Musoma. Wawekezaji katika sekta ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba wameeleza kukabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo gharama kubwa ya chakula cha samaki na vifaa vya uzalishaji, hali inayotokana na uhaba wa viwanda vya kuzalisha pembejeo hizo ndani ya nchi.
Changamoto hizo zimeibuliwa leo Jumamosi, Januari 24, 2026, mjini Musoma wakati wa ziara ya Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza) mkoani Mara, ziara iliyolenga kuhamasisha Watanzania kuwekeza na kusajili miradi yao kupitia mamlaka hiyo ili kunufaika na vivutio vya uwekezaji vilivyowekwa na Serikali.
Akizungumza katika mkutano huo, mfugaji wa samaki kwa njia ya vizimba, Gambales Timotheo, amesema wawekezaji wengi mkoani Mara hulazimika kuagiza chakula cha samaki kutoka nchi jirani ya Kenya, jambo linaloongeza gharama za uzalishaji na kupunguza faida.
“Tunalazimika kuagiza chakula cha samaki kutoka Nairobi, Kenya, kwa gharama kubwa. Kama kungekuwa na viwanda vya kuzalisha chakula hicho hapa au mikoa ya jirani, gharama zingepungua na fedha hizo zingeweza kutumika kupanua uwekezaji,” amesema.
Kwa upande wake, Charles Makoye amesema pamoja na uhaba wa chakula cha samaki, wawekezaji pia wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa viwanda vya kutengeneza vizimba, hususan vya plastiki, hali inayowalazimu kuviagiza kutoka nje ya nchi kwa gharama kubwa.
“Hivi sasa tumeagiza vizimba kutoka China. Gharama ni kubwa sana, lakini kama kungekuwa na viwanda vya ndani, gharama zingekuwa nafuu zaidi,” amesema.
Akizungumzia changamoto hizo, Kaimu Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Uwekezaji kutoka Tiseza, George Mukono, amesema changamoto zilizopo katika sekta ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ni fursa kubwa za uwekezaji kwa Watanzania, hususan vijana.
Amesema Serikali kupitia Tiseza imeweka vivutio mbalimbali vya uwekezaji ili kupunguza gharama na kuvutia uwekezaji wa ndani, ikiwemo msamaha wa ushuru wa forodha kwa asilimia 100 kwa baadhi ya bidhaa na punguzo la kodi kwa asilimia 75.
“Mwekezaji katika sekta hii anapata nafuu kubwa. Kuna msamaha wa ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazotoka ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na punguzo la kodi kwa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje kwa ajili ya uwekezaji,” amesema Mukono.
Ametaja bidhaa zinazonufaika na vivutio hivyo kuwa ni pamoja na vifaa vya kutengeneza vizimba, nyavu za uvuvi, vifaa na injini za boti, magari yenye majokofu ya kuhifadhi samaki pamoja na vifaa vingine muhimu.
Mukono amesema lengo la Serikali ni kupanua wigo wa uwekezaji wa ndani na kuondoa dhana kuwa uwekezaji ni wa wageni pekee, huku akisisitiza kuwa sekta ya ufugaji wa samaki ina uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira na kuongeza pato la wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Tiseza, Balozi Dk Aziz Mlima, amesema mamlaka hiyo ina mpango wa kuanzisha madawati maalumu ya uwekezaji katika kila mkoa ili kutoa elimu na taarifa kwa Watanzania kuhusu fursa zilizopo katika maeneo yao.
Amesema mkakati huo ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani, akibainisha kuwa mwaka jana kampeni hiyo ilichangia ongezeko la uwekezaji wa ndani kufikia asilimia 51, kuzalisha ajira zaidi ya 160,000 na kuvutia uwekezaji wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 9.3.
“Mwaka huu tumelenga kufanya vizuri zaidi. Hili litawezekana endapo Watanzania watazitumia kikamilifu fursa zilizopo na mazingira mazuri yaliyowekwa na Serikali kupitia Tiseza,” amesema.