Dar es Salaam. Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 imeanza kufanya kazi zake faragha, ikiwazuia waandishi wa habari kuingia katika ukumbi ambao waathirika wa matukio hayo wanawasilisha ushahidi wao.
Rais Samia Suluhu Hassan aliunda Tume hiyo kufuatia maandamano yaliyotawaliwa na vurugu siku ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, ikiwa ni njia ya kutafuta chanzo cha vurugu hizo kabla ya kuelekea kwenye maridhiano ya kitaifa.
Tangu imeanza kazi, vyombo vya habari vimekuwa vikitumia nafasi hiyo kuuhabarisha umma kuhusu kazi inayofanywa na Tume hiyo sambamba na kueleza walichozungumza mashahidi wakati wakiwasilisha ushahidi wao mbele ya Tume.
Jana, Januari 23, 2026, Mwananchi lilishiriki mkutano wa Tume hiyo na mashahidi uliofanyika Magomeni, Dar es Salaam liliandika liliandika simulizi mbalimbali za waathirika wa matukio hayo.
Leo, Januari 24, 2026, Tume ilikuwa Wilaya ya Ubungo, ambapo baadhi ya wananchi wamejitokeza kutoa ushahidi wa mambo yaliyowasibu au kuyashuhudia siku ya uchaguzi, na wao kujikuta wakiathirika kwa namna tofauti.
Hata hivyo, tofauti na ilivyokuwa awali, Tume imetangaza kwamba waandishi wa habari hawataruhusiwa kuingia kwenye ukumbi ambao waathirika wangewasilisha ushahidi wao.
Mjumbe wa Tume hiyo aliyeongoza wajumbe wengine kwenye shughuli hiyo, Jaji mstaafu, Profesa Ibrahim Juma ametoa tangazo hilo wakati akifungua kikao hicho huku akieleza kwamba uamuzi huo umechukuliwa ili kulinda faragha ya mashahidi.
“Tutakapoanza kupokea ushahidi, waandishi wa habari wote mtupishe ili tuwape faragha wazungumzaji na kulinda ushahidi wao. Tukishamaliza, mtarudi tena na mtaweza kuuliza maswali ili kupata mnachotaka,” amesema.
Profesa Juma ameongeza kuwa baadhi ya waliotoa ushahidi wao wamelalamika kwamba taarifa zao binafsi zimesambaa kwenye vyombo vya habari na mitandaoni baada ya kuzitoa mbele ya Tume hiyo.
“Tumepokea malamakiko kutoka kwa baadhi ya waathirika waliotoa maoni siku zilizopita, kwamba taarifa wanazotoa nyingine ni taarifa zao binafsi, wasingependa zitangazwe hadharani,” amesema mjumbe huyo.
Profesa Juma ameongeza kuwa waliolalamila wamesema wamekuwa wakitafutwa na vyombo vya habari na mashirika makubwa ya habari kwa ajili ya kufanyiwa mahojiano kutokana na visa walivyoeleza mbele ya Tume.
Kufuatia hatua hiyo, Profesa Juma ametoa maelekezo kuwa kwa vikao vinavyoendelea waandishi wa habari hawataruhusiwa kuingia ndani ya ukumbi wakati Tume ikipokea malalamiko, ili kuwapa faragha watoa ushahidi wa matukio waliyoshuhudia wakati na baada ya uchaguzi.
Hatua hiyo mpya ya Tume imekuja wakati Tume hiyo ikiwa imefanya vikao katika mikoa mbalimbali nchini na maeneo kadhaa ya jiji la Dar es Salaam yakiwemo Temeke na Kinondoni, Mwanza, Mara na Geita ambako waandishi wa habari walishiriki kikamilifu na kuripoti yaliyojiri kwenye vikao hivyo, zikiwemo simulizi za waathirika.
Katika kikao hicho cha Wilaya ya Ubungo ambayo inajumuisha maeneo ya Kimara ambako taarifa za awali za vurugu za uchaguzi huo zilianza kutolewa, watu wengi wamejitokeza huku baadhi yao wakionekana kuwa na ulemavu, wakiwemo waliovunjika miguu na wenye majeraha makubwa.
Wakati waandishi wa habari wakitoka eneo hilo, shahidi wa kwanza, mwanamke ambaye jina lake halikupatikana mara moja, alisikika akiangua kilio akitoa simulizi ya alichokumbana nacho katika matukio aliyokutana nayo.
Akizungumzia uamuzi huo wa Tume, mwandishi wa gazeti la Raia Mwema, Selemani Msuya amesema uamzi wa Tume una athari chanya na hasi.
Kuhusu athari chanya, amesema tangu Tume hiyo imeanza kufanya vikao na matukio mengi yanayoendelea vikaoni kurushwa kwenye vyombo vya habari, yamekuwa yakiibua hisia mbaya katika jamii.
“Baashi ya vyombo vya habari vimekuwa vikirusha mubashara au kusambaza taarifa za waathirika ambazo kwa watazamaji zinaibua hisia mbaya, ukiona video ukatokwa machozi, kwa eneo hili kuzuia urushaji wa moja kwa moja wa taarifa ni jambo jema,” amesema.
Kwa upande wa mtazamo hasi, Msuya ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (Jowuta), amesema kuzuia waandishi kuingia kwenye vikao kunaathiri ubora wa habari ambazo wangezitoa kwa jamii.
“Kuwataka waandishi wasubiri taarifa ya mtu wa Tume, inawanyima kupata habari ambayo kila mwandishi angeitaka, pia, inaondoa uwazi wa jamii kusikia yanayosemwa na watu huko, ili hata ripoti ya Tume ikitoka watu waiamini,” amesema.