Tume yawaonya wasimamizi wa uchaguzi kuelekea chaguzi ndogo

Iringa. Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji Jacobs Mwambegele amewataka wasimamizi wa uchaguzi nchini kuacha kufanya kazi kwa mazoea, badala yake wazingatie sheria, kanuni na maelekezo ya Tume.

Jaji Mwambegele ametoa wito huo Januari 24, 2026 katika ukumbi wa mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kuanzia leo Januari 24 hadi 26, 2026 kwa waratibu wa uchaguzi wa mikoa, wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi ngazi ya jimbo na kata, maofisa uchaguzi, maofisa ununuzi pamoja na wahasibu.

Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wasimamizi wa uchaguzi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa kuzingatia sheria.

Mafunzo hayo yanahusishwa na maandalizi ya uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Peramiho pamoja na uchaguzi wa diwani wa kata ya Shiwinga mkoani Songwe.

Uchaguzi huo umeitishwa kufuatia vifo vya aliyekuwa Mbunge wa Peramiho, Jenista Muhagama na diwani wa Kata ya Shiwinga, Lusekelo Mwalukomo.

Waratibu wa uchaguzi wa mikoa, wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi ngazi ya jimbo na kata, maafisa uchaguzi, maofisa ununuzi pamoja na wahasibu wakifuatilia mafunzo maalum yanayoendelea katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.



Jaji Mwambegele amesema utekelezaji wa majukumu ya uchaguzi unapaswa kuongozwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na sheria zote za uchaguzi ili kuhakikisha chaguzi zinaendeshwa kwa haki na uaminifu.

Jaji Mwambegele ametoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya wasimamizi wa uchaguzi yaliyofanyika mkoani Iringa, yakihusisha waratibu wa uchaguzi wa mikoa, wasimamizi wa uchaguzi pamoja na wasaidizi wao.

Mafunzo hayo yanahusisha pia maofisa uchaguzi, maofisa ununuzi na wahasibu wanaohusika moja kwa moja katika maandalizi na uendeshaji wa chaguzi.

Amesema kila uchaguzi una mazingira yake na changamoto zake, hivyo wasimamizi wanapaswa kuwa makini na kuepuka kurudia mifumo ya nyuma bila kuzingatia hali halisi ya wakati husika.

Kwa mujibu wa Jaji Mwambegele, Tume inatarajia kuona viwango vya juu vya uadilifu vinazingatiwa katika hatua zote za mchakato wa uchaguzi.

“Ni wajibu wa wasimamizi wa uchaguzi kuheshimu viapo mlivyoapa na kutekeleza majukumu yenu bila upendeleo wowote wa kisiasa,” amesema Jaji Mwambegele.

Amewapongeza wajumbe wa Tume pamoja na waratibu wa uchaguzi wa mikoa ya Songwe na Ruvuma kwa uteuzi wao, akisema umezingatia misingi ya weledi, haki na uwazi.

Pia, Jaji Mwambegele amesema uteuzi huo umefanywa kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.

Jaji Mwambegele amewataka wasimamizi wa uchaguzi kushirikiana kwa karibu na vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili katika masuala muhimu ya uchaguzi.

“Na ushirikishwaji wa wadau wa uchaguzi ni muhimu katika kujenga imani na kupunguza migogoro inayoweza kujitokeza wakati wa mchakato wa uchaguzi,” amesema Jaji Mwambegele.

Kwa upande wake, Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Ruvuma, Athumani Kateula amewahamasisha wananchi wenye sifa katika Jimbo la Peramiho kujitokeza kugombea nafasi ya ubunge.

“Ushiriki wa wananchi katika kuchukua fomu, kampeni na kupiga kura ni muhimu katika kujenga demokrasia imara,” amesema Kateula.

Kabla ya kuanza rasmi kwa mafunzo hayo, wasimamizi wa uchaguzi waliapishwa kujitoa katika uanachama wa vyama vya siasa, hatua iliyolenga kuimarisha misingi ya uwazi, haki na kutokuegemea upande wowote katika uendeshaji wa chaguzi nchini.