waongozaji wa ndege kupitia redio za mawasiliano (VHF-Digital radio), reda, pamoja na teknolojia za kutoa taarifa za hali ya hewa kila baada ya nusu saa.
Hayo yamebainishwa jana Januari 23, 2026 na Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Salim Msangi ambaye amesema teknolojia katika mawasiliano ya anga ndio usalama wa anga, hivyo haikwepeki.
Ameyasema hayo alipofungua mkutano wa 45 wa mwaka wa Chama cha Waongoza Ndege Nchini (TATCA), uliofanyika leo Januari 23, 2026 jijini Dar es Salaam.
“Tumejizatiti uhakika wa mawasiliano ya anga ya kisasa kwa kuwa ndio usalama wa anga. Ndege zisipowasiliana angani na waongoza ndege, uwezekani wa kupata ajali ni mkubwa. Sisi kwenye hili tumejizatiti vizuri hatuna ajali inayotokana na kukosa mawasiliano,” amesema.
Mkurugenzi huyo mkuu amesema kufungwa kwa mifumo hiyo kunafanya ndege ziweze kuwasiliana kama inavyotakiwa katika ubora wa kimataifa.
Akizungumzia changamoto, amesema teknolojia zinabadilika mara kwa mara na pia ni gharama. Pia, wataalamu wa sekta ya uongozaji ndege nichangamoto kuwapata ukizingatia na mafunzo yao ni gharama.
Akieleza zaidi amesema, chama hicho malengo yake ni pamoja na kuimarisha usalama, ufanisi, na taratibu za urubani wa anga kitaifa na kimataifa.
Kadhalika, kutoa msaada na ushauri katika uendelezaji wa mifumo salama na yenye mpangilio ya uongozi wa ndege, na kukuza viwango vya juu vya maarifa na taaluma miongoni mwa waongoza ndege.
“Hii ni fursa muhimu kuwahakikishia kuwa tutaendelea kushirikiana na taasisi yenu ili kufikia malengo yote matatu niliyoyataja, na hivyo kuongeza usalama na uhakika wa safari za anga ndani ya anga la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema.
Rais wa TATCA, Merkiory Ndaboya akizungumza kuhusu mkutano huo uliowakutanisha na wadau kutoka nje ya Tanzania amesema wanatumia akili unde (AI) kuwasaidia katika kutelekeza majukumu.
“Pia, ipo mitambo ya kisasa, teknolojia ya reda ambayo inajua ndege iko umbali gani ipo na spidi gani. Teknolojia ya rubani kupata taarifa, mitambo ya kupeleka taarifa kwnye kompyuta kuhusu uelekeo na spidi ya upepo,” amesema.
Kwa upande wake, muongoza ndege kutoka Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Hellen Mosha amesema watatumia mkutano huo kujadili mambo mbalimbali yanayowakabili katika sekta yao.
“Tunahakikisha tunakwenda sambamba na teknolojia,” amesema Hellen.