Viongozi Chadema Mbeya waachiwa kwa dhamana, kuripoti tena Polisi

Mbeya. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Mbeya kimethibitisha kuwa baadhi ya viongozi wake waliokuwa wakishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma mbalimbali, wameachiwa huru kwa dhamana.

Walioachiwa ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Masaga Kaloli na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chama hicho (Bavicha), Elisha Chonya ambao watapaswa kuripoti tena Kituo cha Polisi kati ya Jumatatu hadi Jumatano wiki ijayo.

Viongozi hao walikamatwa Januari 21, 2026 katika kijiji na kata ya Inyala, Wilaya ya Mbeya kwa tuhuma za kuhamasisha watu kufanya mkusanyiko isivyo halali.

Hatua hiyo ilifuata baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa za uwepo wa viongozi hao katika eneo hilo wakifanya maandalizi na kuhamasisha watu kukusanyika kufanya mkutano bila taratibu za kisheria.

Akizungumza leo Januari 24, 2026, Katibu wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Hamad Mbeyale amesema viongozi hao wameachiwa jana baada ya kukamilisha taratibu za dhamana na wanatarajia kuripoti kituo cha Polisi Jumatatu hadi Jumatano.

Amesema kwa sasa chama hicho kinaendelea na mipango kuhakikisha Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mbeya, Getruda Lengesela aliyekamatwa usiku wa Januari 22, 2026 kwa makosa ya kijinai ikiwamo uchochezi, kuhakikisha naye anaachiwa huru.

“Tulifuatilia na tunashukuru tulipata ushirikiano mzuri kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi (RCO) ambaye alitutaka turudi Jumatatu, lakini tukamwambia haitawezekana kwa kuwa kuna ratiba ya mwasisi wa chama, Edwin Mtei, akashauri wasizidi Jumatano.

“Kwa ujumla sisi viongozi tunaendelea na mipango kumsaidia Mwenyekiti Getruda aliyebaki huko ili aweze kuruhusiwa pia au shauri lake liende mahakamani ili wanasheria wetu wafanyie kazi,” amesema Mbeyale.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bavicha, Chonya amesema bado hawajui iwapo shauri lao litapelekwa mahakamani au kubaki kwao kwa kuwa wao walitoa maelezo na wanasubiri maelekezo kutoka kwa wadhamini wao.

“Tuliomba washauri letu lipelekwe mahakamani kwa kuwa tulishawasilisha maelezo, lakini tuliomba tusirudi Jumatatu kwa kuwa tutakuwa hatujawa vizuri, lakini tunaendelea na kuenzi kifo cha mwasisi wa chama, marehemu Mtei,” amesema Chonya.