Ukatili wa kijinsia Tanga waendelea kuongezeka, Tamwa yapaza Sauti

Tanga. Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) kimesema vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto vinaendelea kuongezeka katika Mkoa wa Tanga na Kanda ya Kaskazini, licha ya jitihada zinazochukuliwa na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo kukabiliana na tatizo hilo.

Kauli hiyo imetolewa leo wakati wa mdahalo wa wadau uliofanyika katika Jiji la Tanga, uliowakutanisha wanahabari, walimu, wanafunzi, viongozi wa jamii na wadau wa maendeleo, kwa lengo la kujadili hali ya ukatili wa kijinsia pamoja na nafasi ya vyombo vya habari katika kuelimisha jamii na kuchochea mabadiliko ya mitazamo na tabia.

Akisoma taarifa ya Tamwa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa chama hicho, Dk Rose Reuben, Msaidizi wa Mkurugenzi wa Tamwa, Sylivia Daulinge amesema mdahalo huo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Sauti Zetu, unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), unaolenga kuimarisha sauti za jamii, hususan wanawake na watoto, katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Amesema kupitia mdahalo huo, Tamwa inalenga kuimarisha ushiriki wa vyombo vya habari katika kuripoti masuala ya ukatili kwa weledi, maadili na mtazamo wa haki za binadamu, huku ikihamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika kuzuia na kupambana na vitendo hivyo vinavyoathiri ustawi wa jamii na maendeleo ya Taifa.

 “Mradi wa Sauti Zetu unalenga kupunguza au kumaliza kabisa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kutumia nguvu ya vyombo vya habari, kwa kuwawezesha wanawake na watoto wa kike kupata elimu, uelewa na taarifa sahihi,” amesema Daulinge.

Wadau wa kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto wakishiriki mdahalo wa pamoja kujadili na kuweka mikakati ya kukabiliana na vitendo hivyo mkoani Tanga.



Kwa mujibu wa Tamwa, Mkoa wa Tanga unaendelea kuongoza kwa idadi ya kesi za ukatili wa kijinsia nchini.

Takwimu za Ofisi ya Ustawi wa Jamii Mkoa wa Tanga kwa mwaka 2023 zinaonyesha kuwa takribani asilimia 33 ya wanawake wamewahi kukumbana na ukatili wa kijinsia au wa kisaikolojia, huku idadi ya matukio hayo ikiongezeka kila mwaka.

Daulinge aliongeza kuwa kwa ngazi ya kanda, mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha inachangia takribani asilimia 83 ya kesi zote za ukatili wa kijinsia katika Kanda ya Kaskazini.

“Hali hii inaonesha ukubwa wa tatizo na hitaji la hatua za haraka na za pamoja kutoka kwa serikali, jamii na wadau wa maendeleo,” amesema.

Amebainisha kuwa changamoto kubwa katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia ni pamoja na ukosefu wa taarifa sahihi, waathirika kuogopa kutoa taarifa, pamoja na upungufu wa elimu kwa jamii kuhusu aina za ukatili na madhara yake.

Wakichangia mdahalo huo, mdau kutoka Community Volunteer Services Tanzania (CVS Tanzania), Simon Mashauri, amesema ukatili wa kijinsia hauwaathiri wanawake pekee bali hata wanaume.

“Wanaume wanakumbwa na ukatili wa kijinsia wa aina mbalimbali unaowaathiri kisaikolojia, ikiwemo kubezwa na familia, kudhalilishwa, kusemwa vibaya, kunyimwa tendo la ndoa kama adhabu na kulazimishwa kuficha maumivu yao,” amesema Mashauri.

Ameongeza kuwa baadhi ya wanaume hupigwa au kudhulumiwa na wenza wao, lakini hushindwa kutoa taarifa kwa sababu ya aibu au hofu ya kuchekwa.

“Ukatili wa kijinsia ni changamoto inayoikabili pia jinsia ya kiume kwa kiwango kikubwa, na tunatamani kuona wanaume nao wakisikilizwa,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Tanga, Inspekta Grace Sandy, amesema makosa yanayoongoza kwa mkoa huo ni mapenzi ya umri mdogo sawa na ubakaji.

“Haya ni makosa ambapo binti anaridhia kufanya tendo la ndoa, lakini kwa mujibu wa sheria umri wake haukubaliki. Asilimia kubwa ya waathirika ni wanafunzi au mabinti wenye umri kati ya miaka 15 hadi 18,” amesema Inspekta Sandy.

Naye Kaimu Afisa Elimu wa Shule za Awali na Msingi Wilaya ya Lushoto, Beatus Kifumo, amesema baadhi ya wazazi huwataka watoto wao kuandika vibaya mitihani ya darasa la saba ili wasifaulu, kwa lengo la kuwaoza au kutokana na sababu za kiuchumi.

“Hili ni ukatili mkubwa kwa ndoto za mtoto na mustakabali wake. Tunaendelea kufanya vikao na wazazi kuwaelimisha kuwa vitendo hivyo ni kosa kisheria na kimaadili,” amesema Kifumo.

Walimu waliokuwepo kwenye mdahalo huo, akiwemo mwalimu wa Shule ya Msingi Kisosora, Peasisi Kitala, wamesema wanafunzi hukumbwa na unyanyasaji kutoka kwa baadhi ya madereva wa daladala.

“Wapo wanafunzi wananyimwa kupanda magari licha ya kuwa na nauli, hali inayohitaji nguvu ya pamoja ya vyombo vya dola na jamii kwa ujumla,” amesema Kitala.