Kahama. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wilayani Kahama mkoani Shinyanga limesema utoaji wa elimu ya majanga na uokozi kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari umechangia kupungua kwa matukio ya majanga, hususan ya moto, shuleni na katika jamii kwa ujumla.
Katika mafunzo hayo, wanafunzi wamefundishwa namna ya kutambua majanga katika hatua za awali, huduma ya kwanza, matumizi sahihi ya vifaa vya maokozi, utoaji wa taarifa za dharura pamoja na umuhimu wa kuwa watulivu na kushirikiana wakati wa majanga.
Mkuu wa Kituo cha Zimamoto na Uokoaji wilayani Kahama, Hafidh Omary, amesema hayo leo Januari 24, 2026, wakati wa mafunzo ya vitendo yaliyotolewa kwa wanafunzi zaidi ya 100 wa darasa la saba wa Shule ya Mtakatifu Anthony wa Padua, yaliyofanyika katika ofisi za jeshi hilo wilayani humo.
Omary amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wa kutoa elimu sahihi ya majanga na maokozi kwa wanafunzi, akieleza kuwa kuwafikia watoto katika umri mdogo husaidia kujenga uelewa wa kudumu kuhusu usalama.
“Mwendelezo wa utoaji wa elimu hii kwa wanafunzi katika Wilaya ya Kahama ni mkakati maalumu tuliojiwekea. Tunaamini elimu inapofika kuanzia ngazi ya chini huleta matokeo chanya zaidi. Samaki mkunje angali mbichi,” amesema.
Ameongeza kuwa kuwajengea uwezo wanafunzi kunawawezesha kuwa na uelewa wa kudumu unaowasaidia kujikinga na majanga, kubaini hatari mapema, kutoa taarifa kwa mamlaka husika na hata kuchukua hatua za awali za kudhibiti majanga kabla hayajaenea.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji likionyesha kwa vitendo jinsi ya kuzima moto jinsi ya kuzima moto. Picha na Amina Mbwambo
Kwa mujibu wa Omary, utekelezaji wa mpango huo umezaa matunda kwa kupunguza kwa kiwango kikubwa majanga ya moto yaliyokuwa yakisababishwa na wanafunzi wakiwa nyumbani kipindi cha likizo au wakiwa shuleni.
“Mafanikio yameonekana wazi. Zamani kulikuwa na matukio ya moto kwenye mabweni au majumbani yanayosababishwa na matumizi yasiyo sahihi ya pasi, kuchezea viberiti au vifaa vya umeme, lakini sasa matukio hayo yamepungua sana kwa sababu wanafunzi wamepata elimu na wanajisimamia,” amesema.
Kwa upande wake, mwalimu wa shule hiyo, Joseph Makaka, amesema wanafunzi wamepata mafunzo kwa vitendo na kuahidi kuwa elimu hiyo itawafikia pia wanafunzi wengine waliobaki shuleni ili kuongeza wigo wa uelewa.
Naye mwanafunzi, Amanda Mbago, amesema elimu hiyo itamsaidia siyo tu katika masomo yake bali pia katika maisha ya kila siku, akisema atakuwa balozi mzuri wa usalama nyumbani na shuleni.
Mwanafunzi mwingine, Bertness Wilbert, amesema wamejifunza umuhimu wa kuepuka matumizi holela ya viberiti, majiko ya gesi na vifaa vya umeme, huku akiomba shule kuwekwa ving’amua moshi ili kugundua moto mapema.