668 wabainika kuwa na mabusha Dar

Dar es Salaam. Kati ya wananchi 1,300 waliojitokeza kupima afya zao katika kambi maalumu ya Yombo Kilakala inayotoa huduma hiyo wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam, 668 wamebainika kuwa na ugonjwa wa mabusha na ngiri maji.

  Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe amesema kati ya hao, 457 wamefanyiwa upasuaji na hali zao zinaendelea vizuri.

Dk Magembe ameeleza hayo leo Jumapili Januari 25, 2026 alipotembelea kambi hiyo inayotoa huduma kwa wananchi wenye changamoto ya mabusha, matende na ngiri maji.

“Watu watajiuliza mbona tumeweza kuwahudumia watu namna hii, mchakato huu unatumia njia za kisasa na za kitaalamu. Kwa siku wanaweza wakafanyiwa watu hadi 50,” amesema.

“Utaalamu unaofanyika hapa ni wa hali juu na mgonjwa hawezi kulala siku mbili hapa hospitalini. Hata dawa za usingizi, hapewi zile za mwili mzima bali eneo mahususi analofanyiwa operesheni,” amesema Dk Magembe.

Dk Magembe amesema kambi hiyo imesheheni wataalamu wa afya kutoka wizarani, Muhimbili, Amana, Temeke, Mwananyamala na Tamisemi ili kuwajengea uwezo watumishi kwa kada hiyo.

Katikati ya kambi hiyo, Dk Magembe amefichua kuna wagonjwa takribani 400 walibainika maradhi yao hayahusiani na ngiri maji wala mabusha bali ngiri kokoto (henia).

“Tumeamua wale wote waliokuja katika kambi na kugundulika na magonjwa mengine tofauti ikiwemo henia, tutawahudumia pia.

“Tukimaliza hawa wa ngiri maji na mabusha, tutaweka utaratibu wa kuwahudumia. Niwaombe tuwe na subira tutaendelea nao, ingawa baadhi yao tumeshaanza kuwapa huduma,” amesema Dk Magembe.

Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe akizungumza na wanahabari alipotembelea kambi ya kutoa huduma ya uchunguzi kwa wananchi wanaosumbuliwa na mabusha na ngiri maji iliyopo Yombo Kilakala wilayani Temeke.



Kutokana hilo, Dk Magembe ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam na mikoa jirani kujitokeza wanaposikia kuna kambi zinazotoa huduma ili kupata matibabu.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Mohamed Mang’una amesema kambi hiyo ilianza Januari 5, 2026 na itahitimishwa Januari 30, 2026 akisema kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wananchi.

“Kumekuwa na mwitikio mkubwa uliotokana na uhamasishaji uliofanyika kwenye masoko na maeneo yenye mchangamano wa watu,” amesema Dk Mang’una.

Kwa mujibu wa Dk Mang’una, watu wenye umri wa kuanzia miaka 45 na kuendelea ndio wanaongoza kupata changamoto hiyo kwa waliofanyiwa uchunguzi

Mmoja wagonjwa waliopatiwa matibabu, Faki Mussa anayeishi Buza wilayani Temeke, ameishukuru Serikali kupata matibabu hayo bure baada ya kuhangaika na ugonjwa huo kwa miaka 10.

“Operesheni nimefanyiwa Januari 14, tumehudumiwa vizuri na leo nimekuja kwa ajili ya kufanyiwa ukaguzi.

“Wito wangu wenye changamoto msiogope kuja hospitali, jitokezeni ili mpatiwe matibabu na kuishi vizuri,” amesema Mussa.